NA Saleh Ally
MOJA ya sifa za Kocha Mkuu wa
Arsenal, Arsene Wenger ni ubahili! Kisa amekuwa hataki kutoa fedha ili kununua
wachezaji wapya.
Kwa Tanzania, wabahili wana sifa
nyingi, moja wapo ni kuficha fedha zao kwenye vibubu au vyungu. Sasa Wenger
amebadilika.
Wengi wanasema anaamini sana vijana,
au anaamini sana yale magari ya kukarabati halafu unauza kwa bei kubwa!
Amefanya hivyo kwa mafanikio makubwa
kwa kuchukua wachezaji walioaminika hawafai, akawanunua kwa bei chee na kuwauza
ghali, Arsenal ikaingiza faida.
Utaona juzi na jana vyombo vya habari
vilionyesha kushangazwa na Wenger ‘alivyolilisha’ Jiji la Manchester lenye timu
za Man United na Man City, maana wachezaji kama Emmanuel Adebayor, Gael Clichy,
Kolo Toure, Samir Nasri, Robin van Persie na Bacary Sagna, wote hao aliwapata
kwa bei chee.
Lakini kwa sasa hauwezi tena kumuita
mbahili na ikitokea mtu akafanya hivyo atakuwa amejisahau au anamuonea tu.
Wenger sasa ni kati ya makocha
wanaojichia vilivyo kifedha, ‘matanuzi’ kwenda mbele na hilo halina ubishi.
Msimu uliopita, alimnunua mchezaji
kwa pauni milioni 42 (zaidi ya Sh bilioni 100), ukawa ndiyo usajili ghali
zaidi. Huyo ni Mesut Ozil.
Msimu huu amesajili wachezaji watano
kwa pauni milioni 59, kati ya hizo pauni milioni 32 pekee amemnunua Alexis
Sanchez.
Hivyo kama utajumlisha fedha za Ozil
msimu uliopita na Sanchez msimu huu ni pauni milioni 74. Fedha hizo kwa
wachezaji wawili tu, nani atamuita Wenger mbahili, kumbuka hafundishi Real
Madrid.
Msimu uliopita alipunguza ubahili,
akabeba Kombe la FA. Msimu huu amezidi kupunguza ubahili zaidi. Je, Arsenal
itakuwa bingwa Premiership?
Alexis Sanchez:
Usajili wake unaelezwa kufikia pauni
milioni 32, si kidogo. Anatokea Barcelona kwenye La Liga, lakini uchezaji wake
wa kujituma na nguvu, hakuna hofu ya kushindwa na mfumo wa Kingereza.
Hii inaonyesha kweli Wenger ameondoka
kwenye kundi la wabahili kutokana na kutumia mamilioni ya pauni.
Sanchez alikuwa anaaminika ni wanne
kwa ubora wa ufungaji mabao kwenye La Liga, lakini alikuwa mwiba wakati akiwa
mshambuliaji wa Udinese ya Italia akicheza nyuma ya Antonio Di Natale.
Mesut Ozil:
Wenger alikubali kutoa pauni milioni
42.5 kumtwaa akitokea Real Madrid lakini ikaonekana kama vile amebugi. Msimu
uliopita ndiye alikuwa mchezaji ghali zaidi.
Wachambuzi wa England wakasema hana
nguvu na si imara kupambana kwenye Ligi Kuu England, sasa anawaonyesha.
Kwanza ameisaidia Arsenal kubeba ubingwa
wa FA, pia ndiye mmoja wa wachezaji watatu wa juu waliotoa pasi nyingi za mabao
Premiership msimu uliopita.
Kwenye Kombe la Dunia kaonyesha uwezo
sahihi na sasa anarudi England akiwa tayari na amezoea, matarajio ni kung’ara.
Wapya:
Alexis Sanchez (Barcelona, pauni 32m),
Mathieu Debuchy (Newcastle United, pauni 12m), David Ospina (Nice, pauni
3m), Calum Chambers (Southampton, pauni 12m).
Waliondoka:
Lukasz Fabianski (Swansea City-huru), Bacary
Sagna (Manchester City-huru), Chuks Aneke (Zuite Waregem-huru), Nicklas Bendtner
(huru), Chu Young Park (huru),
Wellington Silva (UD Almeria-mkopo), Thomas Eisfeld (Fulham-siri), Carl
Jenkinson (West Ham-mkopo).
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment