September 20, 2014


PAMOJA na historia zinazogongana lakini ukweli kabla ya jina la Simba, kulikuwa na majina kadhaa yalipita wakati wa uasisi wa klabu hiyo.

Kweli klabu hiyo ilizaliwa mwaka 1936 baada ya kujitenga kutoka kwa New Youngs ambayo sasa ni Dar Young African au Yanga kutokana na watu hao waliokuwa timu moja kupingana baada ya kutoridhishwa na uendeshwaji wake.
Waliojitenga ambao wengi walikuwa ni wasomi ambao walisisitiza wakitaka mambo yao kuendeshwa kisomi waliunga timu inayoitwa Eagle Night na katika miaka ya 1940 wakaibadlisha na kuibandika jina la Sunderland.
Hapo ndiyo chimbuko la kuvaa jezi za rangi nyekundu kama ilivyo Sunderland ya England lilishika kasi lakini mwaka 1971, jina Simba likazaliwa rasmi.
Pamoja na hivyo kumekuwa na taarifa kwamba Simba imewahi kuitwa Queens Sports Club, lakini bado wengi wamekuwa wakipinga kwamba hakukuwahi kuwa na jina hilo au lilipendekezwa na halikuwa kutumika zaidi ya lile la Stanley katika kipindi hicho.
Waliojiondoa New Youngs na kuunda timu mpya ni baada ya kufanya vibaya kwenye Ligi Daraja la Kwanza Tanganyika mwaka 1936 baada ya kushinda mechi tatu tu kwenye ligi hiyo na kuishia kushika mkia baada ya mechi 12.
Mzozo ulitokana na upangaji wa timu na kwa sababu New Youngs ilikuwa ndiyo imepanda daraja kwa kufanya vizuri sana daraja la pili, baadhi ya waliojiengua waliona hakukuwa na umakini pia katika suala la kujali gharana kama ile ya Sh 15 ya ada ya ushiriki wa ligi.
Bado waliona gharama zilikuwa nyingi, mfano zilizotumika kununua vifaa kwa ajili ya wachezaji na ushonaji wa jezi. Kikubwa kwao waliona mambo hayaendi kisomi, au kimpangilio, hivyo wakaunda timu mpya na ndiyo mwanzo wa kuzaliwa na Simba ambao wamekuwa wakiita ni wataratibu, waelewa na wanaopenda soka la kutandaza badala ya lile la haraka na kukurupuka.
Jina Stanley lilikuwa ni la Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Uingereza ambao walikuwa watawala wa Tanganyika wakati huo. Jina la mkoloni huyo lilikuwa pia ni la moja ya barabara za mitaa ya Dar es Salaam ambako yalikuwepo makao makuu ya klabu hiyo ilipoanza.
Kwa sasa barabara ya Staley inajulikana kama barabara ya Aggrey ambayo ni moja ya mitaa maarufu sana jijini Dar es Salaam.
Lakini sababu nyingine zilizoelezwa kujitenga kwa vijana hao waliamini ulikuwa ni wakati mwafaka wa kuongeza timu nyingi za Waafrika au wenyeji ili waweze kupambana na timu za Waasia na Wazungu ambazo ndiyo zilionekana kufanya vizuri huku zile chache za wenyeji zikipanda na kushuka daraja kila kukicha wakati wa ligi iliyokuwa ikiendeshwa kwenye Viwanja vya Gymkhana.




1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic