Timu ya Stand United ya Shinyanga, ilipata ajali ikiwa
safarini kuelekea mkoani Tanga baada ya basi lao kumgonga punda kwenye
Barabara ya Arusha.
Stand ambayo inashiriki Ligi Kuu Bara kwa mara
ya kwanza msimu huu, ilianza kwa kichapo kikali cha mabao 4-1 kutoka kwa Ndanda
na leo inatarajiwa kucheza na JKT Mgambo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mkurugenzi
wa ufundi wa timu hiyo, Muhibu Kanu, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na
kudai kuwa hakuna mchezaji wala kiongozi aliyeumia zaidi ya basi kupata
matatizo na kulazimika kutafuta gari lingine kwa ajili ya kusafirisha timu
hiyo.
“Wachezaji wamepona, hakuna aliyeumia hata mmoja
na ajali ilitokea barabara ya kuelekea Arusha ambapo basi letu liligongana na punda
wale wa mizigo lakini tunashukuru Mungu tulibadili gari na kuendelea na safari,”
alisema Kanu.
0 COMMENTS:
Post a Comment