WAKATI
fulani niliwahi kuzungumzia kuhusiana na namna ambavyo Simba inaweza kufanya
mambo yake yakabadilika katika kipindi kifupi, lakini zaidi nikazungumzia suala
la umoja.
Lakini siku
chache baadaye, aliyekuwa mgombea wa Urais wa Simba, Michael Wambura akaibuka
hasa baada ya Rais wa Simba, Evans Aveva kusema watamjadili Wambura kwenye
mkutano mkuu wa Simba.
Wambura
anapinga kujadiliwa kwa kuwa anaamini uanachama wake sasa ni sahihi kwa kuwa
kamati ya rufaa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilimsafisha baada ya kuwa
ameondolewa na kamati ya uchaguzi.
Kamati ya
uchaguzi chini ya Dokta Damas Ndumbaro ilimuondoa kwa madai unachama wake una
mushkeli na kila kitu kikawekwa wazi. Kamati ya rufaa ilipokutana, ikaamua tena
kwa kupiga kura za vidole kwamba Wambura alikuwa mwanachama halali.
Hapo ndiyo
hoja ya Wambura kuhusiana na kutaka kujadiliwa, lakini bado kamati ya rufaa ya
TFF haiwezi kuwa mwamuzi wa mwisho kuhusiana na uanachama wa Wambura. Yoyote
anaweza asiiamini ndiyo maana hata baada ya kusisitiza Wambura alifanya kampeni
nayo ikaungana na ile ya uchaguzi kumfuta ugombea, kuna wanachama wamekwenda
mahakamani.
Wanachama wa
Simba waliokwenda mahakamani ni wale waliofurahia mara ya kwanza kurudishwa kwa
Wambura kupitia kamati hiyo ya rufaa ya TFF. Safari ya pili ilipobaini kweli
Wambura ana makosa na kuishindilia adhabu aliyopewa, wanachama haohao
hawajaiamini na wamekwenda mahakamani.
Hivyo hata
Simba pia wanaweza kujiridhisha na kama suala lake litajadiliwa na wanachama,
basi litakuwa zuri zaidi kwa kuwa hata wale waliokuwa wanapinga taarifa za kuwa
wanachama wake una walakini watakuwa na nafasi ya kuzungumza mbele ya wenzao na
mwisho hilo litapata mwafaka.
Wambura
anaweza kuwa kati ya viongozi wanaohitajika kwenye soka, lakini kuna mambo
kadhaa likiwemo hilo la unachama anaweza kulifanyia kazi ikiwezekana kabla ya
kugombea tena.
Lakini kwa
Aveva, lazima ajikumbushe kwamba ana mambo mengi sana ambayo ni dhamana
aliyopewa na Wanasimba ambao wamemuamini ili awondoe katika machungu na hali ya
mambo kuwa sintofahamu kama ilivyokuwa kwa uongozi uliopita.
Vizuri nguvu
nyingi za anayotaka kufanya azielekeze kwenye maendeleo ya Simba ambayo
imekwama kwenye tope. Uzito yaani ukubwa wa klabu hiyo unahitaji gia kubwa,
hivyo lazima kuwe na umakini na juhudi za juu kufanikiwa katika hilo.
Aveva hana
haja ya kushika mbili ili moja isije ikamponyoka kwa kuwa lengo kubwa sasa ni
kuipeleka Simba kwenye mabadiliko na baadaye mafanikio na ndicho wanachosubiri
Wanasimba.
Wapiga
kelele hawatakosekana, wako ambao wamekuwa wakisema wanapambana kwa ajili ya
maslahi ya Simba, lakini ukweli wao wanapigania maslahi ya matumbo yao kwa kuwa
klabu kama Simba, kwao ni mitaji.
Wako
wanaolazimisha vurugu ili walipwe wakati wa kipindi cha vurugu, lakini wako
ambao wamekubali kuwa wapambe, ili mradi kuendesha tu maisha yao na si faida ya
maisha ya klabu lakini mazungumzo yao wanasema wanaipenda Simba.
Aveva
amepata kura za wanacham wengi zaidi, mashabiki wengi wanamkubali, hivyo
kuendeleza malumbano na upande mwingine ni kuwapa nafasi wanaotaka afeli ili
aseme, waonekane wameshinda.
Lazima
kuangalia zaidi kuhusu malengo, nini cha kufanya kikosi cha Simba kiimarike na
kuwa bora, lakini mipango ikiwezekana hadi ya miaka kumi ijayo kuisaidia Simba kupita
kwenye reli sahihi.
Aveva
anaweza kuamini ule msemo wa “kelele za chura…” halafu akaendelea na mambo
ambayo yanahusu maendeleo ya Simba. Lakini kikubwa zaidi ni kujitahidi
kudumisha umoja kwa wale watakaokuwa wanakubaliana nao na kutenda hadi miongoni
mwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo.
Kwa
wanachama wanaompinga, pia wanapaswa kufanya mambo kwa kuangalia kipi hasa ni
sahihi kwa kuwa Simba inataka mabadiliko kwenda mafanikio. Wanaotaka
kulazimisha migogoro ili wafaidike kwa kisingizio kuwa wanaipenda Simba, nao ni
tatizo pia.








0 COMMENTS:
Post a Comment