KIPRE |
GUMZO na habari ya mjini hivi sasa ni mechi ya Ngao ya Jamii,
itakayowakutanisha wapinzani wakubwa hivi sasa, Yanga na timu inayokuja kwa
kasi kuleta mabadiliko ya soka nchini, Azam FC.
Timu hizo zinatarajiwa kujitupa uwanjani kesho Jumapili katika mechi
hiyo ya Ngao ya Jamii kama ishara ua ufunguzi wa pazia la msimu mpya wa Ligi
Kuu Bara 2014/2015.
Kila timu imefanya usajili wa kutosha katika kukiimarisha kikosi
chake pamoja na maandalizi, ikiwemo Yanga kwenda kupiga kambi yake Pemba na
Unguja huko visiwani Zanzibar na Azam wakishiriki michuano ya Kombe la Kagame
ambapo walitolewa hatua ya robo fainali.
Katika mechi iliyowakutanisha timu hiyo kwenye Ngao ya Jamii msimu
uliopita, Yanga walifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na kiungo
mkabaji aliyetokea kwenye majeraha, Salum Telela.
Wakati Yanga wakiifunga Azam FC katika mchezo wa Ngao ya Jamii,
yenyewe ilifanikiwa kuweka rekodi ya kuwafunga katika mechi ya mzunguko wa pili
wa ligi kuu mabao 3-2 huku wakitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa mzunguko
wa kwanza.
Katika mechi ya kesho, Yanga wataingia uwanjani wakiwa na kocha wao
mpya, Mbrazili, Marcio Maximo anayesaidiana na Leonardo Neiva, Salvatory Edward
na Shadrack Nsajigwa ‘Fusso’.
COUTINHO |
Wakati Maximo akiwa ni mara yake ya kwanza kukutana na Azam FC,
kocha mkuu wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph Omog, mwenyewe atakaa benchi akiwa
amekutana na timu hiyo mara moja kwenye mechi ya mwisho iliyomalizika kwa sare
ya bao 1-1.
Katika mechi hiyo, kila moja inahitaji ushindi ili kujiwekea heshima
baada ya msimu uliopita timu hizo kufungana mara moja huku mchezo mmoja
wakitoka sare.
Kwa upande wa Maximo mwenyewe anatumia mifumo mitatu, nayo ni 4-4-3,
4-5-1 na 4-3-3, anasema kuwa mechi hiyo ni ‘deby’ kwao kutokana na upinzani
uliopo wakati timu hizo zinapokutana.
“Mimi kama kocha sera yangu ni kwamba, ninataka kila timu ikiwa
uwanjani nichukue pointi tatu, ninataka kila mechi ushindi ili mashabiki wa
Yanga niwape raha.
“Hivyo nitaingia uwanjani kucheza na Azam FC nikiwa na lengo moja
pekee la ushindi katika mechi hiyo, ninajua wenzetu wamejiandaa, pia sisi
tumejiandaa.
“Kikosi kimeimarika kila sehemu kutokana na kambi tuliyoiweka huko
Pemba na Unguja katika kuhakikisha timu inafanya vizuri, ninawaomba mashabiki
waje uwanjani kuipa sapoti timu yao,” anasema Maximo.
Kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wapya Wabrazili, Geilson Santos
Santana ‘Jaja’ na Andrey Coutinho ambao ni hatari katika safu ya ulinzi ya Azam
FC, wengine ni Said Juma, Pato Ngonyani na Edward Charles.
Ukiiangalia Yanga, yenyewe imekamilika katika kila safu ya uchezaji
kutokana na maboresho yaliyofanywa na Maximo, katika mchezo huo timu hiyo
huenda ikamkosa Coutinho kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu aliyoyapata
kwenye mechi dhidi ya Polisi Dar es Salaam na Jerry Tegete aliyeumia nyonga
katika mechi hiyo.
Kukosekana kwa Coutinho ni pengo katika kikosi hicho kutokana na
umuhimu wake ndani ya uwanja kwani yumo kwenye First Eleven ya Maximo.
Naye Omog anasema kuwa, ataingia uwanjani kwa ajili ya kazi moja
pekee ya ushindi katika mechi hiyo na anaamini kikosi chake kimeimarika kwa
ajili ya ushindani katika mchezo huo.
Kocha huyo anatumia mfumo wa 4-4-2 na 4-5-1 ambayo wakati wowote
anatarajiwa kuibadilisha kutokana na aina ya mechi.
Usajili wa Azam FC unaundwa na mshambuliaji Mhaiti, Leonel Saint
Preux, Didier Kavumbagu na Frank Domayo, wawili hawa walikuwa wanaichezea Yanga
msimu uliopita.
Kwa upande wa Domayo, hataicheza mechi hiyo kutokana na kuugua
majeraha ya nyama za paja ambayo yamesababisha afanyiwe oparesheni. Mwingine
mpya ni Ismail Diara wa Mali.
Katika kikosi cha Azam FC, mchezaji wa kuchungwa ni Kipre Tchetche,
Leonel na Kavumbagu kutokana na usumbufu wao ndani ya uwanja, pia uwezo wao wa
kufunga mabao.
Vikosi -Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’,
Juma Abdul, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Simon Msuva,
Hassani Dilunga, Geilson Santos ‘Jaja’, Mrisho Ngassa na Haruna Niyonzima.
Azam FC:
Aishi Manura, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Said Morad, Aggrey
Morris, Kipre Balou, Abubakari Salum ‘Sure Boy’, Kipre Tchetche, Leonel na
Khamis Mcha.
0 COMMENTS:
Post a Comment