September 15, 2014


Kiungo mshambuliaji mpya wa Simba, Mkenya, Paul Kiongera, amedai anahitaji muda kidogo tu ili aweze kuzoeana na wenzake lakini akatamba kuwa mwishoni mwa msimu anataka kiatu cha dhahabu kwa kufunga mabao mengi zaidi kwenye ligi.


Kiatu hicho, msimu uliopita kilichukuliwa na mshambuliaji wa Simba, Mrundi, Amissi Tambwe, aliyepachika mabao 19.

Kiongera alisema anaamini atatimiza ndoto zake hizo alizojiwekea kutokana na ubora wa viungo wao, Shabani Kisiga, Amri Kiemba na Pierre Kwizera.

Kiongera alisema anafurahia kombinesheni yake na Mganda, Emmanuel Okwi katika kikosi hicho kinachonolewa na Mzambia, Patrick Phiri, aliyechukua nafasi ya Zdravko Logarusic aliyetimuliwa.

Aliongeza kuwa, atatumia vyema kila nafasi atakayopata ndani ya uwanja kufunga mabao.
“Kila mchezaji ana malengo yake aliyojiwekea, kwa upande wangu nimepanga msimu ujao nichukue kiatu cha dhahabu kwa kuhakikisha ninafunga mabao kwa kila nafasi nitakayopata.
“Kikubwa, ninaomba ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzangu. Wanipe pasi nzuri za kufunga mabao, kwani wapo viungo wengi wenye uwezo wa kunichezesha uwanjani.
“Pia ninafurahia kombinesheni nzuri yangu na Okwi ndani ya uwanja, ambayo ninaamini kama tukikaa pamoja muda mrefu kwa kuzoeana, nitafanikisha ndoto zangu,” alisema Kiongera.

Kiongera hadi hivi sasa tayari amefanikiwa kufunga mabao matatu katika mechi tatu za kirafiki, ikiwemo dhidi ya Zesco, Gor Mahia na URA.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic