August 23, 2014


FIGO AKIWA NA SALEH ALLY.


Na Saleh Ally
KWA Hispania wanaamini Gareth Bale ndiye mrithi mpya wa winga au kiungo wa pembeni matat, Luis Figo ambaye wakati wa enzi zake anajulikana.
Sifa kubwa ya Figo ni kasi, krosi za ‘moto’ lakini mashuti ambayo yanaelekezwa langoni wakati akiwa katika kasi kubwa.


Figo alitua Madrid mwaka 2000 akitokea Barcelona, aliichezea hadi 2005 akibeba makombe lukuki. Ubingwa wa La Liga mara mbili (2000-01, 2002-2003), Super Cup Hispania (2001 na 2003).
SALEH ALLY AKIZUNGUMZA NA RAYCO GARCIA, KULIA NI KAREMBEU NA KATIKATI YAO NI SANZ.

Achana na makombe hayo lakini Ligiya Mabingwa Ulaya mwaka 2002 ambao pia walibeba Uefa Super Cup kama ambayo Madrid wameibeba kwa mara nyingine.
Hiyo ni Madrid lakini alibeba makombwe mengine ya La Liga, Copa del Rey, Super Cup ya Hispania na ile ya Uefa akiwa na Barcelona.
 Figo pamoja na kutoa pasi tamu za mwisho maarufu kama asisti, pia ana uwezo wa kucheka na nyavu kwa kuwa akiwa na Madrid alicheza mechi 164 alipachika mabao 36 akionyesha ni moto kwa kuwa Barcelona alicheza mechi 172 akapiga mabao 30.
Figo leo atakuwa kwenye kikosi cha wakongwe wa Real Madrid ambao wametua nchini tayari kuwavaa Tanzania Eleven ambao wako fiti kweli na tayari kwa kuonyeshana kazi.
Katika mahojiano mafupi na SALEHJEMBE, Figo mwenye miaka 41 sasa, anasisitiza hawezi kukimbia kama zamani, lakini uwezo wake ni burudani tosha.
“Hauwezi kupingana na umri, lakini aina yangu ya uchezaji inabaki ileile. Vizuri zaidi nacheza na watu wanaonijua au tunajuana vizuri,” anasema huku akitabasamu.
“Njoo siku ya mechi uone, ninaweza kufanya kila unachokijua, kukimbia, pasi nzuri, kufunga na mengine na ndiyo wanavyoweza kufanya wengi katika kikosi chetu.
“Wengi umri umekwenda, lakini wanacheza soka la kuvutia,” anasema Figo ambaye aliichezea timu ya taifa ya Ureno mechi 127 na kufunga mabao 32. Kwenye Kombe la Dunia mwaka 2006 ndiye alikuwa nahodha wa timu hiyo.

Leo Figo atakuwa kazini kupambana na mabeki wa Tanzania Eleven akiwemo Abubakari Kombo na Shadrack Nsajigwa ambao wana sifa ya wachezaji wa kimataifa wa kiwango cha juu kwa ‘levo’ ya kwetu.
Inaonekana itakuwa burudani nzuri lakini kwa muonekano, Figo ni mchezaji ambaye anafanya mazoezi ya kutosha.
“Mazoezi kwangu si kwa sababu ya mechi, nafanya hivyo kama sehemu ya maisha yangu, nina diet maalum kila baada ya kipindi fulani.
“Suala la kuwa niko fiti au la, lisikupe hofu. Kikubwa nasisitiza njoo utuone (Real Madrid), nina uhakika utafurahi, halafu utaniuliza zaidi,” analihakikishia Championi.
Kwa tuzo binafsi alizowahi kupata zinathibitisha kuwa Figo ni kati ya wachezaji wa kiwango cha juu kabisa waliowahi kutokea Ureno na duniani kote.
Kupitia makubwa aliyoyafanya akiwa na Barcelona, Madrid na timu ya taifa ya Ureno inamfanya awe ndiye mchezaji maarufu zaidi katika klabu hizo maarufu za Hispania.
Alikuwa nyota na gumzo ndani ya Barcelona kuanzia mwaka 1995 hadi 2000, akaondoka na kujiunga na Madrid mwaka 2000, wengi wakidhani kasi ingepungua. Lakini miaka mingine aliendelea kuwa moto na gumzo katika jiji la Madrid.
Amewahi kutwaa tuzo binafsi kama zile za Mchezaji bora wa Ulaya chini ya miaka 21 (1991), Mfungaji bora wa Hispania (1994), Mchezaji bora wa Ureno (1995, 1996, 1997, 1998, 1999, 2000).
Mchezaji bora wa kigeni wa Hispania (1999, 2000 na 2001), Mchezaji Bora wa Ulaya (2000), Mchezaji bora wa Dunia (2001), pia ni mmoja wa wachezaji bora 100 wa karne walioteuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Awali alisema ni lazima auone Mlima wa Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote Afrika. Kweli hilo litakamilika baada ya kampuni ya TSN kupanga ratiba ya kuwapeleka.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa TSN, Farough Baghoza, amesema kesho ndiyo itakuwa safari ya kwenda Mlima Kilimanjaro.
“Lengo ni kama kutembelea na kuangalia utajiri wa Tanzania. Kupanda haitawezekana kutokana na ratiba zao kuwabana na unajua inachukua muda kuupanda mlima huo,” anasema Farouk.
Mechi ya leo, tayari imekuwa gumzo katika viunga vya jiji la Dar es Salaam na kuna taarifa baadhi ya wadau kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda, wameanza kuwasili nchini kuhakikisha wanaishuhudia mechi hiyo.

TUZO BINAFSI:
Mchezaji bora wa Ulaya chini ya miaka 21 (1991), Mfungaji bora wa Hispania (1994), Mchezaji bora wa Ureno (1995, 1996, 1997, 1998, 1999, 2000).
Mchezaji bora wa kigeni wa Hispania ( 1999,2000 na 2001), Mchezaji Bora wa Ulaya (2000), Mchezaji bora wa Dunia (2001), pia ni mmoja wa wachezaji bora 100 wa karne walioteuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Fin.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic