Mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi, amefunguka na kumwambia kocha wake, Mzambia,
Patrick Phiri, kuwa nafasi yoyote atakayompanga uwanjani atahakikisha anafunga
tu, hivyo asipate taabu kujiuliza mara mbilimbili kuwa anafaa kucheza nafasi
gani hasa kati ya winga na straika.
Kauli
hiyo ya Okwi inakuja baada ya kuwepo kwa baadhi ya maoni kwa wadau kuwa,
mshambuliaji huyo ameshindwa kufumania nyavu ndani ya mechi tatu za kirafiki za
hivi karibuni kwa kuwa anapangwa kama namba tisa, kitu ambacho Okwi amekipinga
na kutoa msimamo wake huo.
Okwi amesema kuwa yeye ni mshambuliaji mwenye uwezo wa
juu na huwa haangalii anacheza wapi ili aweze kufunga kwa kuwa anajua suala
hilo ni jukumu lake, kwa hiyo atafunga tu bila ya kujalisha kama anacheza
kiungo, winga au mshambuliaji wa kati.
“Huku
kutokufunga kwenye mechi za hivi karibuni, imetokea bahati mbaya tu lakini si
kwamba eti nashindwa kufunga kwa kuwa nacheza mshambuliaji wa kati, kocha
anaweza kunipanga kokote pale anapopenda yeye na mimi nikafanya kazi yangu kama
kawaida wala haina shida.
“Mimi kazi yangu hasa ni kufunga na
kuisaidia timu kupata ushindi na naweza kuyafanya hayo hata nikicheza kiungo,
winga au mshambuliaji, kwa hiyo ni kocha mwenyewe atakapoona nafaa, akinipanga
mimi nitafanya kazi yangu,” alisema Okwi.
Tangu
Okwi atue Simba hivi karibuni akitokea Yanga, tayari ameshacheza mechi tatu za
kirafiki lakini zote hakuna aliyobahatika kutikisa nyavu. Mechi hizo ni dhidi
ya Gor Mahia ya Kenya waliyoshinda mabao 3-0, kisha URA ya Uganda waliyofungwa
1-0 kabla ya kuwavaa Ndanda wikiendi iliyopita na kutokananao suluhu.
0 COMMENTS:
Post a Comment