VIZURI sana kama hakutakuwa
na sababu ya kuanza kwa lawama kwa wachezaji wa timu ya soka ya taifa, Taifa
Stars ambao jana walipambana vilivyo kutaka kuvunja ‘utaratibu’, kuwa Msumbiji
ni wagumu kwetu.
Mechi imemalizika kwa mabao
2-2 huku wageni wakisawazisha katika dakika za mwisho kabisa baada ya Isaac
Calvaho kufunga bao la kusawazisha kutokana na pasi nzuri ya Elias Pelembe
‘Domingues’.
Kuwalaumu kwa sasa kwa kuwa
tunaamini Taifa Stars bado wana kazi mbele yao haitakuwa sahihi, badala yake ni
kuwapa moyo lakini ni kuwaeleza ukweli kwamba kuna sehemu fulani walikosea.
Katika mechi ya jana, Stars
waliianza vibaya, wao ndiyo walionekana ni kama wageni na muda mwingi waliwapa
nafasi
Msumbuji kuuchezea mpira na hawakuwa na presha kubwa.
Moja ya sifa kubwa ya
Msumbiji ni kucheza vizuri, pasi za uhakika na staili yao ni ya KIreno.
Kuwanyima raha ni lazima kuwazuia kucheza mpira waliouzoea, lakini jana haikuwa
hivyo.
Kidogo imeishangaza kuona
Stars ikishindwa kuwabana Msumbuji kwa staili yao ya uchezaji kwa kuwa Kocha
Mart Nooij anajua kuhusiana nao kwa kuwa alikuwa kocha wao, labda aseme
maelekezo yake hayakufuatwa.
Kitu kingine, Stars hawakuwa
na nguvu ya kutosha katika kiungo na ilionekana muunganiko wa Erast Nyoni na
Mwingi Kazimoto kutokuwa na nguvu ya kutosha, hivyo kuwapa nafasi ‘Wamakonde’
hao kucheza.
Suala la kutokuwa na mkakati
madhubuti wa kumdhibiti Elias Pelembe maarufu kama Domingues, pia ni jambo
ambalo limeiangusha Taifa Stars. Kwa kuwa rekodi yake inajulikana kuanzia kwa
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ hadi Kocha Nooj.
Domingues ni mmoja wa
wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu katika ukanda wa chini ya Jangwa la
Sahara. Sasa anakipiga Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, ni msumbufu na
anajua cha kufanya.
Katika mechi ya jana,
alifunga bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti baada ya ndugu yake kufanyiwa
madhambi halafu akatoa pasi ya bao la pili. Hii inaonyesha kiasi gani ni hatari
kwa Stars.
Ndiye aliyechangia kwa kiasi
kikubwa Taifa Stars kung’olewa kwa mikwaju ya penalti, mara ya mwisho
ilipocheza mjini Maputo baada ya mechi kumalizika kwa sare ya mabao 1-1 jijini
Dar na baadaye jijini humo.
Domingues alikuwa msumbufu,
tatizo kubwa kwa ngome ya Stars. Lakini katika mechi ya jana, hakukuonekana
kama kulipangwa njia ya kumdhibiti mkali huyo wa Msumbiji anayevaa namba saba
mgongoni.
Mechi ilikuwa ngumu na
huenda bado ninaweza kupeleka malalamiko yangu kwa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), kwamba kuamua kuweka kiingilio kikubwa huku likijua mechi itaonyeshwa
kwenye runinga, limechangia kukosekana kwa watu wengi wa kuishangilia Stars kwa
nguvu.
Vizuri sasa TFF ya Malinzi
ikaangalia umuhimu wa kupata watu wengi uwanjani Stars inapokuwa inacheza,
kuliko kutaka kupata fedha nyingi tena kwa mipango duni. Ninaamini hata fedha
zilizopatikana katika mechi hiyo zitakuwa chache sana, yote hiyo ni mipango
duni.
Stars wana nafasi ya
kujipanga, ikiwezekana kambi ibaki Dar es Salaam ili wajiandae vilivyo kwa
ajili ya mechi ya pili na hakuna sababu ya kukata tamaa kwa kuwa wakipambana
vilivyo wana kila sababu ya kusonga mbele.
Vizuri kurekebisha makosa
kadhaa, wachezaji waliocheza chini ya kiwango kama Mrisho Ngassa, Kelvin
Yondani na wengine, waamini ilikuwa siku mbaya na wanaweza kufanya vizuri zaidi
kwa kuwa kuna kitu muhimu cha kufanya.
Lakini waliofanya vizuri
jana kama Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Hamis
Mcha na wengine, waamini wanaweza kufanya vizuri zaidi na siku ikifika,
wakaipiganie nchi yetu.
0 COMMENTS:
Post a Comment