KIPIGO cha mabao 3-0
walichokipata Simba katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Zesco ya
Zambia, kimekuwa gumzo!
Simba waliojitokeza
kwa wingi kuangalia utambulisho wa wachezaji wao wapya na wale wa zamani kwa
mara nyingine, waliondoka uwanjani wakiwa vichwa chini huku watani wao wa jadi
Yanga, wakiwa na furaha ya kufa mtu.
Utani ni jambo la
kawaida, Simba ikifungwa ni furaha kwa Yanga, hivyo mashabiki wachache ‘walioutuliza’
Uwanja wa Taifa kwa kuwazomea Simba waliojitokeza kwa wingi, ilikuwa haki yao.
Wakati Yanga
wanawazomea Simba, hapo unazungumzia ushabiki, lakini Simba imepoteza mechi
hiyo, sasa tunaangalia masuala ya ufundi. Kwanza tuanze na Kocha Mkuu wa Yanga,
Marcio maximo.
Hivi karibuni, Maximo
ameingia kwenye lawama na mashabiki wa soka wamekuwa wakiamini ni muoga sana
kwa kuwa hataki mechi za kirafiki, kisa anaona ni aibu kwake kufungwa.
Hata Katibu Mkuu wa
Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicholas Musonye,
amemuita Maximo ni muoga lakini kocha huyo Mbrazili akasisitiza anatengeneza
timu na huu si wakati mwafaka.
Kipigo cha Simba
kutoka kwa Zesco, tena huku Wazambia hao wakionyesha uwezo mkubwa wa pasi,
mipango ulionyesha kuwa Simba bado ‘hawajakwiva’ na wanahitaji mazoezi zaidi
ili kujiweka kwenye kiwango sahihi.
Kweli bado hawajawa
tayari, ndiyo maana wanakwenda kambini Zanzibar kwa wiki tatu, maana yake
wamecheza na Zesco wakiwa hata hawajafikia katikati ya maandalizi sahihi, lakini
mashabiki hawalijui hilo na walichotaka ni ushindi.
Wakati tunatoka
uwanjani, mashabiki wengi walikuwa wakilaumu kwamba Simba haina lolote, hata
wachezaji waliosajiliwa ni bure na kusisitiza kwamba ‘wamepigwa changa la macho’
kwa kuwa Simba itaendelea kuwa inayoyumba kama misimu miwili iliyopita.
Asilimia 80 ya
mashabiki wa Simba waliokuwa uwanjani hapo wameshindwa hata kung’amua kwamba
pamoja na Zesco kutoka katika nchi iliyopiga hatua zaidi kisoka, lakini
walikuwa tayari na wanashiriki ligi, tofauti na Simba iliyojaza wageni na sasa
ndiyo imeanza kujipanga.
Aliyewashauri Simba
wailete Zesco wamshukuru. Kwani hata kama wamepata kipigo, lakini watakuwa
wameona matundu na namna ya kuanza kuyaziba na hii itawasaidia kuwa bora zaidi.
Kuona mapema makosa au
ulipoteleza inakuwa ni bora zaidi kwa kuwa utapata muda wa kujirekebisha kwa
nafasi na ikiwezekana kwa sasa, Simba wanahitaji mechi nyingine ya kirafiki
ndani ya wiki mbili.
Katika mechi
inayofuata, Loga anaweza kutumia kipimo kuangalia wingi wa makosa katika mechi
ya kwanza na hiyo atakayocheza, kwamba yanapungua au kuongezeka.
Wakati matamasha zaidi
yanalenga kuingiza fedha, inawezekana badala ya mipango ya kuuza jezi kwa wingi
au kuingiza fedha nyingi kupitia haki za runinga, viongozi wetu wanabuni matamasha
kama hayo, kujiingizia kipato ili kupunguza makali ya uendeshaji wa timu.
Kocha kama mtaalamu si
wa kulaumiwa katika kipindi hiki, badala yake apewe nafasi ya kumaliza
maandalizi ya kikosi chake na kukifanya imara kama anavyotarajiwa na Zesco imekuwa
msaada kusaidia kurekebisha upungufu uliojitokeza.
Mashabiki
waliolalamika, huenda kweli hawaelewi, lakini wanapaswa kujifunza na
kukubaliana nami kwamba, ukiangalia rekodi ya matamasha ya Simba Day, Simba
imepoteza mechi zake za siku hiyo kwa asilimia 90.
Hivyo ni timu
inayocheza ikiwa haijakamilika. Ndiyo maana nikawa najiuliza, kama Simba ‘wamemaindi’
hivyo, unafikiri Maximo angekubali kuingiza timu mapema? Yanga wangevumilia
mikwaju hiyo mitatu ya Zesco halafu wakae kimya!
0 COMMENTS:
Post a Comment