September 24, 2014


Na Saleh Ally
UHURU Selemani ni kati ya wachezaji Watanzania ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye soka nchini, ndiyo, hilo halina ubishi.

Amecheza Coastal Union, Mtibwa Sugar na Simba. Kushiriki kwake kwenye mchezo huo ndiyo mchango wake katika soka, usisahau amecheza hadi timu ya taifa.
Wakati Taifa Stars inacheza mechi ya kirafiki na kufungwa kwa mabao 5-1 dhidi ya Brazil mwaka 2010, Uhuru Selemani alikuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars chini ya Marcio Maximo.
Bila kujali ni mchango mkubwa au mdogo lakini ukweli ni kwamba Uhuru ana mchango wake katika soka nchini. Ila kitu kimoja leo lazima tukijadili, ana tatizo gani?

Kunaweza kukawa na maswali mengi sana, kwamba Uhuru ana nini hasa kinachomfanya ashindwe kufanya vizuri katika kiwango kinachotakiwa hasa?
Nani anaweza kusema kiwango cha Uhuru kimepanda ndani ya misimu mitatu iliyopita? Huenda mtazamo wangu ni tofauti, ninaona Uhuru ni yuleyule na huenda anaporomoka tu!
Ukiangalia hawezi kulilia nafasi maana karibu makocha wote ambao wamekuwa Simba yeye akiwa ni mchezaji wamekuwa wakimpa nafasi, lakini hazitumii vizuri.
Kama utakwenda kwa takwimu, kwamba amefunga mabao mangapi na kutoa pasi ngapi kwa msimu, ndiyo litakuwa tatizo kabisa. Sijui mara ya mwisho lini alifunga mabao nane au kutoa pasi tano za mabao!
Kama kweli Uhuru ana kasi, mzoefu, amecheza Ligi Kuu Bara kwa kipindi cha zaidi ya misimu mitano, tatizo lake ni lipi hasa?

Makocha wote kutoka nje wamekuwa na matatizo naye. Utakumbuka kipindi cha Milovan Cirkovic, raia wa Serbia, alisema Uhuru anacheza kwa kufuata jukwaa na si maelekezo yake.
Kocha Zdravko Logarusic raia wa Croatia akamuita Uhuru ni mchezaji wa Facebook, baadhi ya walio kwenye kikosi cha Simba, wakasema amemkatisha tamaa na si sahihi kumueleza mchezaji hivyo.
Katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, kocha Patrick Phiri raia wa Zambia alimuingiza katika mechi dhidi Coastal Union, akashindwa kucheza na akasema hakuwa na msaada.
Sasa Uhuru huyu ni mchezaji wa jukwaa, halafu akawa mchezaji wa Facebook, kocha wa sasa anasema hakuwa na msaada. Wote hawa ni makocha tofauti kutoka nchi tofauti kabisa!
Jiulize wanamuonea? Ajiulize mwenyewe kweli hawampendi na wanamkandamiza? Mimi nina jibu langu ingawa kila mmoja atachagua lake, kuna tatizo kwa Uhuru na lazima alifanyie kazi, asipofanya hivyo, mwisho atatafuta mchawi, kumbe mchawi ni yeye mwenyewe.
Niseme wazi, Uhuru tunaheshimiana, tukikutana tunazungumza vizuri na nikihitaji jambo kuhusiana na habari amekuwa akinipa ushirikiano, lakini huu ni ujumbe wangu kwake, tena wazi kwamba lazima afanye kitu katika hali hiyo.

Wakati mwingine ninaona kama amekuwa ni mtu mwenye papara uwanjani, anayetaka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Ana mawazo mengi kwa jambo moja, hivyo anatakiwa kujipima.
Wote tunaweza kuona mengi kuhusu Uhuru, lakini yeye mwenyewe atakuwa anajua tatizo ni nini. Binadamu anavyojitathmini mwenyewe na kuona tatizo ni lipi kwake, akilikubali ni rahisi kulimaliza. Hili ataamua mwenyewe Uhuru, ila lazima afanye sasa.

Milovan:
“Uhuru ni mchezaji wa jukwaa, anataka kuwafurahisha mashabiki. Anasikia raha kelele zinazoashiria kumshangilia kutokana na anachofanya lakini si kile anachoelekezwa na kocha.
“Ninaona anacheza soka kwa ajili yake na wala si kwa ajili ya timu. Kwangu nafasi ya kumchezesha itakuwa ndogo kwa kuwa nimejitahidi, haelewi.”

Loga:
“Mimi namuona ni mchezaji wa kwenye Facebook, sidhani kama yuko makini, si mtu anayetaka kubadilika, anasahau mara moja kila unachomuelekeza.
“Kweli namuona mchezaji wa Facebook, maana ndiko anakocheza mpira, kila wakati anaweka picha mpya. Hana msaada na timu.”

Phiri:
“Nilimuingiza Uhuru nikijua atakuwa msaada, najua ana kasi na nguvu, hivyo angeweza kuongeza kasi ya mashambulizi.
“Hakufanya hivyo, hakuwa na msaada wowote. Lakini ndiyo hivyo, tunahitaji kusahau ya leo na kuendelea mbele kwa kuwa safari bado ni ndefu.”




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic