July 4, 2014




Na Saleh Ally
SHOO ya kwanza ya robo fainali ya Kombe la Dunia inatarajiwa kuanza leo Ijumaa wakati wenyeji Brazil watakapokuwa wakipambana kuwang’oa Colombia walioonyesha kushangaza wengi kutokana na kikosi chao imara.


Colombia wamefikia robo lakini wakiwa na rekodi nzuri hatua ya makundi, walitokea Kundi C ambako walishinda mechi zao zote tatu dhidi ya Ugiriki (3-0), Ivory Coast (2-1) na Japan (4-1).

Katika hatua ya 16 Bora, wakakutana na Uruguay na kuichapa kwa mabao 2-0, hivyo kuwa na rekodi ya kushinda zaidi ya bao moja katika mechi zao zote nne walizocheza.

Brazil wanajua watakuwa na kazi kubwa kupambana na Colombia lakini gumzo la mchezo wa leo ni watu wawili, Neymar na James Rodriguez.

Vijana wote hao wamerudi nyumbani kuzipigania timu zao za taifa, ingawa wanatokea barani Amerika Kusini lakini wote wanafanya kazi barani Ulaya, Neymar akiwa na FC Barcelona ya Hispania na Rodriguez akikipiga katika kikosi cha matajiri wa Ufaransa, AS Monaco.

Mashabiki wanaozungumza Kihispaniola, wamelalamika kuona Rodriguez anatumia jina la Kiingereza katika jezi yake na wao linawatatiza kulitamka. Wengi wanatamka Hamez, lakini hakuna mwenye hofu na kinda huyo.

Tayari amepachika mabao matano na ndiye anaongoza wakati Neymar ana manne katika nafasi ya pili, sawa na Lionel Messi wa Argentina na Thomas Muller wa Ujerumani.

Shoo itazidi kuwa kali kwa kuwa Neymar ana jina kubwa, lakini Rodriguez amefanya vitu vikubwa zaidi. Achana na kufunga tu, Mcolombia huyo anaongoza kwa kupiga mashuti mengi yaliyolenga lango akiwatupa mbali nyota wa dunia kama Messi, Muller, Cristiano Ronaldo, Karim Benzema na Neymar.

Mashuti yake yamelenga kwa asilimia 88, Neymar ni asilimia 82, utaona wawili hao licha ya kufukuzana vibaya, lakini wamewazidi nyota kadhaa kama Benzema mwenye 68%, Muller 55% na Messi mwenye 46%.

Nani atakuwa shujaa wa taifa lake na tayari wachambuzi wa Amerika Kusini wanaamini Colombia ina nafasi na iwapo itavuka hapo, inaweza kufika fainali na kubeba Kombe la Dunia.

Takwimu za utendaji kazi, kwa maana ya kasi, mashuti, pasi na nyingi za kiufundi zinaonyesha wawili hao hawana tofauti kubwa. Kimahesabu Neymar anakuja juu zaidi na hata uzoefu anao.

Burudani nyingine ni kwamba, wote, kila mmoja umri wake ni miaka 22 lakini ndiyo tegemeo la taifa. Gazeti moja la Colombia limeandika: “Watoto tegemeo wa mataifa.” Likimaanisha wawili hao watakaotupiwa macho na wengi, watafanya nini kuyasaidia mataifa yao.

Hakuna anayeweza kufanya kazi pekee, kama ni msaada, Neymar ana watu wenye uwezo mkubwa kumsaidia kufanya kazi kama Oscar au Hulk, bado Rodriguez naye ana nafasi pia ya kufanya vizuri kwa kuwa ana sapoti ya wakali kama Juan Cuadrado, rasta hatari sana huyu na Jackson Martinez.
Wakati Colombia walipopata uhakika kwamba nyota wao, Ramadel Falcao hatakuwa katika kikosi hicho, hofu ilitawala na Fred Guarin anayekipiga Inter Milan ndiye alionekana mchezaji maarufu zaidi na tegemeo. Sasa gumzo na tegemeo ni Rodriguez.
Takwimu ni jambo moja, katika soka mambo yanaweza kubadilika wakati wowote, wa juu akawa chini. Hivyo majibu ya maswali yatapatikana pale mwamuzi atakapopuliza kipenga.

Rodriguez:
Shambulizi 80%
Ubunifu 83%
Ulinzi 51%
Kontroo 85%
Kukokota 86%
Umaliziaji 78%
Stamina 73%
Kasi 81%
Mashuti 79%

Neymar:
Shambulizi 84%
Ubunifu 76%
Ulinzi 43%
Kontroo 91%
Kukokota 92%
Umaliziaji 84%
Stamina 86%
Kasi 89%
Mashuti 77%

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic