Wakati mamilioni ya Watanzania wakifuatilia Fainali za Kombe la
Dunia nchini Brazil, Shirika la kutetea haki za watoto la Plan International
limeingia ubia na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya
kutetea na kuhamasisha juu ya ulinzi wa haki za mtoto hapa nchini.
Kwa lengo hilo, mkataba wa ushirikiano umesainiwa leo katika
ofisi za makao makuu ya TFF jijini Dar es Salaam baina ya Mkurugenzi wa Plan
International Tanzania, Jorgen Haldorsen na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Ushirikiano huo unalenga kufanya kazi pamoja katika kushughulikia masuala ya
ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni.
Kwa mujibu wa Haldorsen, mchezo wa mpira ndio unaoongoza nchini
na kote duniani kwa kuwa na ushabiki mkubwa na kwamba joto kali juu ya Fainali
za Kombe la Dunia linaloendelea Brazil ni ushahidi tosha.
“Tunatambua uwezo wa mchezo huu wa kuwajumuisha watu. Sasa
tunataka tuwajumuishe watu sio tu kwa ajili ya furaha lakini pia kama njia ya
kuleta mabadiliko juu ya usawa wa kijinsia kwa kutetea na kuhamasisha juu ya
haki za mtoto wa kike,” aliongeza.
Mkurugenzi huyo alidokeza kuwa ushirikiano na TFF ni sehemu ya
kampeni ya kimataifa inayoendeshwa na shirika hilo kote ulimwenguni inayoitwa ‘Because
I Am A Girl’-BIAAG au kwa Kiswahili- KWA SABABU MIMI NI MSICHANA ambayo
inalenga kuwatoa mamilioni ya wasichana kutoka katika umaskini kupitia
uhamasishaji juu ya haki zao, elimu na stadi za maisha.
“Kwa kupitia ubia huu tutakuwa na uwezo wa kuwafikia mamilioni
ya Watanzania na tutawapa wasichana ujumbe kuwa KWA SABABU MIMI NI MSICHANA,
lazima nipate fursa sawa na wavulana. KWA SABABU MIMI NI MSICHANA, lazima niwe
na uwezo wa kufunga magoli ya kufikia ndoto zangu katika maisha,” Haldorsen
alieleza.
Kwa upande wake, Rais wa TFF, ambaye ni mjumbe katika Kamati ya
Huduma kwa Jamii ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulimwenguni- FIFA,
alisema kuwa ubia huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera za huduma kwa jamii ya
TFF na kwamba wana furaha kushirikiana na Plan International kwa lengo hili
muhimu.
“Ushirikiano huu ni muhimu sana kwetu kwani unakileta chombo
kikubwa kabisa cha michezo hapa nchini pamoja na shirika la Plan International
hususan kwa ajili ya haki za mtoto wa kike. Tunategemea kutumia mtandao wetu
nchi nzima kuelimisha juu ya usawa wa kijinsia na uhamasishaji wa haki za mtoto
wa kike,” alisema Rais Malinzi.
Kwa pamoja tutashughulikia masuala ya usawa wa kijinsia, hususan
kupambana na ndoa za utotoni ambazo zinawazuia mamilioni ya watoto wa kike
nchini wasiweze kumaliza shule, kufikia ndoto zao katika maisha, na vile vile
kuwaacha waendelee kuteseka katika umaskini,” Rais Malinzi aliongeza.
KUHUSU PLAN INTERNATIONAL: Plan International ni
shirika la kimaendeleo la misaada ya kibinadamu, linalomlenga mtoto
lisilofungamana na mrengo wowote wa kidini, kisiasa au kiserikali.
Plan
International ilianzishwa zaidi ya miaka 70 iliyopita na inaendesha shughuli
zake katika nchi 70 duniani. Plan International imekuwa inafanyakazi hapa
Tanzania tangu mwaka 1991 ikiwasaidia watoto na jamii kupata huduma za afya,
elimu, maji, usafi na mazingira, kujikimu na ulinzi. Inaendesha miradi Dar es
Salaam, Morogoro, Dodoma, Geita, Pwani, Mwanza na Rukwa.
KAMPENI YA KWA SABABU MIMI NI MSICHANA –BIAAG: Kampeni ya Kwa Sababu Mimi ni Msichana-BIAAG (2012-2016) ni
kampeni ya Plan ulimwenguni kote inayolenga kuelimisha na kutetea haki za mtoto
wa kike na kuwatoa mamilioni ya wasichana kutoka kwenye lindi la umaskini
kupitia elimu na utoaji wa stadi za maisha na kazi.
Kampeni hii
inalenga kupambana na ubaguzi wa kijinsia na kuboresha maisha ya wasichana
milioni 4 duniani na zaidi ya laki 3 hapa Tanzania kwa kuwawezesha kujiunga
shuleni, kupata stadi za kiufundi na maisha, kujikimu, na kushiriki katika
shughuli mbalimbali katika jamii na kulindwa, kwa kukabiliana na vikwazo dhidi
ya maendeleo ya mtoto wa kike.
0 COMMENTS:
Post a Comment