Na Saleh Ally
SUALA
la uchaguzi wa Simba uliopangwa kufanyika keshokutwa Jumapili limekuwa na
vipingamizi vingi hapa katika, likiwemo lile suala la baadhi ya wanachama wake
wachache kuamua kwenda mahakamani kuusimamisha.
Kama
kuna wanachama wa Simba watakuwa wanakubaliana nami kuwa uchaguzi huo lazima
ufanyike, iwe keshokutwa Jumapili au siku nyingine, basi wao wanapaswa
kujipanga kwa hesabu za kuchagua viongozi sahihi kwa klabu yao.
Nimeamua
kuandika Hoja Yangu leo nikilenga suala la nani achaguliwe ikiwa ni sehemu ya
niliyoyaona kwenye uchaguzi uliopita na mingine baadhi ya klabu hiyo au
nyingine ambayo uchaguzi wake wa viongozi umekuwa ukisababisha matatizo kadhaa,
nitafafanua.
Wakati
wanachama wanakwenda kwenye uchaguzi, utaona wengi wamekuwa wakiangalia nafasi
za juu nani hasa atakuwa kiongozi. Mfano mwenyekiti na makamu wake na sasa kwa
Simba itakuwa ni rais na makamu wake.
Nafasi
ya rais kwa sasa inagombewa na Evans Aveva na Andrew Tupa, makamu wa rais ni
Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Sued Nkwabi.
Nafasi
hizo mbili za juu ndiyo zimekuwa jicho, kila mtu anataka kujua nani atachukua
nafasi hiyo na itakuwaje lakini si lahisi kusikia nafasi za wajumbe
zinazungumziwa kwamba nani atachukua.
Kuzidharau
nafasi za wajumbe ni kosa kubwa, huenda wengine wamewahi kulifanya huko nyuma
na hawakujua lilikuwa ni tatizo kubwa kiasi kutokana na wao kutokuwa makini
wakati wa kuchagua wajumbe.
Wajumbe
hao wataingia kwenye kamati ya utendaji, maana yake ndiyo watakaokuwa
wakipitisha mambo yote makubwa yanayohusiana na klabu pamoja na kikosi cha
SImba. Hivyo lazima wawe watu imara, wenye fikira pevu, ‘fikira jenzi’ na
wanaotaka maendeleo ya dhati kwenye klabu hiyo.
Hakuna
anayeweza kunikatalia kwenye uchaguzi wa klabu hizi kubwa, wako wanaotaka
kuingia kwa ajili ya kujinufaisha wao, wanaotaka kuonekana tu, wanaofuata
mkumbo na wengine wanajua hawana uwezo wa kuongoza, lakini watataka tu
wagombee.
Wanachama
wa Simba watakuwa wanawachagua watu wanaowajua, wanaishi nao, majirani zao,
wanajua habari zao, hivyo wanapaswa kuwa makini kwenye kuamua badala ya kufanya
kwa kufuata mkumbo au kubahatisha.
Uchaguzi
wa kishabiki pia umekuwa ni tatizo kubwa katika matokeo ya uchaguzi mwinhi
katika klabu au mashirikisho ya michezo mbalimbali nchini. Mwisho wake ni
kuchagua watu kwa kubahatisha na iingie kwenye kipindi kigumu kwa miaka minne.
Kama
rais na makamu wake watakuwa watu imara, halafu Simba ikawa na wajumbe ilimradi
na watu waliwachagua kishabiki au kwa kufuata mkumbo, mwisho wake wawili hao
imara wanakuwa kwenye mzigo mkubwa.
Kulahisisha
mambo, lazima kutokuwa na wajumbe mizigo kwenye klabu hiyo. Hivyo wanachama
ndiyo watakuwa na kazi kubwa kwenye uchaguzi huo kuhakikisha Simba haiangukii
kwenye wajumbe mizigo.
Wanachama
ndiyo wenye uamuzi wa mwisho kuhusiana na nani au yupi awe kiongozi wa klabu
yao. Hakuna atakayekuwa anataka kupiga kura kumchagua kiongozi ambaye
ataiangusha iingie kwenye matatizo.
Hivyo
kitu cha kwanza ni kuepusha viongozi au wajumbe mizigo ambao watakuwepo, hawana
mchango wowote, kazi yao kupiga majungu na kawaida, watu wengi wenye uwezo
mdogo kwenye kuamua mambo makini au kutatua mambo magumu, wana tabia za majungu
na kuanzisha migogoro.
Wengi
wenye uwezo mdogo wa kujibu hoja, hukimbilia maneno mengi, wana tabia za
kulaumu sana, wanaamini wameonewa na ndiyo wamekuwa matatizo makubwa hata kwa
Simba yenyewe. Hivyo mkichagua kwa umakini viongozi wenu wa juu, basi msipuuze
umuhimu wa kuchagua wajumbe imara pia ili kuunda uongozi imara.
Kila
la kheri Jumapili.
0 COMMENTS:
Post a Comment