SOKA lina historia ndefu sana, kwa hapa
Tanzania ni nadra kukuta mtu anaingia hivihivi katika ngazi ya utawala pasipo
kupitia uchezaji. Ni wachache sana, hususan kwa timu kubwa za Yanga na Simba.
Viongozi waliopo wengi, wao wana historia kubwa katika klabu zao.
Na mmojawapo ni Ibrahim Akilimali, maarufu
kama mzee Abramovich, ambaye anasema kama ingekuwa inawezekana hata kupitia
maombi, basi angekesha akimuomba Mwenyezi Mungu damu yake aifanye iwe ya
kijani. Ni shabiki, mwanachama na mnazi wa kutupwa wa Klabu ya Yanga.
Jina la Abramovich amepewa kupitia lile la
bilionea wa Kirusi, Roman Abramovich anayeimiliki Chelsea. Akilimali si tajiri,
lakini moyo wake ni wa utajiri kwa klabu yake ya Yanga na hasa mapenzi makubwa
aliyonayo.
Abramovich, hakuwahi kucheza soka maishani
mwake, pengine wengi wangejiuliza, aliingiaje kwenye himaya ya Yanga mpaka
anakuwa mmoja wa viongozi wenye umaarufu klabuni hapo, akiwa kama Katibu Mkuu
wa Baraza la Wazee wa Klabu ya Yanga?
Ana historia ndefu katika maisha ya soka hadi
kufikia leo hii kutambulika kama Abramovich anayefahamika kwenye vyombo vya habari
kutokana na umaarufu wake wa kuisifia Yanga. Katika mahojiano maalum na
Championi Jumatatu, ameeleza mengi likiwemo suala la tambiko kwa timu kabla ya
kucheza mechi.
Historia yake katika soka:
“Jina langu kamili, naitwa Ibrahim Omary
Akilimali, mzaliwa wa Kigoma. Historia yangu katika suala zima la soka, mimi ni
mmoja wa wapenzi na wanachama wa mwanzo kabisa wa Klabu ya Young African Sports
Club, tangu mwaka 1956. Kuna sababu kuu mbili zilizonifanya niipende Yanga
yapata miaka 58 sasa.
“Mosi, ni neno ‘Afrika’. Tangu zamani mimi
nilipenda kudumisha na kuutukuza Uafrika wangu, kipindi hicho nilikuwa mfuasi
na mwanachama wa Chama cha Tanu (Tanganyika African National Union), ambacho
baadaye kiliipatia Tanganyika uhuru wake mwaka 1961.
“Niliingia katika chama cha Tanu mwaka 1955,
mwaka mmoja baada ya kuundwa kwa chama hicho. Hivyo kukawa na thamani na
kulikuza neno Afrika. Wakati nikiwa bado Kigoma, nilikuwa nikisikia kuna timu
inaitwa Young African Sports Club, kwa hiyo nikawa nimependezewa sana na neno
African, nikaona ilikuwa ni sehemu muhimu ya kuukuzia Uafrika wangu, ukawa ni
mwanzo wa kuipenda Yanga.
“Sababu ya pili, baba yangu alikuwa ni mfuasi
mkubwa wa neno Afrika pia akiwa ni mpenzi mkubwa wa Klabu ya Yanga, kwa hiyo na
mimi nilirithi mapenzi. Hizo ndizo sababu za mimi kuwa Yanga damu mpaka sasa.
Aliingiaje Yanga?
“Mpaka mwaka 1962, nilikuwa mpenzi tu, hata
kabla ya kuja Dar es Salaam. Nimekuja hapa Dar mwaka 1966 na kupata kazi
bandarini mwaka 1967 kama Kuli. Zamani viongozi na wamiliki wa bandari walikuwa
ni wanachama wa Yanga, hata wachezaji ambao hawakuwa na kazi basi
waliunganishwa kufanya kazi bandarini. Mwaka 1972 nilipata kadi yangu ya
uanachama wa Yanga hadi leo hii. Miaka 42.”
Milima na mabonde aliyopitia:
“Nimepitia mengi, migogoro ya hapa na pale ya
klabu yangu. Kwanza kabisa zamani klabu hazikuendeshwa kwa sheria za TFF,
ziliendeshwa na wazee (kwa Yanga kulikuwa na Baraza Tochi), kwa hiyo kulikuwa
na changamoto kadha wa kadha…mara huyu kiongozi kung’ang’ania madarakani, ooh..
wanachama waukatae uongozi fulani, watu walipigana hovyo.
“Lakini mimi nilikuwa mfuasi wa kufuatilia
chanzo cha mgogoro na kuhakikisha tunapata suluhu. Tumekwenda hivyo na migogoro
kama hiyo ndiyo ilipelekea kuundwa kwa timu ya Pan Africa. Haikuundwa hivihivi,
bali lilikuwa ni zao la migogoro ndani ya Yanga enzi za utawala wa mzee Tabu
Mangara, hadi Mkuu wa Wilaya ya Ilala wakati huo, Kunambi akaingilia kati
lakini mwisho wa siku tukamuangusha.
“Watu wake wa karibu wakamshauri kwamba hawezi
kutoka hivihivi Yanga, ndipo wakajiunga na timu ya Jogoo huko Morogoro na
baadaye kuunda timu iliyoitwa Pan African. Na wachezaji wote wa Yanga kama
Sunday Manara, Kitwana Manara wote wakajiunga na timu hiyo.”
Historia ya Baraza la Wazee Yanga:
“Wakati naingia kama mwanachama wa Yanga 1972,
kulikuwa na Baraza la Wazee lililoitwa Baraza la Tochi. Kazi yake kubwa ilikuwa
ni kumulika na kuchunguza maadui wa Yanga. Wajumbe wa baraza hili walikuwa ni
watu wazima, wazee na wasiri sana, ambao walihusika na kutoa taarifa sahihi kwa
uongozi kuhusu wabaya na wahujumu wa klabu yao.
“Baadaye neno tochi likafifia, likabakia jina
Baraza la Wazee. Wajumbe wa baraza hili ni lazima wawe wazee na hawa ndiyo
wenye kuijua Yanga na miiko yake, ndiyo maana lipo mpaka sasa. Kutokana na kazi
yake, kwani wazee ndiyo wanaijua Yanga kwa undani zaidi.”
Aigawa Yanga
Kutokana na migogoro, mwaka hadi mwaka,
Abramovich ambaye kwa sasa ni katibu wa Baraza la Wazee, anasema alikuwa kiongozi
katika kuikataa Yanga kufanywa mali ya kampuni, enzi za utawala wa Jabir
Katundu.
“Alikuwa na siasa nzuri za kimaendeleo, lakini
kutokana na upeo wetu mdogo sisi tulikataa timu yetu kuwa mali ya kampuni,
mvutano ukatokea mpaka tukaamua kuunda Yanga Asili, nikishirikiana na Salum
Mwaipande.
“Tuliushitaki uongozi uliokuwa madarakani
(Jabir Katundu na katibu wake George Mpondela) kwa sababu hatuhitaji Yanga
ifanywe kampuni. Migogoro ya namna hiyo imekwenda mpaka 2006, tulipompata Yusuf
Manji aliyetupatanisha na kuitoa Yanga Asili mpaka Yanga tunayoiona leo hii.
“Hatukujua faida yake, baadaye nilikuwa wa
kwanza kutia saini wakati Yanga inafanywa kampuni wakati wa utawala wa Abbas
Tarimba na Francis Kifukwe.”
Hee..! kumbe Fat ni zao la Yanga!
“Anasema Yanga ilikuwa zao la kuundwa kwa
Chama cha Soka Tanzania (Fat, sasa TFF) ingawa hakutaka kulizungumzia kwa kina.
