Na Saleh Ally
YANGA ni klabu iliyoshiriki
kwa nguvu katika kutafuta Uhuru wa Tanganyika ambao baadaye ulipatikana mwaka
1961 na kujiondoa kwenye mikono ya Waingereza waliokuwa watawala.
Sehemu moja ya kuonyesha
kuwa kweli Yanga ilishiriki ni nembo yake ambayo hadi leo imekuwa na alama ya Bara
la Afrika ikiwa ni sehemu ya kusisitiza kuwa Waafrika wanapaswa kujitegemea
bila ya kuongozwa na watu kutoka nje ya bara hilo.
Wakati wa utawala wa
kikoloni, hakukuwa na nafasi ya kutosha kwa Waafrika kusimama na kujieleza
kuhusiana na walichotaka kwa uwazi, badala yake mambo mengi yalilazimika
kufanyika kwa siri kuhofia adhabu kutoka kwa wakoloni.
Jina la Young African
ilikuwa ni sehemu ya dhana, kwamba linawabeba Waafrika vijana, hivyo ikawa rahisi
kuihusisha klabu na wazalendo waliokuwa wakitaka kwa dhati uhuru wa nchi yao
ambao ulikuwa lazima upiganiwe.
Kuanzia mwaka 1951, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, alikaribishwa na wazee waliokuwa Yanga na walikuwa
tayari kushirikiana naye. Baadhi yao ni akina Dunstan Omar, Sheikh Suleiman
Takadir, Idd Faiz Mafongo, Ally Sykes, Abdulwahid Sykes, Juma Sultan ‘Mabosti’,
Said Chaurembo, Sheikh Jumbe Tambaza, Bibi Titi Mohammed, Tatu Binti Mzee na
wengine wengi.
Wakati huo Nyerere alikuwa
mwalimu katika Sekondari ya St Francis (sasa Pugu), mikutano ilianza kufanyika
kwenye makao makuu ya Yanga ikiwa inahamasisha Watanganyika kuzungumzia unyonge
wao ndani ya nchi yao na baada ya hapo kuanza kudai uhuru.
Mkutano hiyo
haikuwafurahisha wakoloni hata kidogo, mara nyingi walituma mashushushu na
kutaka kujua kilichokuwa kikiendelea ndani. Lakini Nyerere na wenzake wa Yanga
waliamua kubuni mbinu tofauti kuwakwepa.
Kwa kuwa hakukuwa na ujanja
wa kuhama katika eneo hilo na kufanya mikutano kwingine, mbinu mbadala moja
wapo ilikuwa ni kukifanya kikundi cha taarabu cha Jipisheni kuendelea
kutumbuiza kila walipoanza vikao.
Kikundi hicho ambacho
baadaye kilipewa jina la Egyptian Musical Club, kiliendelea kutumbuiza huku
watu wakishangilia kwa nguvu. Ingawa kelele zilikuwa juu, lakini Nyerere na
wanachama wengine wa Yanga ambao pia walikuwa wanachama wa Tanu waliendelea na
mikutano yao kuhakikisha wanafikia malengo.
Mwasisi wa kikundi hicho
cha taarabu, Maalim Bom Hambaroni, yeye alijitolea ikiwa ni sehemu ya mchango
wake na wanamuziki wa kikundi hicho wakakubaliana na hilo kila mmoja akiwa
amepania kuona siku moja wanakuwa huru.
Baadhi ya wanamuziki wa
kikundi hicho na wanachama wa Yanga walipokezana kuimba huku wengine wakipika
chakula ambacho Nyerere, viongozi wa Yanga na wanachama wa Tanu walikula na
baadaye kuendelea na vikao vyao hivyo vya ukombozi wa Tanganyika.
Mara kadhaa, katika baadhi
ya mechi, klabu ya Yanga ilitoa kiasi cha fedha na kuhakikisha kinaisaidia Tanu
katika mambo yake kadhaa ya kichama kwa lengo la kufanikisha upatikanaji wa
uhuru.
Kutokana na ushirikiano wa juu aliokuwa akiupata kutoka Tanu
na Yanga, Nyerere aliamua kuacha kazi yake ya kufundisha ili apate nafasi ya
kutosha kupambana kusaidia kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika.
Alianza kuzungumza kila
sehemu Tanganyika, dereva akiwa ni Said Tanu, ambaye alikuwa shabiki wa ‘kulia’
wa Yanga na aliwahi kueleza kwamba nje ya siasa, mwalimu alizungumza sana
kuhusu mpira na Yanga ndiyo iliyokuwa ikiukosha moyo wake.
Baadaye kwa ushirikiano wa
Tanu, wananchi wengi, Nyerere alifanikiwa ku ipatia
Uhuru wa Tanganyika, rasmi Desemba 9, 1961.
Uhuru wa Zanzibar:
Uhuru wa Zanzibar pia Yanga
ilishiriki kwa kuwa mwanamapinduzi namba moja, Abeid Amani Karume alikuwa
anapenda sana mpira na ndiye mwanzilishi wa klabu ya African Sports ya
Zanzibar.
Wakati fulani hata kabla ya
uhuru wa Tanganyika, viongozi wa Yanga walialikwa Zanzibar na Karume. Wakiwa
kule Yanga na African Sports, wakafanya mkutano wa kutaka kudumishwa undugu kwa
watu wa Bara na wale wa visiwani.
Mikutano ilikuwa miwili,
mmoja ulifanyika Zanzibar na mwingine ukafanyika Dar es Salaam, lengo lilikuwa
ni hilo kusaidia kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika pia Zanzibar.
Mfano timu hizo ziliandaa
mapambano mawili, moja likachezwa visiwani na fedha zikaichangia ASP kuendelea
kupambana dhidi ya wakoloni, halikadhalika mechi nyingine ikapigwa Bara na
fedha zikaisaidia Tanu kwa lengo lilelile.
Katika mechi iliyochezwa
Kajengwa Makunduchi, Zanzibar na ile ya Ghymkhana (sasa Karume), watazamaji
walikuwa wakiingia wanalipa kwa kuweka fedha kwenye vibubu moja kwa moja ili
kudhibiti mapato.
Ndiyo maana hata baada ya
Zanzibar kupata uhuru, Karume alikuwa akizialika ikulu klabu za Yanga, Simba,
African Sports ya Tanga na ile ya Zanzibar kwenda kusherekea sikukuu mbalimbali
kama pasaka au Idd.
Kwa hayo hii ni sehemu ya
kuonyesha Yanga ilishiriki kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa uhuru wa Tangayika,
Zanzibar au Tanzania kwa ujumla na ndiyo maana ilipewa jina la timu ya
wananchi.
Muungano:
Yanga inaelezwa kuwa sehemu
iliyochangia kwa kiasi fulani kupatikana kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ambao ulizaa Tanzania. Maana ndiyo zilichangia Nyerere na Karume kuwa karibu na
suala la kuungana likaanza.
Kwa kuwa Nyerere na Karume,
wote waliamini jambo moja kuwa kuungana ni kuongeza nguvu, hivyo waliweza
kuzungumza kwa urahisi zaidi kwa kuwa waliona walikuwa na sera zinazofanana.
Hivyo suala la muungano
halikuwa na ugumu na ikawa pia lahisi kwa Tanu na ASP kuungana na kutengeneza
Chama cha Mapinduzi (CCM).
SOURCE: CHAMPIONI








0 COMMENTS:
Post a Comment