WAZO la awali ilikuwa ni kwamba kikosi cha wakongwe cha Real
Madrid kicheze mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya soka ya taifa, Taifa Stars.
Nilikuwa kati ya wale waliopinga hilo.
Waandaaji Kampuni ya Tanzania Sisi ni Nyumbani
(TSN), chini ya mkurugenzi wao Farough Baghoza, wakaonyesha ni watu wanaoweza
kusikiliza jambo ambalo lina hoja ya msingi kwa kuwa wadau wengi walichangia na
kuona haikuwa sahihi.
Kweli wakalifanyia kazi na kuamua kuita kikosi
cha wachezaji wakongwe kutokana na timu mbalimbali za Tanzania kama vile Simba,
Yanga, Sigara, Pan African na nyingine nyingi kuunda kikosi.
Tayari chini ya Charles Boniface Mkwasa ‘Master’
akishirikiana na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Fred Felix Minziro ‘Majeshi’,
wameanza maandalizi kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
Hili ni wazo sahihi kwamba wakongwe wa Real
Madrid ambao wataongozwa na wachezaji kama Luis Figo, Christian Karembeu, Steve
McManamann, Fernando Morientes, Fabio Cannavaro, Michel Salgado na wengine,
watakutana na wakongwe wenzao.
Mechi hiyo itapigwa kesho Jumamosi kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar, nimeanza kuona pilika na namna ambavyo watu
wamekuwa wakikimbilia tiketi kwa kuwa waandaaji waliweka hadi zile za kiwango
cha chini cha Sh 5,000.
Hadi kuwa na kiingilio cha Sh 5,000, inaonyesha
pamoja na gharama kubwa za maandalizi, waandaaji bado wamewafikiria Watanzania
na uwezo wao na hasa wapenda soka. Wamewapa nafasi ya kwenda kuwaona nyota kama
hao niliowataja.
Kumuona Figo akicheza dhidi ya Abubakari Kombo
kwa Sh 5,000 tu ni zawadi na huenda itakuwa mechi ambayo kila atakayepata
nafasi ya kuiona, itakuwa ni mara moja tu na si zaidi ya hapo.
Ninaweza kusema si vizuri kukosa kama una
nafasi ya kufika, kwa kuwa soka ndiyo burudani yetu. Kuburudika si vibaya,
lakini ninalenga watu kutokwenda kwenye mechi hiyo kwa wingi kwa lengo la
kuangalia Figo na wenzake wanakimbia vipi, wanapigaje chenga ili washangilie
tu, halafu wakitoka, imepita.
Ujio wa kikosi hicho, hata kama tutajikausha,
ukweli ni bahati. Hakuna ubishi, wengi wao ni wachezaji waliocheza kiwango cha
juu. Kucheza Real Madrid, ndiyo juu ya mlima, ni timu bora na maarufu
ikiwezekana kuliko zote duniani.
Uchezaji wao lazima utakuwa na jambo au utofauti
mkubwa na kwa kuwa watakuwa wakicheza dhidi ya wakongwe wetu, tunaweza
kujifunza mengi kwamba wachezaji wa nyumbani wana nini na wanakosa kipi.
Kweli itakuwa ni mechi ya kujifurahisha, lakini
katika soka ushindani ni kitu kisichofichika. Hivyo lazima ushindani
utajitokeza na mwisho itakuwa rahisi kupima mambo.
Watakaoingia uwanjani pamoja na kuwa wadau au
mashabiki wa soka, watakuwa na idara zao kama waamuzi, marefa, wachezaji
wanaoendelea kucheza, makocha na kadhalika. Basi vizuri kuifanya mechi hiyo ni
shule.
Ukweli si kila kitu lazima usome darasani,
badala yake kuna madarasa yanayopatikana kwa siku moja na yanaweza kukuachia
somo la siku kibao na faida kubwa, ila kama kweli utataka kujifunza au
kujielimisha.
Kuangalia Figo anaonekana vipi, sijui umbo
kubwa, mguu wenye ‘kiazi’ kikubwa, sura yake inafananaje, hiyo ni burudani.
Lakini hakikisha hautoki Uwanja wa Taifa bila ya kuwa umefaidika na kisomo.
Msisitizo ni kwamba, si lazima ujifunze kupitia
akina Figo, Karembeu na wenzake. Badala yake unaweza kujifunza pia kupitia
wakongwe wetu ambao wanaweza kupimika wakati
wakicheza na wale wenye kiwango na
maisha ya juu.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment