Na Saleh Ally
MAKAO makuu ya Yanga ni pale makutano ya
Jangwani na Twiga jijini Dar es Salaam, historia inaonyesha ujenzi wa jengo
hilo ulianza baada ya viongozi wa Yanga kutaka kufanya ukarabati kwenye jengo
lao la Mafia.
Kutokana na kutokuwa na fedha, wakafikisha
ombi kwa Rais wa Zanzibar, Abeid Amani Karume na kumueleza kuhusiana na ukarabati
wanaotaka kuufanya kwenye jengo lao la Mafia. Naye akawataka wafunge safari
hadi Zanzibar wakati wa sikukuu ya Pasaka ambayo alikuwa akiwaalika kama kawa.
Lakini Karume akatoa wazo kwamba Mwenyekiti wa Yanga Kondo
Salum Kipwata na katibu wake waende Zanzibar wakiongozana na kiongozi wa
Sunderland (sasa Simba), wakakubali.
Wakati huo Mwenyekiti wa Sunderland alikuwa
ni Ramadhani Kirundi, aliongozana na Kipwata na katibu wake hadi Zanzibar na
wakasherekea pasaka pamoja na baada ya hapo wakaingia katika mazungumzo ya
suala la zile fedha za ukarabati wa jengo.
Karume aliwaambia kuwa amesikia walichotaka,
akawaambia alikuwa na wazo la kujenga jengo moja ambalo Young African na
Sunderland wangelifanya makao makuu yao. Wazo hilo lilipingwa vikali na Kirundi
aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali za mkoa wa Dar es Salaam, ikiwemo nafasi
ya Meya wa mji huo.
Kutokana na msimamo wa Kirundu, Karume
aliamua kutoa kiasi cha Sh milioni 2 ambazo Young African ilianza kuzitumia kwa
ujenzi wa makao makuu ya klabu hiyo pamoja na Uwanja wa Kaunda.
Hata hivyo haikuwa lahisi baada ya zengwe
kuibuka na Manispaa ya Jiji kupitia wataalamu wake wa ujenzi walisema haikuwa
sahihi kujenga ghorofa katika eneo hilo lingeweza kuanguka na pia eneo hilo
lilitengwa maalum kwa ajili ya jalala.
Kutokana na zengwe kuwa kubwa, kwa mara
nyingine, Rais Karume aliingia suala hilo kwa kufikisha taarifa yake kwa Ikulu
ya Tanzania Bara na siku chache baadaye akasafiri hadi Dar es Salaam
akiongozana na mainjinia wa ujenzi kutoka nchini Ujerumani.
Aprili 4, 1971, Wajerumani walikamilisha
suala la kupima na kuweka msingi na Mwananchi Engineering Contracting Company
ndiyo ikafanya ujenzi huo.
Hata hivyo, wakati jengo linaanza nafasi ya
usimamizi ikawa chini ya MWenyekiti Mangara Tabu Mangara baada ya Kipwata
aliyafanya pilika zote za uongozi kufanikisha hilo, kufariki dunia.
Magari:
Achana na jengo tu au watu wengi kuona Yanga
inamiliki basi ambalo limetokana na udhamini, lakini wakati huo chini ya
Mangara, Yanga ilimiliki magari kadhaa.
Yanga ilikuwa na basi dogo aina ya Ford kwa
mkoa wa Arusha ilijulikana kama ‘Viford’, lilikuwa lina uwezo wa kubeba abiria
30, pia ilikuwa na basi kubwa aina ya Isuzu lililochukua watu 65, pia gari
ndogo aina ya Honda.
Hii inaonyesha kiasi gani Yanga iliendelea
kuwa na utajiri mkubwa chini ya uongozi wa Mangara ambaye alikuwa mmoja wa
viongozi imara waliowahi kupita Yanga.
