Na Saleh Ally
UMEWAONA wale raia wa Brazil namna walivyomwaga machozi baada ya timu yao
kufungwa mabao 7-1 katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Suala la kufungwa mabao hayo saba limekuwa gumzo duniani kote, lakini karibu
kila mmoja, wakiwemo waliotaka Brazil ifungwe, wamejikuta wakiowaonea huruma.
Wachezaji wa Ujerumani wamekubali kwamba walikubaliana wakati wa
mapumziko ya mchezo huo wapunguze kasi kuepusha kuidhalilisha Brazil ambayo
ilionekana ingeweza kufungwa hata mabao 10 au zaidi siku hiyo.
Binadamu yeyote, hata akiwa jambazi ameumbwa na huruma au imani, hawezi
kupingana na maumbile kwa kila kitu, hivyo inafikia wakati lazima aonyeshe
huruma.
Raia wa Brazil wamelia sana, kipigo hicho dhidi ya Ujerumani kimekuwa ni
msiba wa taifa, lakini vilio vyao havijaenda kimyakimya kama ambavyo ule msemo
wa machozi ya samaki, machozi yanakwenda na maji.
Kufungwa kwa Brazil kweli ni ishu kubwa, lakini machozi ya Wabrazili
yamekuwa ni ishu kubwa zaidi kwa kuwa wameonyesha kiasi gani ni watu wenye
uzalendo na nchi yao hadi kufikia kulia kiasi kile.
Hakuna tena anayeweza kusema tofauti kuhusiana na kilichoonekana kwamba
watu wa Brazil wanalipenda taifa lao, walitaka lishinde dhidi ya Ujerumani na
kuingia fainali, walitaka timu yao ichukue kombe.
Yote yameshindikana na Brazil imejikuta ikiangukia kwenye kipigo kikali
ambacho wanaamini ni cha ‘aibu’ ingawa kwenye mchezo wa soka ukikosea,
kuadhibiwa ni haki yako.
Kwa wewe, mimi na mwingine, tunaweza kuyaona machozi ya Wabrazili hao
kama ni sumu kwetu, kitu kinachoumiza na unapaswa kujiuliza mara mbili, tatu
kwamba umekuwa mzalendo katika nchi yako kupitia jambo lipi.
Kama ni kwenye mpira, timu yetu yenye maandalizi ya kawaida, wachezaji wa
kiwango cha kawaida, makocha wa bei chee, lakini bado tumekuwa tukijazana
uwanjani kuizomea karibu kila mechi.
Wako watu wamekuwa wakiingia uwanjani kuwashangilia wachezaji wa klabu
zao, hasa wale mashabiki wa timu kongwe za Yanga na Simba. Hili halijaisha
ingawa kwa kiasi fulani limepungua.
Wako ambao Taifa Stars ikifungwa, wanaona sawa, wanatukana na wakati
kushangilia timu za wageni wakionyesha kinachofanyika hakiwaumizi na wanasahau
ile timu imebeba bendera ya taifa letu.
Inawezekana Taifa Stars wanaudhi, lakini kuna haja ya kujikagua kupitia
machozi hayo ya Wabrazili kwamba adhabu ambayo tumekuwa tukiitoa kwa timu na
wachezaji wa timu hiyo ni sahihi.
Wabrazili baadhi waligeuka na kuwa na tabia za Kitanzania na kuwazomea
wachezaji wao, lakini hao ni tone ndani ya bahari kwa kuwa tumeona waliolia ni
wengi, wameonyesha mapenzi ya juu kwa taifa lao.
Inawezekana Watanzania ni wagumu sana kulia, ndiyo maana ni nadra kutokea
kama vile kwa Wabrazili ambao bila ya kujali mzee, kijana, mtoto, mwanamke,
wote waliangua vilio vilivyoonyesha uchungu wa dhati.
Hapa nyumbani, wanawake na wasichana wengi wanaona hawahusiki na timu
yetu ya taifa kwa kuwa soka ni mchezo wa wanaume. Hawako sahihi kwa kuwa hata
wanawake wanacheza soka sasa.
Pamoja na soka kuchezwa na wanawake lakini timu ya taifa ni ya Watanzania
wote bila ya kujali mwanaume au mwanamke, hivyo vizuri ikiungwa mkono na kupewa
nguvu na kila mmoja. Hali kadhalika, hilo lifanyike katika michezo mingine.
Sitaki na sisi Watanzania tulie, ila nataka tujifunze kupitia machozi
hayo ya Wabrazili kwamba wana mapenzi na wanaumia kuona taifa lao linafanya
vizuri. Tuumizwe na kufeli kwa timu yetu ya taifa.
Pia linapofikia suala la kutoa michango, basi litakuwa ni jambo la msingi
iwe michango endelevu, mawazo jenzi na tuamini timu hiyo si ya TFF, serikali au
wanasiasa, badala yake ni timu ya kila Mtanzania na inaweza kufanya vema kama
tukiungana na kuisaidia.
Kweli Wabrazili wamelia kwa
ajili ya nchi yao, lakini machozi yao yameumiza kila mmoja na asiyekuwa
mzalendo kwa taifa lake, atajiuliza kama kweli yuko sahihi. Wamefundishwa na
wametufundisha.
0 COMMENTS:
Post a Comment