December 2, 2016



Hakika unaweza kushangazwa na namna Simba inavyohaha kuwabakiza vijana iliowalea na taarifa zinasema kijana aliyepewa unahodha, Jonas Mkude amewazimia simu viongozi wa klabu hiyo.

Habari za uhakika zinasema, Simba wamekuwa wakihaha kumpata Mkude ili kumalizana naye katika suala la usajili, lakini yeye alikuwa amezima simu tangu Jumatatu.

“Kweli Mkude alizima simu kabisa baada ya kuwa tumefanya naye majadiliano kwa mara ya kwanza. Kukawa hakuna mwafaka sahihi, wakati tunasubiri arudi kumalizana naye, akazima simu.

“Tulimtafuta kwa siku mbili, mwisho tukawaambia Meneja Mussa Mgosi na Mratibu, Abbas Ally kumtafuta. Nao wakafanya hivyo bila ya mafanikio na mwisho tumeamua kukaa kimya na kusubiri,” chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba kilieleza.

“Sasa kama anataka kusaini sawa, au tumesikia kuna mtu kamshawishi asisaini ili akacheze Afrika Kusini sawa. Tunajua namna ya kulifanyia kazi hili na kupata jibu. Tumechoka kufanywa kama watoto.”

Imeelezwa, ili kuongeza mkataba Mkude alikuwa akitaka kupewa Sh milioni 80, baadaye akashuka hadi 60 wakati Simba walikuwa wameishia 40, wakapanda hadi 50 na Mkude ndiyo akaamua kuzima simu.

Wiki hii mwanzoni, Mkude aliliambia gazeti hili atakwenda kusaini Yanga badala ya Simba kama hali ya kutofikia mwafaka itaendelea.

Lakini siku chache baadaye, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga naye akatoa kauli yake kwamba hawana mpango na Mkude na wanaangalia mbali zaidi kwa kusaka viungo ‘wakata umeme’ wenye uzoefu kwa ajili ya michuano ya kimataifa na inaelezwa hiyo inaweza ikawa sababu ya kumtia hofu Mkude na huenda akaanza kuwatafuta viongozi wa Simba, ili wamalizane.

Inaripotiwa kuwa juzi na jana Mkude alikuwa mmoja wa wachezaji wa Simba walioshiriki katika mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi jijini Dar.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic