July 26, 2014



NI takriban mwezi mmoja kabla ya pazia la michuano ya Ligi Kuu Bara kufunguliwa, tayari kushuhudia uhondo wa miezi nane mingine, baada ya kuukosa kwa miezi minne ya mapumziko.


Ni miezi mahususi kumpata bingwa, ambaye atarithi taji hilo kutoka kwa Azam au Azam waendelee kulishikilia.
Yapo mengi yatakayojili, lakini ni historia ya soka la Bongo kuwa na nyota kutoka Mali na Brazil, mataifa ambayo hatujazoea kuchukua wachezaji. Azam kuna Mmali Ismail Diara kama ilivyo kwa Yanga na Wabrazili Andrey Coutinho na Genilson Santos ‘Jaja’ ambapo ni mara ya kwanza Yanga kuwa na wachezaji kutoka nchini humo.

Lakini pia Azam inaweza kuweka rekodi ya kuwa na nyota kutoka Amerika ya Kati, Leonel Saint-Preux anayetokea Visiwa vya Haiti, vinavyopakana na Jamhuri ya Dominica. Hii itakuwa ni rekodi ya aina yake kwa Bongo.
Lakini kwa upande wa pili, msimu wa 2014/15, kuna wachezaji ambao hakika tutayamiss majina yao.
Ifuatayo ni orodha ya nyota ambao ni vigumu kuwaona katika msimu ujao na kama ikitokea ni asilimia moja kati ya mia.


10. Amani Simba
Mmoja wa makipa waliojijengea majina makubwa katika soka la Tanzania kwa miaka mingi, katika klabu mbalimbali. Ameshapita katika klabu kama Simba, Kagera Sugar, Moro United, Reli Morogoro na timu ya taifa kwa vipindi tofauti, katikati ya msimu uliopita alikuwa na kikosi cha Ashanti United, alitangaza kuachana na soka, kwa kile alichobaini kuwa ni muda muafaka kukaa na familia yake.

9. Vituko vya Mhe Ismail Aden Rage ‘Tutu Vengere’
Ni mtu mwingine, ambaye hakika umati wa wanasoka Tanzania utamkumbuka. Ismail Aden Rage, aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba na Mbunge wa Tabora Mjini, alikuwa mmoja wa viongozi ambao hawakuishiwa vituko katika miaka yake minne, lakini sasa anabaki kuwa historia, baada ya kumpisha Evans Aveva.
Kauli zake za kebehi na kejeli zilizochanganyika na siasa nyingi katika utendaji kazi, ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha apewe jina la utani la ‘Tutu Vengere’, yaani mtu mwenye msimamo mkali. Hii ilikuja baada ya kuigomea TFF kuitisha mkutano wa dharura kutatua migogoro iliyokuwa imetanda Msimbazi. Rage aliweka ngumu na TFF wakanyamaza kimya.

8. Salum Sued
Nidhamu na umakini katika ulinzi, vilimpa cheo cha nahodha wakati Stars ikinolewa na Marcio Maximo, kabla ya kustaafu mwaka 2010 kuichezea timu ya taifa na kujikita kuichezea Mtibwa Sugar. Kamwe huwezi kumuona tena katika uzi wa timu yoyote ya ligi kuu, labda iwe timu ya maveterani au zile za mchangani.
Wiki mbili zilizopita, Sued aliuandikia barua uongozi wa Mtibwa kuhusu azma yake ya kuachana na soka, baada ya kuitumikia kwa kipindi cha miaka isiyopungua 15.

7. Martin Mganyizi
Zungumzia mafanikio yoyote ya Kagera Sugar, lazima umtaje beki Martin Mganyizi. Alikuwa na kikosi cha ‘Wakata Miwa’ hao wa Kaitaba kwa zaidi ya miaka 10 na ni mmoja kati ya nyota walioipandisha ligi kuu 2004.
Baada ya kumalizika msimu uliopita, alitangaza kuachana na soka na kujikita katika shughuli binafsi za jamii. Kustaafu kwake na kuondoka kwa Themi Felix, aliyesaini Mbeya City, kunaifanya orodha ya nyota walioipandisha ligi kuu Kagera Sugar kuisha.

