Na Saleh Ally
LIVEPOOL ilimnunua mshambuliaji Mario
Balotelli kwa kitita cha pauni milioni 16 kutoka AC Milan ya Italia,
haikuwa na ujanja kwa kuwa ilikuwa inahitaji huduma yake kutokana na kuondoka
kwa Luis Suarez aliyetua Barcelona.
Wakati inakubali kutoa fedha hizo, Liverpool
ilikuwa na mipango mingi ikiwemo ile ya kibiashara, kwamba itazirudisha vipi
fedha zake.
Huduma ya Balotelli ni sehemu ya kurudisha
fedha hizo, lakini bado kupitia mchezaji huyo kutokana na umaarufu alioondoka
nao England akirejea Italia kujiunga na AC Milan, ungesaidia kufanya biashara
ya jezi, fulana na vitu vingine.
Hilo likadhihirika, siku ya kwanza tu baada
ya Balotelli kutua England na kujiunga na klabu hiyo, Liverpool ikauza jezi za
pauni 50,000.
Hesabu za Liverpool ni zile ambazo timu
kubwa za Ulaya na hata zinazochipukia, mfano Real Madrid na Cristiano Ronaldo
na Gareth Bale au Barcelona na Suarez ambaye walianza kuuza jezi zake hata
kabla hajatua Hispania.
Klabu hizo zinatambua suala la biashara,
kwamba kila kinachofanyika kinahusisha fedha na kawaida ili iitwe biashara
lazima kuwe na mzunguko wa fedha unazozalisha.
Hivyo lazima ziwe na kitengo
maalum cha masoko ambacho kinafanya programu zinazohusiana namna fedha
inavyoweza kuingia na klabu kupata faida.
Tanzania hili haliwezekani? Maana hakuna
tofauti, pia fedha zinatumika. Hata si kama zile za Real Madrid, Manchester
United, lakini ili klabu pia zinahitaji kutumia na kuingiza fedha. Ukubwa wa
Yanga na Simba unazifanya zitumie zaidi, hivyo zinapaswa kuingiza zaidi.
Inawezekana kwa kuwa zina mtaji wa wateja
wengi, yaani mashabiki na wanachama wengi kuliko klabu nyingine zote nchini.
Vipi watu wa mipango, iwapi mipango ya
masoko? Kwa nini haina vitengo vya masoko na sasa inaonekana kuna watu wan je
wenye mipango kuliko hata ya klabu hizo zinazoongozwa na Yusuf Manji na Evans
Aveva.
Wajanja wanaipandia mipango ya Yanga, mwisho
wao ndiyo wanaoingiza fedha na Yanga na Simba zinaambulia sifa au ujiko pekee.
Mfano mzuri ujio wa Andrey Coutinho na
baadaye Jaja, wote kutoka Brazil. Kilikuwa kipindi kizuri cha Yanga kuuza lundo
la jezi.
Simba pia, baada ya kufanikiwa kumrejesha
Emmanuel Okwi akitokea Yanga, mashabiki na wanachama wake walikuwa na hamu
kubwa ya jezi zake.
Lakini hakuna kilichofanyika, badala yake
wajanja wachache kama wale wakati wa mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara kati ya
Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar, waliuza jezi kibao za Jaja, Coutinho na Okwi huku
Yanga na Simba zikiambulia ziro.
Wachezaji hao wote wamezigharimu klabu hizo,
lakini wanaokwenda kufaidika kifedha ni wengine na wakati mwingine utaona bora
ziwe na “kamati za ufundi” kuliko vitengo maalum kwa ajili ya masoko.
Fedha ilizotumia Yanga kuwasajili Jaja na
Coutinho, angalau robo au nusu yake zingerudi kupitia mauzo ya jezi zao.
Yanga haina haja ya kupata presha, ni
kuingia mkataba na kampuni ambayo ingekuwa ikifanya kazi ya kuziagiza na
kuzisambaza, halafu unafuatia mgawo wa asilimia. Halikadhalika kwa Simba.
Sasa katika hili kuna ugumu upi na kama
Yanga na Simba zinashindwa na wale watu ambao wanauza katika mechi tena za timu
hizo iwe Yanga au Simba wanaweza, tatizo ni nini?
Lazima mambo yaende na wakati na kama kuna
mengi ya maendeleo Simba na Yanga wanaiga kuyoka Ulaya. Basi hili liwe sehemu
ya kuanza kubadilika.
Kama kwa mwaka kila moja, Simba na Yanga
zikiingiza angalau milioni 100 kupitia jezi, zitakuwa zimefaidika kuliko kukosa
na kufaidisha wengine ambao wanatumia jezi na rangi za klabu hizo na hata
majina ya wachezaji wao ili kujifaidisha!
0 COMMENTS:
Post a Comment