Na Saleh Ally
JINA la Hassan Dalali ndiyo linaonekana kuwa
na heshima zaidi kwa wenyeviti waliowahi kupita au waliopo katika Klabu ya
Simba Sports Club ya Dar es Salaam, Tanzania.
Dalali ambaye aliiongoza Simba kutokea 2006 na
kukabidhi madaraka 2010, baada ya kuwa ameongezewa miezi sita kutokana na
wanachama kuona wakifanya uchaguzi wataivuruga klabu yao, amekuwa kipenzi zaidi
cha mashabiki na wanachama.
Katika mahojiano maalum na SALEHJEMBE,
Dalali anasema anastahili kuwa kipenzi cha Wanasimba kwa kuwa ni mwenyekiti
anayekufa maskini, hadi leo maisha yake ni magumu, mfano mzuri, anaishi bondeni
na yote hiyo ni mapenzi yake kwa Simba.
Dalali anasema ameifanyia mengi Simba ambayo
itakuwa ngumu kwa mwenyekiti au kiongozi yeyote kukubali kufanya kwa kuwa
mapenzi yake ya Simba ni vigumu kufanya hivyo.
“Nilikuwa ninabeba maji ya wachezaji wakaoge,
usidhani nilifanya hivyo kwa nia tofauti. Lakini nilitaka kuwaonyesha kwamba
nataka washinde mechi dhidi ya Yanga na kocha Phiri akaweka kikao na kuwaeleza
kama mzee anabeba maji nyie muoge, basi lazima mshinde, kweli ujanja wangu
ukafanikiwa tukawapiga Yanga.
“Nakufa masikini kweli, lakini sijilaumu.
Niliwahi kukataa gari nikataka Simba ipewe fedha. Kuna Mwanasimba mmoja
aliniona nikiwa kwenye daladala naenda mazoezini, ikamuuma, kesho yake
akanitafuta na kuniita ofisini.
“Sipendi kumtaja, alinieleza niende Pugu Road
kuchagua gari kwa ajili ya matumizi yangu, nikakataa kwa kuwa Simba haikuwa na
fedha na wachezaji wanakunywa maji ya viroba ya Sh 50.
“Alitoka nje ofisini kwake na kunipa dakika 10
nijifikirie, aliporudi msimamo wangu ukawa uleule, kuisaidia Simba.
“Basi kwa kuwa ni mtu mkubwa, akasema
atufanyie mpango tupate wadhamini na ndiyo mwanzo wa kupatikana kwa TBL ambayo
hadi leo inalipa mishahara ya Simba,” anasema Dalali, sura yake ikionyesha
upole, anaongeza:
“Nimepita kwingi sana, wakati fulani Simba
hatukuwa na fedha, licha ya umasikini wangu nikachukua jokofu la kwanza
nikauza, fedha hazikutosha, nikachukua la pili, nikauza tena ili kusaidia mambo
yaende vizuri ndani ya kikosi, nakumbuka bado fedha hazikutosha, kiongozi
mwenzangu Chano Almasi akaweka rehani gari lake.”
Dalali anaendelea kujivunia kwamba amefanya
mengi makubwa akiwa kiongozi Simba ingawa imekuwa vigumu wengi kukumbuka au
kulitambua hilo.
Umoja:
Mimi ndiye niliyerudisha umoja Simba baada ya
kuikuta imevurugika kabisa, kipindi hicho kuna ugomvi mkubwa kati ya Friends of
Simba (Fos) na uongozi.
Wanachama zaidi ya 600 walifutwa kwenye
mgogoro huo, nikaanzisha zoezi jipya la kadi, nikawarudisha nikilenga kurudisha
umoja.
Hatukuwa na fedha kabisa, nikaamua kuanzisha
kundi la Fans of Simba ambalo lilisaidia sana kipindi hicho angalau kuwasaidia
wachezaji kupata mishahara.
Nakumbuka ilikuwa mwaka 2007, kweli mtu ninayemshukuru
zaidi kwa kipindi hicho ni Dioniz Malinzi ambaye alituma Sh milioni 80 kwa
ajili ya usajili.
Kipindi hicho hali ilikuwa mbaya sana wakati
naingia, wachezaji walikuwa wanakunywa yale maji ya pakti ya Sh 50 (kabla
serikali haijayapiga
marufuku).
Mwisho nilimkabidhi Rage Simba moja, yenye
mafedha, isiyofungika, yenye wanachama 5000 kutoka 500 niliowakuta, yeye
akaivunja na kuifanya iwe Simba poa inayofungika kirahisi na isiyo na kitu,
ndiyo maana nasema uongozi wa Simba una kazi kubwa, lazima utulie.
Simba Day:
Hakuna ubishi Simba Day ndiyo tamasha kubwa
zaidi la soka nchini, Yanga na timu nyingine zinaweza kuiga, hakuna sababu ya
kuona aibu, ni jambo zuri na utaona linavyowakutanisha Simba.
Mimi ndiye nilitoa ushauri wa kuanzishwa
kwake. Nakumbuka tulikuwa tumekaa pamoja na viongozi kama Kassim Dewji,
Mohammed Nassor ‘Kigoma’, Salim Try Again, Mwina Kaduguda na wengine,
nikawaeleza wazo langu, wakaliunga mkono, likafanyiwa kazi.
Kiongozi mmoja tu, Gumbo ndiye alikuwa hataki
kabisa, nakumbuka hadi tulizozana na mimi nikamuanzishia msala kwamba ni Yanga
kwa kuwa mwaka 1969 aliwahi kupewa Sh 3,000 ili ajiunge na Yanga, akakubali
lakini viongozi wakaingilia na kusitisha zoezi hilo.
Wadhamini:
Pamoja na uongozi wangu kusaidia kupatikana
kwa TBL na wao wakasema Yanga lazima wawepo, mimi ndiye niliwapata Push Mobile
ambao pia wamekuwa wakiingiza fedha Simba.
Niliisaidia kupata wadhamini, ikaweza kusimama
yenyewe na sasa ndiyo nguzo ya klabu.
Uwanja:
Uongozi wa (Ismail Aden) Rage umekuwa
ukijivunia uwanja, lakini ukweli sisi ndiyo tulioununua uwanja huo wakati wa
uongozi wangu kule Bunju.
Tuliambiwa Sh milioni 106, tukaanza kulipa
kidogo hadi tulipopewa nyaraka za kuumiliki, baadaye tukaukabidhi uongozi wa
Rage.
Niwe mkweli, najivunia sana uwanja huo na
ikifika siku Simba ikaanza kuutumia itakuwa faraja kwangu.
Simba B:
Kwa mara ya kwanza inaanza kuwa imara ni kile
kipindi changu kwa kuwa niliamini watoto hao watatusaidia baadaye kama
ilivyokuwa zamani.
Wakati naingia, ukata uliimaliza hata Simba ya
wakubwa, isingekuwa rahisi kuwalea watoto, lakini nilijitutumua na kuipa uhai na
wengi leo ni tegemeo Simba.
Ubingwa:
Katika uongozi wangu wa miaka mitatu,
nilichukua ubingwa mara mbili nikakosa mara moja nikiwa katika nafasi ya pili.
Huo mwaka tuliokosa ubingwa, kosa lilitokana na
meneja wetu wa timu kujisahau akamchezesha Juma Nyosso katika mechi dhidi ya
Coastal Union.
Wakati huo kocha alikuwa Patrick Phiri, hakujua
kama ni sahihi au la. Hivyo Coastal wakakata rufaa, tukapokonywa pointi tatu,
tukaukosa ubingwa kwa tofauti ya pointi mbili.
Ubingwa nilitwaa msimu wa 2007-08 (ligi
ndogo), tuliwafunga Yanga Morogoro. 2008-09, tukashika nafasi ya pili na
2009-2010 tukabeba ubingwa bila kufungwa hata mechi moja.
Rekodi:
Msimu wa 2009-10, tulitwaa ubingwa bila ya
kupoteza hata mechi moja. Usisahau, tulitoka sare mechi mbili tu dhidi ya Kagera
na African Lyon.
Maana yake, atakayetaka kuivunja, atalazimika
kushinda mechi zote au kama ni sare, apate moja tu.
Nembo:
Wakati naingia madarakani niliikuta Simba
ikitumia nembo yenye simba wawili kushoto na kulia.
Nikachukua uamuzi wa kijasiri na
kuwabadilisha, ingawa ilikuwa vigumu kwa wengi kukubali lakini nikapitisha
uamuzi wa kutengeneza nembo yenye Simba mmoja tu, nikimaanisha Simba ni moja na
si zaidi ya hapo.
Kukataa Sh milioni 3:
Mwaka 2004 niliamua kugombea umakamu
mwenyekiti dhidi ya Charles Masanja. Mtu mmoja ambaye ni tajiri hata sasa
tunafahamiana akajitokeza na kutaka kunipa Sh milioni 3 ili nijitoe.
Ingawa maisha yangu yalikuwa magumu, nilikuwa na
njaa kweli, nilikataa katakata.
Mwisho nikashindwa kwenye uchaguzi, lakini sikujuta
kwa kuwa Sh milioni 3, haikuwa na thamani ya mapenzi yangu kwa Simba.
Mimi najua maana ya Simba kwa kuwa nimepita
kila hatua, kuanzia mwanachama, komandoo hadi kiongozi nikianza na mwenyekiti
wa matawi wilayani Dar es Salaam, mwaka 1995 nikagombea ukatibu uenezi
nikashindwa na Rashid Mchatta, mwaka 2004 nikashindwa umakamu na Masanja. Halafu
2006 nikashinda uenyekiti, utaona kwamba sikuwa nabahatisha.
WENYEVITI 1965 HADI 2014:
1.
Ramadhani Kirundu-1965-1970
2.
Abubakary Mwilima 1970-1974
3.
Joachim Kimwaga 1974-1975
4.
Emanue Makaidi 1976-1977
5.
Joachim Kimwaga 1977-1978
6.
Alfred Sanga 1979-1982
7.
Joachim Kimwaga 1983-1986
8.
Emanuel Mkaidi 1987-1988
9.
Juma Sakum Uhovuge 1989-1992
10. Mikidadi Kasanda 1992-1993
11. Amiri Ali Bamchawi 1993-1994
12.
Ismail Rajabu Kaminambeho 1995-1998
13.
Yusuf Hazari 1999-2000
14.
Juma Salum Uhovuge 2000-2001
15. Ramadhani Balozi Alikamu 2001-2003
16. Ayubu Saleh Chamshama 2004-2005
17. Hayaz Mruma Mkt/Muda 2005
18.
Michael Richard Wambura 2006 (Kamati ya Sarungi)
19.
Hassan M. Dalali 2006-2010
20.
Ismail Aden rage 200-2014
21.
Evans Elieza Aveva 2014-2018
0 COMMENTS:
Post a Comment