MAREHEMU MZEE SMALL, MAMA SAID NA SALEH ALLY |
Na Saleh
Ally
TAKRIBANI
miezi sita kulizagaa taarifa kuhusiana na kifo cha msanii maarufu wa maigizo na
vichekesho, Said Ngamba maarufu kama Mzee Small.
Lakini
sasa hatuko naye baada ya kufikikwa na mauti juzi saa 4 usiku alipokuwa
amelezwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
SALEH ALLY AKIWA NA MAREHEMU MZEE SMALL WAKATI WA UHAI WAKE |
Nakumbuka
siku hiyo ilikuwa takribani saa 6 usiku, nikaamua kufanya juhudi za kutaka
kuhakikisha pamoja na kwamba taarifa hizo zilikuwa zimezagaa katika mitandao ya
kijamii pamoja na blogu mbalimbali.
Nilihofia
kuzungumza na mkewe, nilimtafuta mmoja wa wanaye ambaye alinieleza kushangazwa
na taarifa hizo lakini mzee wake alikuwa hai ingawa alikuwa mgonjwa.
Kwa kuwa
nilihakikishiwa kuhusiana na hali yake, sikuwa na hofu tena ya kupiga simu
yake, nilipopiga simu ya Mzee Small alipokea mkewe, nimezoea kumuita mama Said.
Mama
Said alinilieleza kuwa mumewe kweli ni mgonjwa lakini hakuwa na hali mbaya na
walikuwa wote wamelala. Kwa kuwa nimezoena na mke wa Mzee Small, nilimuambia
siamini hadi nitakapozungumza naye.
Nilimsikia
anamuamsha, mwisho Mzee Small alichukua simu na kuanza kuzungumza na mimi.
Lakini kilichotokea, hakunikumbuka, alionekana wazi amenisahau, nilishangaa,
nikaumia lakini nikawaza haiwezi kuwa kawaida, lazima atakuwa anaumwa.
Siku
iliyofuata, niliondoka ofisini nikiwa nimeongozana na timu ya vijana wa
Championi kwenda kupatafuta nyumbani kwa Mzee Small eneo la Tabata, pamoja na
urafiki wangu na mzee huyo kwa takribani miaka 12, sikuwa nimewahi kufika
nyumbani kwake.
Nilianza
kufahamiana naye wakati nikiwa Habari Corporation, baadaye nikahamia Mwananchi
na alikuwa na kawaida ya kupita ofisini pale Tabata Relini na kunisalimia.
Siku
hiyo, tulijitahidi hadi tukafanikiwa kufika nyumbani kwake. Lakini tuliambiwa alikwenda
hospitali ambako amekuwa akifanyishwa mazoezi baada ya kupata nafuu kubwa
kutokana na mwili wake kupooza upande mmoja, nakumbuka wa kulia.
Hivyo
mimi, wenzangu kutoka Championi tuliendelea kumsubiri na mara ya kwanza namuona
tena Mzee Small, alifika akiwa kwenye pikipiki, nakumbuka alikuwa amevaa jezi
ya zamani ya timu ya taifa, Taifa Stars.
Majirani
walimpokea kama mbunge, wakamsaidia kuteremka kwenye pikipiki naye akaanza
kuwatania akiwaita ni wachumba zake. Mwisho aliinua uso na kuniona, alishituka
sana.
Hisia za
urafiki wetu zilikuwa kwenye macho yake, alionyesha kushangazwa na kuniona pale
na wala hakuwa akikumbuka kama tulizungumza usiku wa kuamkia siku hiyo lakini
akanieleza alitaka kunyoa ndevu kwanza, halafu baada ya hapo ndiyo tungezungumza.
Nilimsubiri
kwa takribani dakika 20, ananyolewa huku akinipa stori na baada ya hapo,
akaniomba tuongozane kwenda nyumbani kwake ambako alitununulia wote soda na
baada ya hapo stori kuhusiana na kuzushiwa kifo zikaanza.
Katika
mengi tuliyozungumza huku akimsisitiza mkewe kuwa mimi ni kati ya wanaye, Mzee
Small aliniambia maneno hayo: “Siku itafika, najua lazima nitakufa kwa kuwa
mimi ni mwanadamu, siwezi kukwepa.”
“Lakini
kama nitatangulia, basi andika, waambie ndugu zangu wasimtese mke wangu kwa
kuwa huyu ndiye ndugu yangu namba moja na amepigana sana kunisaidia. Utaona
usiku, mchana na kila siku niko naye.
“Mimi
nina nyumba hii na kuna nyingine ambayo anaishi mwanangu, sasa sitaki kusikia
wanamyanyasa huyu mama kwa kuwa naye amekuwa akijitolea katika ujenzi. Nasema
hizi ni nyumba zangu na mke wangu.
“Usije
ukasema Mzee Small amechanganyikiwa, nasema kwa kuwa najua. Kuna baadhi ya
ndugu zangu sasa hawazungumzi na mke wangu, wanasema eti ameniroga mimi, hiki
ni kichekesho. Lakini bado siwaoni kunisaidia, hivyo nikifa uwaambie, yule mzee
wangu alisema msimnyanyase mke wake.”
Hiyo
ilikuwa ni mara ya mwisho mimi kumuona tena Mzee Small, lakini tulikuwa
tukiendelea kuwasiliana kwa simu mara kadhaa nikitaka kumjulia hali na wakati
mwingine yeye ndiye alinipigia na kutaka kujua ninaendeleaje.
Juzi saa
moja usiku, Mama Said alinipigia simu na kuniambia: “Baba yako ni mgonjwa,
amezidiwa sana, sasa niko kwenda daladala narudi nyumbani, nimemuacha Muhimbili
lakini amekata kauli na anakoroma tu.”
Siko Dar
es Salaam, nisingeweza kwenda hospitali, lakini nilishituka na kupata hisia
mbaya, lakini nikamuachia Mwenye Mungu kwa kuwa najua ni mwingi wa rehema na
mwenye kurehemu.
Asubuhi
ya jana nilipata taarifa za kifo cha Mzee Small ambaye alifariki saa 4 usiku,
saa tatu tu baada ya mimi kuwa nimewasiliana na mkewe Mama Said ambaye
alipambana katika shida zote za mzee wetu.
Kila
kitu majaaliwa, sitamzika Mzee Small ambaye anayezikwa leo saa 10 kama
nilivyotaarifiwa. Najua haya pia ni majaaliwa, ila ninaumia lakini sina uwezo wa kutengua uamuzi wa Mwenyezi
Mungu.
Mzee
Small aliniahidi, pindi atakapopata nafuu tu, basi atafunga safari na
kunitembelea katika ofisi za Championi ndani ya Global Publishers kama
alivyokuwa akifanya nilipokuwa nikilisukuma Mwanaspoti ndani ya Mwananchi.
Lakini hajakuweza, bado naamini, yote ni majaaliwa.
Ninaamini
nimefikisha ujumbe wake alionipa kuwaeleza ndugu na jamii. Pole zangu kwa
familia na mashabiki wake, lakini niwakumbushe, machozi hayatatosha kumuenzi
Mzee Small, alichokifanya kwenye kazi zake ndiyo kienziwe.
Mi nasema ujumbe haujawafikia walengwa,andika hii makala katika gazeti na copy kama 20 upeleke nyumbani pale.......ingependeza wakati huu bado msiba upo au vizia wakati wa 40.....alikuambia sababu alijua sauti yako kwa maana ya kalamu itawafikia wengi...ni hayo tu
ReplyDelete