Jengo la Mafia:
Hili ndiyo jengo kongwe zaidi kwenye klabu
ya Yanga, kabla ya kupatikana kwa jengo hilo, Yanga ilikuwa ikifanya kazi ya
kuhama sehemu moja kwenda nyingine tokea ikijulikana kama New Youngs na hata
baadaye ‘Simba’ walipojitenga, nao wakapanga pia.
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti Jabir
Katundu akaamua kubuni mpango wa kupata nyumba ambayo itakuwa makao makuu ya
klabu. Ukafanyika mkutano na makubaliano yakafikiwa kualika timu kutoka Kenya.
Ikaalikwa Abaluhya ambayo ilikuwa kali na
inakubalika. Ikatua na kucheza na Yanga na mapato yote, hata wachezaji
hawakupewa posho, yakatumika kununua kiwanja na baadaye kuanza ununzi wa nyumba
ya Mtaa wa Mafia.
Nyumba ya Mafia ilikuwa ya Sunderland, ndiyo
mashabiki wa Yanga walizoea kusema wakati huo, lakini ukweli ni kwamba nyumba
ile ilikuwa inamilikiwa na shabiki na mwanachama wa Sunderland.
Shabani Feruzi ndiye alikuwa mmiliki wa
nyumba hiyo kwa jumla ya Sh 17,000 tu. Mmiliki alichukua Sh 13,500 na
zilizobaki zilitumika kuwalipa madalali pamoja na wengine waliohakikisha
ununuzi unafanikiwa.
Katika mechi dhidi ya Baluhya, Yanga ilipata
fedha nyingi sana, zilikuwa ni Sh 21,300. Hivyo fedha nyingine zikatumika
katika mambo mengine ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kupaka rangi za jengo na
kuindoa nyeupe na nyekundu aliyokuwa amepaka mmiliki wa awali ambaye ni mnazi
wa Sunderland.
Historia ya Yanga:
Young African ina historia ndefu lakini
ukweli ndiyo klabu ya kwanza ya Waafrika ambayo ilijiimarisha na baadaye kuwa
mfano kwa nyingine.
Ilianzishwa mwaka 1935 kwa jina la New
Youngs, makao makuu yake yalikuwa pale Mwembe Togwa, kwa mara ya kwanza
ikasajiliwa rasmi Februari 12, 1935.
Mwembe Togwa kwa sasa ni maarufu kama Fire,
Kariakoo. Kutokana na kusaka maendeleo, New Youngs ilikwenda inahama taratibu
hadi ilipobadilishwa jina na kuwa Young African, siku kadhaa baada ya wengine
kujitenga na kuanzisha klabu ya Stanley ambayo baadaye ilikuja kuwa Sunderland halafu
Simba.
Wakati inaanzishwa ilikuwa klabu pekee ya
Waafrika hasa wazalendo wenye maisha ya kawaida, Waafrika wachache
walijichanganya kwenye klabu za Wazungu na Waasia kama Aga Khan, Goans Club,
European Club na Yatch Club na ilipozaliwa Sunderland ndiyo ikawa klabu ya pili
ya weusi.
Wakati huo kiongozi mkuu wa klabu ambaye
sasa ni mwenyekiti, aliitwa Patron na rekodi zinaonyesha mwenyekiti wa kwanza
ni Athumani MWinyichande na katibu wake ni Mwichande Chonjo.
Maisha ya makao makuu ya klabu yalikuwa ni ya
kutangatanga, baada ya kutoka Mwembe Togwa, klabu ilihamia Mtaa wa
Udowe/Sikukuu, halafu ikahamia Sikukuu/Mafia na baadaye Mtaa wa Lumumba.
Juhudi zikafanyika kwa mchango wa mechi
moja, uongozi ukafanikiwa kununua nyumba yake pale Mafia. Halafu ndipo zilipotolea
fedha la Rais Karume mpango wa kujenga makao makuu na Uwanja wa Kaunda
ukafanyika, sasa nyumbani kwa Yanga ni mtaa wa Twiga na Jangwani.









0 COMMENTS:
Post a Comment