MANJI |
Na
Saleh Ally
INAWEZEKANA
hata wewe umewahi kujiuliza siku moja, kwamba Yanga na Simba ambao ndiyo
wakongwe wa soka wataendelea kuishi katika mazingira duni kwa kipindi kirefu
kiasi gani?
Yanga
na Simba, hadi sasa zimekuwa zikifanya mazoezi kwenye viwanja vya kukodi katika
shule au vyuo, ndiyo zinajiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara iliyopangwa
kuanza Septemba 20, mwaka huu.
Ninawaza
utaniambia jibu, hivi; atafanya kwa kutembeza, maarufu kama biashara ya
kutembeza, ile inayofanywa na kina ‘Chinga’, kama hivyo itakuwa ni kweli, basi,
tukubaliane Yanga na Simba zinaendesha mpira wa ‘kutembeza’?
Sidhani
kama ni sahihi kwa klabu hizo kongwe kuwa na timu zinazocheza au kushiriki
mpira wa kutembeza. Nasema hivyo kwa kuwa hadi sasa zinategemea kuingiza
mamilioni kuendesha timu, klabu na faida juu kupitia mpira.
Lakini
hazina uhakika vikosi vyao vitajiandaa wapi zaidi ya kudandia viwanja vya vyuo,
shule au maeneo mengine. Hiki si kitu sahihi kuendelea kufanya hivyo.
AVEVA |
Yanga
wanalipa Sh 100,000 kwa siku kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola,
Mabibo jijini Dar. Kama wataendelea kufanya mazoezi kwenye uwanja huo wa shule
kwa miaka minne baadaye, bora wangekuwa wametengeza uwanja wao wa mazoezi.
Tayari
Yanga wana eneo pale Kaunda, wakati wakiendelea kushughulikia suala lao la
kuongezewa eneo ili wapate nafasi ya ujenzi wa uwanja mpya, bado wanaweza
wakatengeneza sehemu tu ya kuchezea ‘pitch’ na kuepuka gharama za Sh 100,000
kwa siku ambazo ni nyingi sana kwa watu wawili ambao watakuwa wakisimamia
uwanja.
Hali
kadhalika, Simba wana eneo lao Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Niliona wameanza ujenzi wa uwanja huo, yaani sehemu ya kuchezea. Kama hilo ni
kweli, vyema kuliharakisha na kulipa kipaumbele.
Haraka
unaweza kuangalia kwamba kwa nini Yanga na Simba wanaweza kujenga viwanja vyao
vya mazoezi au huenda suala hilo lingekuwa limefanyiwa kazi kitambo kama wote
wangelitilia mkazo.
Usajili
wa wachezaji wapya hasa wale wa nje umekuwa ukianzia zaidi ya dola 15,000
(zaidi ya Sh milioni 24.7), kwa wachezaji watano kama watasajiliwa ndani ya
misimu miwili ni zaidi ya Sh milioni 120.
Lakini
jiulize namna Yanga na Simba wanavyokwenda na mfumo wa ununuzi wa magari mapya
kwa gharama kubwa, halafu linapofikia suala la matairi wananunua mitumba ambayo
hayana uhakika katika usalama wa gari ambalo ni ghali.
Kwamba
wanawasajili wachezaji kwa bei kubwa sana kutaka wazichezee timu zao. Hakuna
ubishi kuwa klabu inapomsajili mchezaji kuichezea timu yake inachokuwa inataka
ni matunda au sema mafanikio, si maneno.
Sasa
kama mchezaji anasajiliwa mwisho anaishia kukaa nje ya uwanja kutokana na kuwa
majeruhi, hiyo ni sehemu ya matumizi mabaya ya rasilimali za taasisi.
Simaanishi ukiwa uwanja mzuri mchezaji hawezi kuumia, lakini uwanja mbovu, una
asilimia nyingi za kuchangia wachezaji kuumia.
Vipi
klabu hizo zitumie gharama kubwa za wachezaji mfano hao kutoka Burundi, Brazil,
Kenya, Rwanda na kwingineko, pia ziendelee kuwalipa mishahara mikubwa, halafu
wajiandae kwenye viwanja vya kubahatisha!
Makocha
wote waliowahi kufundisha Yanga na Simba kwa kipindi karibu cha miaka 10
wamekuwa wakilalamika viwanja. Ernie Brandts wa Yanga ndiye ninamkumbuka zaidi
kwa kuwa alionyesha kuumizwa tokea mwanzo na ubora wa viwanja.
Wakati
wake, Yanga ilikuwa ‘inadandia’ Uwanja wa Bora Kijitonyama ambao unatumiwa na
timu ya mtaani ya Kijitonyama. Hapa pia unaweza kujifunza thamani au maana ya
klabu kongwe isivyoeleweka vizuri.
Nakumbuka
nilisafiri na Simba ambao waliweka kambi nchini Oman, nikiwa huko nilielezea
namna hadi timu za daraja la nne zilivyo na viwanja bora kabisa vya kufanyia
mazoezi. Mwisho nikasisitiza namna klabu za Tanzania zinavyoweza kuwa na
viwanja kwa kutumia gharama ndogo tu ili timu zao ziwe na uhakika wa mazoezi.
Huenda
viongozi waliokuwepo awali kutokana na umri mkubwa au kutolitilia mkazo sana
suala hilo waliona kawaida tu. Lakini sasa Yanga ina Yusuf Mehbub Manji, Simba
ina Evans Elieza Aveva.
Sina
maana ni majina tu, lakini ni watu ambao wamefanya mengi kwa maana ya mipango
kisoka. Manji alifanya ukarabati wa makao makuu ya klabu yake, kukawa na
mabadiliko makubwa ambayo hayakufanywa kwa zaidi ya miaka 20.
Pia
amekuwa na mengi aliyofanya kama usajili wa juu kabisa, kuajiri makocha na
wengine ni ghali na kadhalika. Aveva hali kadhalika, ndiye alianzisha Kundi la
Friends of Simba (FOS). Hakuna ubishi kwa muda mfupi limefanya mambo mengi
sana.
Achana
na wale ambao wamekuwa hawapewi shukrani hata kidogo kwa FOS, lakini
walichofanya na kwa kushirikiana nao pamoja na Wanasimba wengine, Aveva anaweza
kuchangia kuleta mabadiliko na yakaanzia kwenye uwanja wa mazoezi.
Uwanja
huo hauwezi kuwa unatumiwa na vikosi vikubwa tu vya Yanga au Simba. Klabu zote
zinazungumzia programu za kukuza vijana. Haziwezi kuwa na mafanikio wakati
hazina hata viwanja vya kuwakuza watoto hao.
Wakati
mwingine naona Yanga na Simba, kila upande una mpango wa kupata mtoto wakati
zinaishi kwa kutegemea msaada wa majirani. Wachezaji makinda wanahitaji viwanja
vizuri na bora.
Manji
amefanya mengi sana kwa Yanga, hata kama atakuwa shukrani hapati. Hali
kadhalika Aveva na rafiki zake wa FOS. Ninaamini wanachama na mashabiki wa
Yanga na Simba watakuwa tayari kuwasaidia kufanikisha hilo.
Lakini
hata kama michango na kupatikana kwa fedha za klabu kutashindikana, basi
niwaume sikio, mnaweza kwenda kwenye makampuni makubwa kama Coca Cola, mabeki
na mengine mengi na kuwaambia wawatengenezee pitch halafu muweke mabango yao
kwa miaka kadhaa na watafaidika na matangazo, tafadhali Manji na Aveva, ondoeni
aibu hii.
0 COMMENTS:
Post a Comment