6.  Erackson Kakolaki
Baada ya kuitumikia Azam kwa mafanikio makubwa, mataji kama Kombe la Mapinduzi mara mbili, Ligi Kuu Bara na kushiriki michuano ya kimataifa, hatimaye aliamua kutundika daluga na kugeukia ukocha.
Ni kama Kakolaki alikuwa akisubiri ubingwa wa ligi kuu, kwani baada ya kuchukua ubingwa huo msimu uliopita, ikiwa ni mara ya kwanza tangu Azam ipande ligi kuu, ndipo akaachana na soka.

5. Waganda wa Kagera
Mwanzoni mwa mwezi huu, Klabu ya Kagera Sugar ilitangaza kutema zaidi ya nyota 10, wakiwemo nyota wote wa kimataifa; kipa Hannington Kalyesubila na straika Hamisi Kitagenda, wote raia wa Uganda.
Chanzo kikuu ni viwango duni vya nyota hao, ambapo Kitagenda ndani ya msimu mzima hakuwahi kuifungia Kagera hata bao moja licha ya kucheza mechi nyingi. Ni sababu hiyohiyo iliyomuondoa kipa Kalyesubila ambaye alikuwa akiishia benchi na mzawa Agathon Anthony akishika usukani.


4. Crispin Odulla, Mieno ‘Hump’
Chochote ambacho Coastal Union watajivunia katika ligi kuu msimu uliopita, lazima majivuno hayo yamguse Odulla. Mkenya huyo, alikuwa mhimili mkubwa katika kiungo cha Wagosi wa Kaya lakini itakuwa ngumu kumuona tena kwenye soka la Bongo, tayari amesaini Bandari FC ya huko kwao Kenya.
Kama ilivyo kwa Odulla, Mkenya mwingine, Humprey Mieno ‘Hump’ na jezi yake namba 30, itakumbukwa katika kikosi cha mabingwa Azam FC. Akicheza sambamba na Kipre Balou, Aboubakar Salum ‘Sure Boy’, kiungo huyo aliyetambulika zaidi kama ‘Hump’ akifupisha jina lake, alikuwa mmoja wa viungo washambuliaji hatari, lakini katikati ya msimu aliamua kusitisha mkataba na kujiunga na miamba ya Tusker ya Kenya.

3. Abdulhalim Humud
Muite Gaucho wa Bongo, anakumbukwa akiwa na kikosi cha Azam 2012 kabla ya kusaini Simba, lakini wiki kadhaa zilizopita, aliomba kuvunja mkataba na klabu hiyo, baada ya kuona mambo hayakwenda ‘fresh’ kama alivyotaka. Na msimu ujao atakuwa na mabingwa wa zamani wa ligi ya Kenya, Sofapaka ambapo amesaini mkataba wa miaka miwili.

2. Gilbert Kaze
Alikuwa ni pacha wa Joseph Owino katika kulinda ukuta wa Simba raundi ya kwanza ya msimu uliopita, lakini ujio wa Mkenya Donald Musoti katika nafasi ya ulinzi wa kati, uliharibu kila kitu kwa Kaze na kujikuta akiishia benchi, kabla ya kupatwa na jeraha la goti ambalo waweza kusema lilizika ndoto zake Msimbazi.
Tayari Simba wametangaza kuachana naye na wamemalizana, hivyo ni nadra kumuona tena kwa msimu huu unaotarajiwa kuanza Septemba 20.
1. Brian Umony
Bao pekee la dakika za lala salama katika mchezo wa kufunga pazia, lililoipa Azam ushindi dhidi ya JKT Ruvu, litabaki kuwa historia kwao. Bao hilo lilifungwa na Umony, aliyetokea benchi, hivyo kunogesha ubingwa wao wa kwanza katika historia yao.
Achana na hilo, Umony aliiokoa Azam tena katika mchezo na Mgambo kwenye Uwanja wa Mkwakwani kwa kuifungia mabao mawili, hivyo kuvunja mfupa uliozishinda Simba na Yanga, kwani ilikuwa ni siku chache vigogo hivyo vilikuwa vimechezea kichapo. Lakini tayari Azam wameachana naye, sababu kubwa ni majeraha ya mara kwa mara.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic