August 17, 2014


JENGO LA PPF TOWER AMBAKO TFF WALIKUWA WAMEHAMIA, OFISI ZAO ZILIKUWA KATIKA GHOROFA YA TATU.


Baada ya kupoteza mamilioni ya fedha bila ya sababu za msingi, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeamua kurejesha ofisi zake Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.


TFF imesema imefanya hivyo, eti kwa vile mipango ya uendelezaji wa eneo hilo bado haijakwenda kama ilivyopangwa awali.
WALIHAMA HAPA, SASA WANARUDI BILA YA MABADILIKO YA JAMBO LOLOTE KAMA AMBAVYO WALIVYOPANGA AWALI.

Pia TFF ikaongeza kwa mbwembwe kabisa kuwa uamuzi huo ni moja ya maazimio yaliyofikiwa kati ya Kamati ya Utendaji ya TFF na ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) uliokuwepo nchini kwa wiki nzima kwa ajili ya kufanya mapitio (review) ya uendeshaji wa TFF.
Kitu kinachoshangaza kwamba iliamua kuhama pale bila ya kuwa na uhakika na wanachotaka kukifanya.

Kodi waliyotumia, fedha zilizotumika kwa ajili ya kuhamisha vifaa vyao kutoka Karume hadi kwenye jengo la PPF Tower katika ya jiji la Dar es Salaam, zimekwenda bure na zingeweza kutumika kulipa madeni lukuki ya shirikisho hilo au kutumika kwa programu za kuendeleza vijana au kusaidia mpira wa Tanzania!

Akizungumza Dar es Salaam leo (Agosti 17 mwaka huu), kiongozi wa ujumbe huo wa FIFA uliokuwa na maofisa sita, Zelkifli Ngoufonja amesema wamepitia maeneo mbalimbali ya uendeshaji wa TFF na mpira wa miguu kwa ujumla na kukubaliana kufanya uboreshaji kwa lengo la kuongeza ufanisi.

Ngoufonja ambaye ni Meneja Mwandamizi wa FIFA anayeshughulikia Programu za Maendeleo Afrika amesema kabla walikutana na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali kwa lengo la kuangalia jinsi watakavyochangia katika uendelezaji mpira wa miguu nchini.

Amesema wamekubaliana na TFF katika mpango wa utekelezaji (Action Plan) na maazimio waliyokubaliana ikiwemo na muda wa utekelezaji wake, hivyo FIFA watafuatilia na kutoa msaada ili kuhakikisha utekelezaji unafanyika kama ilivyopangwa.

Maeneo yaliyofanyiwa kazi ni utawala bora (Governance), Maendeleo ya Ufundi (Technical Development), timu za Taifa (National teams), Mashindano na Vitendea Kazi (Competitions and Facilities), na Utawala na Uongozi (Administration and Management).

Maofisa wengine wa FIFA waliofuatana na Ngoufonja ambaye ni raia wa Cameroon ni Meneja wa Programu za Ustawi (Performance), Marco Schuepp, Ofisa Maendeleo, Ashford Mamelodi, Ofisa Maendeleo wa Ufundi, Govinden Thondoo, Mkufunzi wa Makocha, John Peacock na Mshauri wa Programu za Ustawi, Ian Riley.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic