UONGOZI wa
Simba chini ya rais wao mpya, Evans Aveva, wametangaza kamati yao ya usajili
ambayo itahakikisha inamalizia kwa uhakika zoezi la usajili.
Kamati ya
usajili ya Simba ina watu wazito, mfano hawa wanne ambao ni wakongwe katika
Kundi la Friends of Simba (FOS) kama Kassim Dewji, Crescentius Magori, Musley
Al Rawah, Zacharia Hans Pope, pia kuna Rodney Chiduo na Said Tully.
Ukiangalia
watu hao, hakuna ubishi watakuwa makini kwa kuwa wamekuwa mara nyingi kwenye
kamati za usajili au zile zinazohusisha masuala ya wachezaji au mashindano
mbalimbali. Lakini ni watu ambao wako tayari kupoteza muda na hata fedha zao
ili kufanikisha malengo ya wanachokitaka kwa ajili ya usajili bora wa kikosi
chao, hilo ni jambo bora kabisa.
Kwa upande
wa Yanga, wao wamekuwa wakitumia zaidi kamati ya mashindano ambayo pia hufanya
kazi ya usajili wa wachezaji ambao baadaye huitumikia Yanga kwa lengo la
kuhakikisha inashinda mechi zake na kupata mafanikio.
Kamati hiyo
inajulikana katika usajili wake, imefanikiwa kuwapata wachezaji kadhaa nyota
ambao walikuwa wanawaniwa na timu nyingine kama Azam FC au Simba.
Ushindani wa
usajili wa wachezaji kutoka timu mmoja kwenda nyingine unazidi kuwa mkubwa
upande wa klabu hizo kongwe na ili ziendane na wakati lazima mambo ya kitaalamu
yapewe nafasi.
Ninapozungumzia
utaalamu, sizungumzii ulee ambao unapewa jina la kamati ya ufundi. Nazungumzia
taalum ya soka ambayo watu watakuwa wameingia darasani ya kuisomea.
Kamati hizo
mara chache zimekuwa zikipata nafasi ya kuwauliza makocha wanachotaka. Lakini
mara kadhaa zimekuwa zikikiuka ripoti za makocha na kufanya usajili kulingana
na zinavyoamini.
Yote
yanawezekana lakini kufanya mambo yaende kitaalamu zaidi, lazima kuwe na mmoja
wa wajumbe ambaye ana taalum ya ukocha na ingekuwa vizuri zaidi Yanga na Simba
zikaanzisha utaratibu wa kuwa na makocha wasaidizi ndani ya kamati hizo.
Kocha
msaidizi atakuwa na nafasi ya kuwa daraja kwa kuwa atafanya mawasiliano na bosi
wake ambaye ni kocha mkuu na pia atafanya hivyo kwa wajumbe wa kamati ya
usajili.
Pia kocha
huyo msaidizi atakuwa na nafasi nzuri ya kutoa ushauri wa kiufundi ndani ya
kamati hiyo.
Mapendekezo
yanaweza kuwa yake kwa mujibu anavyoiona yeye lakini pia baada ya kuwa amekaa
na kocha mkuu na kujadiliana naye.
Maana yake
atakachokuwa akikiwasilisha kinaweza kuwa kile ambacho amekubaliana na bosi
wake ambaye ni kocha mkuu. Hali hii itasaidia mambo mengi sana na taratibu
itarudisha mambo kwenye mstari.
Kwa kocha ni
rahisi kujua sifa nyingi zaidi za mchezaji, mfano faida zake anapokuwa anatumia
miguu yote. Wepesi au uzito wake, kiwango cha upigaji mashuti, vichwa na mambo
mengine.
Lakini bado
kocha ana uwezo wa kujua kuhusiana na mchezaji ambaye sasa anaonekana hayuko
katika kiwango kizuri, bado akasajiliwa kwa ajili ya kumboresha na kuamini
atakuwa bora zaidi, yote hayo yanawezekana.
Kwa kifupi,
kamati hizo za usajili zinaweza kufanya mambo yake kwa mpangilio wa juu zaidi
kama zitakuwa na watalaamu ambao watasaidia mambo kwenda kitaalamu kuliko kwa
uzoefu pekee.
Dewji, Magori,
Musley ni kati ya wale walioanza kazi hiyo kitambo, utaona walishiriki katika zile
enzi cha kikosi cha Simba kilichokuwa kinasumbua mfano mwaka 2003.
Lakini sasa
ni kipindi cha utaalamu zaidi, pamoja na kwamba wanajua, lakini ushauri wa
kitaalamu unaweza kuwasaidia wakiwa ndani ya vikao vyao na watatimiza vyema
malengo yao. Hata kama wanapata mawazo ya makocha, basi vikao vyao bado
vinawahitaji hao makocha.
0 COMMENTS:
Post a Comment