Na Saleh Ally
GUMZO kubwa la sahihi au la! Liko kwa
mshambuliaji wa Yanga, raia wa Brazil, Geilson Santana maarufu kama Jaja.
Wako wanaosema Mbrazili mwenzake Andrey
Coutinho ni hatari na sahihi zaidi, lakini huyo si straika, halafu umbo na aina
ya uchezaji ni tofauti na Jaja, si sawa kuwalinganisha!
Jaja ameichezea Yanga mechi nne za kirafiki,
moja mjini Pemba, mbili mjini Unguja na ya nne, kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam ambako kuna ‘wataalamu’ kibao.
Tayari ‘wataalamu’ hao wameanza uchambuzi
kuhusiana naye, kwamba hafai, hajui kukimbia, mzito kama mshambuliaji wa zamani
wa Simba, Betram Mwombeki na mengine mengi.
Kumfananisha na Mwombeki na kuamini si
mshambuliaji mkali ni kosa, kwa kuwa Mwombeki ni kati ya washambuliaji bora na
alidhihirisha hilo akiwa Simba.
Wanaosema kuhusiana na Jaja, hakuna
anayemchambua kwa takwimu, badala yake ni mapenzi binafsi na ‘hisia za zamani’
za wapenda soka wengi nchini ambao katika soka, zaidi wanavutiwa na chenga na
kukimbia kwa kasi na mpira.
Takwimu za mechi sita za kirafiki, bado
zinamlinda Jaja kama mmoja wa washambuliaji wazuri ambao wanapambana kuzoea
mazingira tofauti ya alipokulia.
Hata kama Brazil nao ni masikini, lakini kuna
utofauti na hapa nyumbani na hata uchezaji wa soka. Amerika Kusini na Afrika,
hakuna ubishi ni tofauti.
Lakini Jaja bado anajitahidi kuonyesha uwezo wa
kupambana, lakini huenda havutii kwa muonekano kwa sababu hana kasi wala si
mkali wa kukimbia kama alivyo Mrisho Ngassa, Emmanuel Okwi au Simon Msuva.
Haiwezekani wachezaji wote uwanjani wakawa
wanakimbia tu na kisayansi kila mchezaji anavyozidi kuwa na umbo kubwa, kasi
pia inapungua.
Jaja ni mshambuliaji, kama ni muziki wake kuna
mtu anataka kuusikia, basi rahisi tu. Aongeze sauti ya redio yake, halafu aanze
kusikiliza, kama kutakuwa na sehemu inaonyesha amefunga mabao au la.
Kama hakutakuwa na mabao baada ya mechi nne,
tano au 13 za mzunguko wa kwanza kunaweza kuwa na maswali sasa. Kwamba vipi
kama yeye ni mshambuliaji halafu hafungi?
‘Kumjaji’ sasa kwa sababu ya mbio nyingi na
chenga ni kumchanganya au kujichanganya. Lakini pia huenda itakuwa ni kung’ang’ania
kubaki kwenye kuamini mbio na ‘vyenga’ tu.
Apewe muda, ligi inaanza hivi karibuni. Halafu
tuone akiwa Dar es Salaam na sehemu nyingine zenye viwanja vizuri anafanyaje?
Akiwa kwenye viwanja vya mikoani atafanya nini?
Lakini atawezaje kupambana na mabeki wa Kibongo ambao wanagonga ugoko kama
hawana akili nzuri, atawezaje kufunga? Akishindwa, maswali yanaanza, hapo
hakuna kupindisha tena.
Mechi:
Yanga imecheza mechi nne za kirafiki na
kufanikiwa kufunga mabao sita huku ikiwa imefungwa bao moja tu.
Kwa tathmini ya kiufundi inaonyesha ina
mwenendo mzuri zaidi kila upande ingawa safu yake ya ulinzi iko vizuri zaidi
kuliko ushambuliaji.
Mechi nne, imeruhusu bao moja tu, ni jambo zuri
zaidi. Kufunga mabao sita katika mechi nne, bado ni vizuri ingawa inaweza kuwa
vizuri zaidi.
Katika mabao hayo, Jaja alifunga mawili,
akianza na mechi ya kwanza ambayo Yanga ilishinda kwa bao 1-0 dhidi ya
Chipukizi mjini Pemba.
Baada ya hapo akacheza mechi mbili mjini
Zanzibar dhidi ya Shangani iliyoshinda 2-0 pia dhidi ya KMKM ikashinda kwa
idadi hiyohiyo.
Mechi zote mbili, Jaja hakufunga hata bao moja.
Aliporejea Dar es Salaam, mechi dhidi ya Thika akatupia bao tena ambalo lilikuwa
pekee la ushindi.
Ushindi:
Mechi za kirafiki hazina pointi, kwa mabao yake
mawili ambayo yaliipa Yanga ushindi, kama ingekuwa ligi, maana yake angekuwa
ameipa Yanga pointi sita muhimu.
Kuisaidia timu kushinda mara mbili, si kitu
kidogo. Hivyo si rahisi kusema Jaja hawezi au kiwango chake si kizuri.
Katika mabao sita ya Yanga, yeye amefunga
mawili. Anayelingana naye ni Coutinho tu ambaye pia alifunga mawili, moja
katika mechi dhidi ya Shangani na ile ya KMKM.
Kwa washambuliaji wa kati aliyefunga bao ni
Hussein Javu tu, wengine kama Jerry Tegete, Said Bahanuzi na Hamis Kiiza hakuna
aliyefunga.
Dakika:
Jaja amecheza dakika 213 akiwa na Yanga, mechi
tatu za mwanzo alipewa dakika 45 kila moja. Mechi ya mwisho dhidi ya Thika
akacheza dakika 78.
Katika dakika 213, alifunga mabao mawili. Bado
inaonyesha ana nafasi ya kufanya vizuri kama mwendo wake utakuwa na grafu
inayopanda. Akizubaa, itaporomoka na maswali yataanza, kazi kwake itakuwa ni
kutoa majibu na huenda hadithi hazitakuwa na nafasi.
Takwimu:
Mechi 4, Mabao 2, Dakika 213
Mechi ilizocheza Yanga:
Chipukizi 0-1 Yanga
Shangani 1-2 Yanga
KMKM 0-2 Yanga
Yanga 1-0 Thika United
0 COMMENTS:
Post a Comment