WAKATi ikiwa imebaki wiki moja kabla ya kuanza
kwa Ligi Kuu Bara, hisia za mambo mengi kujitokeza linaweza kuwa jambo la
kawaida kabisa.
Lakini maswali ya nini kitatokea ni kawaida pia
kwa kuwa inapoanza ligi, mambo yanaanza kujitokeza na ndiyo burudani yenyewe.
Kizuri, hakuna ligi ambayo humalizika bila
kuacha funzo au gumzo. Kunakuwa na mengi ya kujifunza kwa kuwa katika mechi 36
kwa kila timu kuna mengi yanayotokea.
Katika udhaifu ambao umekuwa ukizidi kuutafuna
mpira wa Tanzania ni watu kuendelea kupenda Yanga na Simba pekee wakasahau hata
timu zinazotoka kwenye mikoa ya asili yao.
England ambao tunataka kuwafuata au tunafurahia
kujifunza kwao, watu hupenda timu kutoka katika maeneo yao. Hakuna ubishi mtu
wa Mbeya ana haki ya kuipenda Mbeya City na wala asione haya.
Kuipenda Yanga ama Simba si dhambi, lakini si
lazima. Kama wewe ni Chinga, Ndanda FC imepanda, sasa huu ndiyo wakati wako wa
kuonyesha upendo na hauna sababu ya kuwa na woga.
Kweli timu hiyo inaweza isikufurahishe sana kwa
kuwa haina uwezo wa kuwasajili akina Paul Kiongera au Coutinho kutokana na
uwezo wake kifedha, lakini tukubaliane zinahitaji kukua.
Kukua kwake kunahitaji fedha kwa ajili ya
kuziboresha na kusajili wachezaji wa kiwango cha juu. Hawawezi kupatikana bila
fedha na ili fedha iingie, lazima kuwe na ushirikiano na mapenzi ya dhati.
Tumeona Mbeya City na wala msione haya
kuwatolea mfano kwa msimu wao mmoja uliopita kwamba watu walikuwa tayari kuona
timu yao inapata mafanikio na ndiyo maana ikafikia hapo, ndiyo maana kuna watu
wamekuwa tayari kuingiza fedha zao kwa Mbeya City.
Wako wengine ni wafanyabiashara jasiri kama
vile Bin Slum Tyres Ltd ambaye amekubali kuingiza fedha zake hadi Ndanda FC na
Stand United ambazo ndiyo zimepanda daraja na hazina lolote.
Mfanyabishara yeyote lazima awe makini kwenye
matumizi ya fedha anazoingiza. Kwa Ndanda au Stand lazima awe na hofu kwa kuwa
hajaona wanachofanya kwenye ligi kuu.
Lakini Bin Slum amefumba macho na kuwapa
udhamini, maana yake anawaonyesha viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu hizo
kuanzia mikoani mwao au kwingine kuwa wanapaswa kujitolea kwanza ili
kuhakikisha zinakuwa na mafanikio kwenye msimu wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
Wasitake mafanikio ya haraka kama Mbeya City au
kulazimisha mambo, badala yake angalau wabaki ligi kuu lakini uwezekano wa
kufanya vizuri zaidi upo.
Toto African kwa Mwanza ilionekana ni kama timu
ya upande fulani, wengine wakaipiga vita kwa juhudi kubwa na sasa hawawezi
kuona mechi za Ligi Kuu Bara kwa kuwa Mwanza hakuna timu, kitu ambacho ni
upuuzi mkubwa.
Yaliyotokea kwa Toto inawezekana kabisa
yatatokea Shinyanga na hata kule Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara kwa timu hizo
mbili kunusa ligi kuu na kuteremka kama wananchi wake hawatakuwa imara na
kuonyesha mapenzi.
Kuzipenda Simba na Yanga na kuisahau timu ya
mkoani kwenu hasa ukiwa unaishi hapo, si sahihi. Hiyo ndiyo inayokusaidia
kuzileta timu hizo za ligi kuu ukaiona ukiwa hapo nyumbani.
Wanaoweza kuzimaliza Ndanda na Stand United
watakuwa ni watu wa Mtwara na Shinyanga na si zaidi. Na tayari nilipokuwa
Shinyanga niliona kuna mgawanyiko kati ya Mwadui na Stand.
Lakini kuna kila sababu ya kuamini uzalendo ni
jambo namba moja na kama ni suala la mapenzi kwa Yanga na Simba, basi lifuatie
na nguvu za mapenzi ziwe kwa kile kilicho nyumbani kwenu na hii itazifanya
Yanga na Simba, zisikie joto la ushindani na wakati mwingine kujiimarisha zaidi
kuliko kuchukulia mambo rahisi kama zinavyofanya sasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment