Uongozi wa timu ya Mbeya City ya jijini Mbeya, umefunguka
kuwa haupo tayari kuuza mchezaji wao yeyote kwa dau lolote watakaloahidiwa na
timu kubwa za Simba, Yanga na Azam.
Timu mbalimbali zimekuwa zikiwanyemelea wachezaji wa Mbeya
City kufuatia uwezo waliouonyesha kwenye ligi msimu uliopita.
Wachezaji ambao wametajwa kuwa wanaweza kusajiliwa na timu
hizo ni Saad Kipanga, Paulo Nonga, Hassan Mwasapili.
Katibu wa Mbeya City, Emmanuel
Kimbe, alisema kwa upande wao
fedha sio tatizo la kuwaruhusu wachezaji wao kusajiliwa na timu nyingine na
badala yake wanachokihitaji wao ni kuona wachezaji wao wanabakia klabuni hapo
msimu ujao.
“Hatuna mpango wa kuwaruhusu wachezaji wetu kwenda kokote
hata kama klabu itakuja na dau la kiasi gani, hatuwezi kuwaruhusu wachezaji
wetu kuondoka.
“Fedha siyo msingi, msingi kwetu ni wachezaji kwani hatupo tayari
kupokea kiasi chochote cha fedha, tunachohitaji ni kubaki na wachezaji wetu tu.
“Kuhusu kambi tunatarajia kuingia mwanzoni mwa mwezi Julai kwani
kwa sasa wachezaji wamepumzika kutokana na michuano ya Nile Basin waliyotoka
kushiriki nchini Sudan,” alisema Kimbe.
0 COMMENTS:
Post a Comment