Aliyewahi kuwa Kocha Msaidizi wa Taifa
Stars, Sylvester Marsh, amesema uwezo ulioonyeshwa na timu hiyo katika mechi
yake dhidi ya Msumbiji ni mkubwa na anaamini itashinda katika mchezo wa marudiano.
Stars ilikutana na Mambas ya Msumbiji
wiki iliyopita katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika inayotarajiwa kufanyika mwakani nchini Morocco ambapo katika mchezo wa
awali, ilifanikiwa kutoka sare ya mabao 2-2.
Mambas ni moja kati ya timu ambazo zimekuwa
zikiisumbua Stars kwa muda mrefu pindi zinapokutana nayo.
Marsh amesema kuwa mwenendo wa timu hiyo kwa
sasa ni mzuri kufuatia maandalizi waliyoyafanywa na kuwataka Watanzania wasiwe
na haraka ya kupata mafanikio, kwani hali hiyo hutokea hata katika maisha ya
kawaida.
“Uwezo wa Stars kwa sasa upo juu ya
Mambas kwa jinsi nilivyowaona walivyocheza katika mechi ya kwanza licha ya
kutoka sare, hivyo nina imani kubwa kuwa itashinda na kuitoa katika mchezo wa
marudiano.
“Tumeweza kuona katika mchezo wa awali
tulifanikiwa kuitoa Zimbabwe licha ya kuwa na matokeo mabaya ya awali katika
uwanja wa nyumbani.
“TFF imejitahidi kwa kiasi kukubwa
kuiandaa timu hiyo kwa kukaa kambi kwa muda mrefu na kuipeleka nje ya nchi kwa
ajili ya kujiandaa pamoja na kucheza mechi za kirafiki, ambapo imebadilika kwa
kiasi kikubwa, hivyo ni vyema wadau wakawa na subira kuhusiana na suala hilo
ili timu iweze kufanya vizuri hapo baadaye,” alisema Marsh.








0 COMMENTS:
Post a Comment