July 28, 2014

OKWI KAZINI...


Na Saleh Ally
GUMZO la Yanga itachukua uamuzi gani kuhusiana na wachezaji wake wawili wa kigeni raia wa Uganda ndiyo limekuwa likichukua nafasi kubwa katika usajili wa mwisho.


Tayari Yanga ina wachezaji wanne wa kigeni ambao ni Jaja na Coutinho kutoka Brazil, Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite raia wa Rwanda na hawa wanaonekana tayari wamepita, hakuna mgogoro kwao.

Nafasi imebaki moja, lazima Emmanuel Okwi au rafiki yake, Hamisi Kiiza ambao wote ni raia wa Uganda, mmoja wao ataachwa. Swali limekuwa ni nani?

Kadiri siku zinavyosonga mbele, suala hilo linaonekana kuwa ni mjadala mkubwa na taarifa za mapema juzi na jana, zinaeleza uongozi wa Yanga umelikabidhi kwa kocha Marcio Maximo ambaye ataamua.
KIIZA MAZOEZINI

Maximo atapewa nafasi ya kuwaona wote wakicheza. Huenda atataka kuhakikisha lakini hana ugeni sana na Okwi ambaye alikuwa akiichezea Simba.

Okwi hajashuka kiwango, bado ni mchezaji ambaye timu yoyote ingehitaji kumtumia kama msaada kwake, hali kadhalika Kiiza, kwamba ni mfungaji mzuri sana.

Kwa sababu za kiufundi inaonekana Yanga itamhitaji Okwi kuliko Kiiza kutokana na nafasi zao. Angalia hivi; Kiiza ana uwezo mkubwa zaidi wa kucheza namba kumi ambayo ni ndani au karibu na namba tisa, lakini anaweza kujitahidi kucheza pembeni kushoto, yaani 11.

Lakini Okwi ni hatari zaidi anapokuwa pembeni kushoto, yaani 11, lakini pia anaweza kufanya vizuri kama akitumiwa kama namba 10, yaani acheze ndani.

Kwa hali ilivyo, Yanga inamhitaji Okwi kuliko Kiiza kwa kuwa ina zaidi ya washambuliaji watano ambao wanaweza kucheza namba tisa na kumi.

Washambuliaji wazalendo ambao wanaweza kucheza namba za ushambuliaji kati ni Jerry Tegete, Said Bahanuzi na Hussein Javu. Wabrazili Jaja na Coutinho pia wana uwezo wa kucheza 9 na 10.

Tegete anahitaji nafasi, uwezo wake unajulikana, pia ni vizuri kuwapa nafasi wachezaji wazalendo ingawa nao wanatakiwa kujituma na kuonyesha uwezo na si kusubiri kubebwa kwa kisingizio cha uzalendo.

Bahanuzi, Javu bado wanaweza kuwa na mabadiliko na kufanya vizuri, hivyo wapewe nafasi katikati ili wacheze na kuonyesha uwezo. Jaja na Coutinho, bado Yanga pia ina nafasi ya kuwaona na hii ni taarifa tosha kwamba namba 9 na 10, tayari kuna watu na ushindani mkubwa wa namba.

Hapa ndiyo utapata jibu kwamba hata bila ya Maximo kuwaona, Yanga inamhitaji Okwi kuliko Kiiza ambaye kama akipewa nafasi ya kubaki, maana yake idadi ya washambuliaji wa kati itazidi kupaa na kupunguza wale wa pembeni ambao wanahitajika zaidi.

Pembeni, Yanga itawatumia Mrisho Ngassa na Simon Msuva au Nizar Khalfan. Ukiangalia Okwi kwa nafasi ya pembeni kushoto kwa ajili ya kusukuma mashambulizi ni bora zaidi kiuwezo.

Ndiyo maana unaweza kusema Yanga wanapoteza muda katika suala hilo la Kiiza na Okwi na badala yake uongozi ungeweza kuamua mambo haraka na kumalizana na Okwi ili arejee na kuanza kazi mara tu baada ya majukumu ya timu ya taifa.

Yanga walikuwa na madai yao kwa Okwi, naye alikuwa na yake, hivyo ni suala la kumalizana na kueleza kila upande unataka nini kifanyike, mara moja mambo yatakuwa mazuri.

Kweli Okwi anadai, aliahidiwa lakini halikutekelezwa, ana haki ya kuchukia, lakini naye akapitiliza na kufikia hadi kuonekana kufanya utovu wa nidhamu, pia alikosea. Hapa kila upande una makosa!

Kiiza bado ni mchezaji mzuri, lakini kama ingekuwa ni kuangalia aachwe au abaki, basi angeingizwa kwenye kundi la wachezaji watatu, yeye, Jaja na Coutinho halafu ipimwe kuwa kati yao nani aachwe.

Bado Yanga ina nafasi ya kumbakiza Okwi, lakini kama mwenyewe atakuwa na msimamo tofauti, hapo ndiyo kunaweza kukawa na uamuzi tofauti. Hivyo hakuna haja ya kupoteza muda na kufanya siasa ilichukue suala hilo, limalizwe kitaalamu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic