Na Saleh Ally
REKODI inaonyesha kwa mara ya kwanza Arsenal na Man City zilikutana
Jumamosi ya Desemba 1893 kila moja ikiwa na jina tofauti na lile la sasa.
Man City ilikuwa nyumbani katika mechi hiyo ikijulikana kama
Ardwick, ikalala kwa bao moja dhidi ya Arsenal ambayo iliitwa Woolwich. Mechi
iliyofuata, City ikalala tena kwa bao moja.
Baada ya hapo timu hiyo kutoka katika miji yenye upinzani mkubwa
kisoka ya Manchester na London, zimeendelea kuwa na upinzani mkubwa.
Mechi zao zinawavuta mashabiki wengi kwa kuwa Arsenal haitaki
kupoteza dhidi ya timu za Mji wa Manchester, hii ni rekodi ya kila upande
kutaka kuonekana unajua sana mpira kuliko mwingine.
Leo kazi inaendelea, ndani ya Uwanja wa Emirates, Arsenal wanakuwa wenyeji
na wana rekodi nzuri ya kuifunga Man City mabao mengi wanapokuwa nyumbani.
Mechi ya mwisho zilipokutana katika Ngao ya Jamii, Arsenal iliibuka
na ushindi wa mabao 3-0. Hii inaonyesha kufunga mabao mengi zaidi ya hayo
inawezekana.
Lakini mvuto na utamu wa mechi unaongezeka zaidi kwa kuwa City
hawawezi kukubali kufungwa kirahisi mara mbili mfululizo huku wakijua kulivyo
na umuhimu wa kushinda mechi za kwanza za ligi.
Ligi Kuu England, biashara ni asubuhi; ukilala mapema, basi hata
kuamka itakuwa shida na mwishoni mwa ligi mambo yanakuwa magumu.
Kila upande una wachezaji nyota ambao wanaweza kufanya matokeo yawe
tofauti, mfano Arsenal wakiwa nyumbani, watu kama Jack Wilshere, Santi Cazorla,
Mesut Ozil, Alexis Sanchez, Yaya Sanogo na sasa Danny Wilbeck ambaye atakuwa na
kazi ya kuonyesha kwamba hakukosea kutua London akitokea Manchester United.
Lakini City shughuli yao ni pevu, Yaya Toure, Jesus Navas, David
Silva, Stevan Jovetić, Edin Dzeko, Kun Aguero na bado wana vifaa vingine kibao.
Hivyo ni mechi ambayo itakuwa na ufundi zaidi ukizingatia kila
upande una kocha bora, Arsene Wenger wa Arsenal na Manuel Pellegrini wa Man
City.
Kila timu ina uwezo wa kubadili matokeo kupitia sehemu nne. Kuanzia
kwa makocha ambao ni wazoefu na wajuzi na kila mmoja amewahi kuonja utamu wa
ubingwa wa England.
Lakini safu za ulinzi ni imara lakini zina wachezaji ambao wana
uwezo wa kufunga mabao ya vichwa kama watapata nafasi ya kona au mipira ya
adhabu itakayotupiwa langoni.
Viungo, unaweza ukasema mechi ya leo ni ya viungo. Mechi
inayowakutanisha mafundi na bila shaka kila upande utaonyesha uwezo wa juu na
hakuna ubishi, mpira utachezwa sana katikati.
Sehemu ya mwisho ni washambuliaji ambao kila upande uko vizuri
ingawa kiwango cha ufungaji kwa msimu uliopita, Man City wanaonekana wako
vizuri zaidi.
Bado unaweza kuachana na hadithi ya mla jana, halafu ukasubiri leo
na kuangalia nani atafanya vizuri zaidi.
Safu hii ya ulinzi itakuwa imara au fowadi gani itatupia zaidi.
Hakika itakuwa ni mechi ya burudani.
Tangu 2010:
Wakali hao wamekutana mara tisa tangu msimu wa 2010-11, kati ya hizo
saba ni za Premier League moja ya Kombe la Ligi na nyingine moja, Ngao ya
Jamii.
Arsenal inaonekana si wababe kwa Man City kwa kuwa katika mechi zote
hizo, wameshinda mbili ile ya 1-0 iliyopigwa Aprili 8, 2012 Arsenal ikiwa
nyumbani Emirates na ya mwisho ya Ngao ya Jamii ambayo waliibuka na ushindi
mnono wa mabao 3-0.
Man City ndiyo wanaonekana kuwa wababe zaidi kwa kuwa katika mechi
tisa, wameshinda mechi nne sare ni tatu za mabao 1-1 mara mbili na suluhu.
Kwa kipindi cha miaka yote mitatu, Man City ndiyo wameonekana kuwa
wababe zaidi kwa kuwa hata mechi ambayo imekuwa na idadi kubwa ya mabao, wao
ndiyo waliibuka na ushindi.
Desemba 14, 2013, Man City iliicharaza Arsenal kwa mabao 6-3 katika
mechi ambayo wengi hawakuamini, lakini City walitawala mchezo na kupata mabao
mengi zaidi.
Mabao Mengi:
Mechi mbili zilizozikutanisha timu hizo ndiyo zilikuwa zina mabao
mengi, moja Arsenal wakishinda na nyingine City nao wakishinda.
Mechi ya kwanza iliyokuwa ina mabao mengi zaidi ni ile ambayo
ilikuwa na jumla la mabao 10. Arsenal ndiyo ilishinda kwa mabao 7-3.
Nyingine ambayo ilikuwa ina mabao mengi zaidi ni ile yenye 9, ambayo
City walishinda kwa mabao 6-3 dhidi ya wageni wao vijana wa Wenger.
Usisahau mwaka 1956, Arsenal tena ilishinda kwa idadi kubwa kama
hiyo ya mabao 7-3 katika mechi ya Ligi Kuu England.
Rekodi zinaonyesha Arsenal inaongoza kwa kushinda kwa mabao mengi
zaidi dhidi ya Man City lakini yenyewe imepoteza zaidi.
Maana yake kwa mechi moja, Arsenal ndiyo imetikisa mara nyingi zaidi
ngome ya Man City, maana imefunga mabao saba na City kwa mechi moja, mabao
mengi zaidi ni sita.
Msimu huu:
Kila timu imecheza mechi tatu tayari katika msimu wa 2014-15 na Man
City iko katika nafasi ya nne ikiwa na pointi sita baada ya kushinda mechi
mbili na kupoteza moja kwa bao 1-0 dhidi ya Stoke City ambao sasa wamekuwa
wababe wao.
Arsenal iko katika nafasi ya saba, nafasi ambayo msimu uliopita
ilikuwa na mwenyewe ambaye ni Manchester United.
Arsenal imeshinda mechi moja, sare mbili na haijapoteza. Ina pointi
tano ikiwa na maana itapambana zaidi kuongeza idadi ya ushindi na kuzuia kupoteza.
Idadi ya mabao ya kufunga, Arsenal imefunga matano na kufungwa
manne, kihesabu safu yao haijakaa vizuri sana kwa kuwa tofauti ya mabao
inaonyesha wana uwezo wa kufunga mengi lakini ni rahisi kufungwa mengi pia.
Kwa upande wa City wao wamefunga mabao matano, hii inaonyesha safu
yao ya ushambuliaji ina makali sawa na ile ya Arsenal.
Lakini safu ya ulinzi ya City ni ngumu ukilinganisha na ile ya
Arsenal kwa kuwa imefungwa mabao mawili tu katika mechi tatu.
0 COMMENTS:
Post a Comment