“Kwa kifupi, ni kwamba Yanga ndiyo ilikuwa timu ya kwanza kuileta Gor Mahia (ya
Kenya) hapa nchini, ilikuwa na wanachama na wapenzi wa Yanga, hivyo walikuja
hapa kucheza mchezo mmoja, katika mapenzi hayo, ndiko kukaanzishwa kwa vyama
vya soka kama Fat.”
Halipwi hata senti Yanga:
Akieleza mafanikio yake ya kuwa mwanachama na
mwanaharakati wa maendeleo ya Yanga, Abramovich, anasema halipwi chochote, bali
mafanikio yake siku zote ni furaha ya ushindi, basi. “Mafanikio yangu kwa Yanga
ni furaha tu basi, siyo kingine. Kwa mfano, tunapomfunga mtani wetu Simba, basi
ninafurahi sana. Lakini siyo kusema kutokana na kuipenda kwa miaka yote hiyo na
kuwa karibu nayo kiasi hicho, labda kuna mshahara napewa. Silipwi hata senti
tano.”
Aomba Mungu ampe damu ya kijani
“Kiukweli kama ingekuwa inawezekana kwa
Mwenyezi Mungu, ningemuomba anibadilishie damu yangu kutoka nyekundu, aifanye
ya kijani au ya njano.”
“Hii inatokana na mapenzi yangu kwa Yanga
ambayo inatumia rangi za kijani, njano na nyeusi. Rangi nyekundu ni Simba.”
Kutana na Kamati ya Miziziology
Ni kama jambo la kushtua lakini huo ndiyo
ukweli, kwamba Yanga haiwezi kuanza ligi bila kufanyiwa tambiko. Mzee Abramovic
amefunguka mkanda mzima.
“Yanga kuna kamati mbili. Kamati Kuu ya
Utendaji na Kamati Kuu ya Utendaji ya Miziziology. Kamati hii huendeshwa na
wazee na huteuliwa na mwenyekiti wa kamati ya utendaji ambaye anamteua mzee
mmoja kuwa kiongozi wao.
“Kazi yake kuu ni kutunza tamaduni na miiko ya
klabu, pamoja na kufanya tambiko kwa timu kabla ya kuingia kwenye ligi, kusoma
dua kwa marehemu wazee wote walioanza kuiongoza Yanga pamoja na kufukiza ubani.
Pia hujishughulisha katika kuimarisha urafiki kati ya Yanga na timu nyingine,
maana wao ndiyo wana kumbukumbu, historia ya klabu yetu.”
Maana ya Miziziology:
“Wewe hujawasikia waganga? Hujawahi kuona timu
inakwenda uwanjani na kuku au paka au pengine mnyama anapita katikati ya uwanja
wakati mchezo unaendelea? Miziziology ni utamaduni wetu ambao tumeuzoea wa
kufukiza ubani, hata Ulaya na Kombe la Dunia vitu hivi tuliviona. Kwa kifupi
Miziziology ni utukuzaji na utoaji wa baraka za kimila kwa timu.”
Tukio ambalo hawezi kulisahau
“Sitasahau siku ambayo nilituhumiwa kuwa
nilikuwa naisemea timu, mwenyekiti Manji alipowauliza wanachama wanichukulie
hatua gani na wanachama wakamtaka anifukuze uanachama. Kiukweli niliumia kupita
maelezo kusikia kauli ile. Yaani na miaka yangu yote tangu niipende Yanga na
jinsi nilivyoipigania mpaka leo hii, nilihuzunishwa sana na kauli ya wanachama
wenzangu. Lakini namshukuru Mungu yote yalikwisha, lakini mpaka nafukiwa chini,
sitasahau kauli za watu wale.
“Nashukuru sana kwa kuwa Manji alilikataa ombi
lile na kuonyesha kunidhamini, pamoja na kuumia, mimi ni mtu mzima, naendelea
kuipenda Yanga na pia naweza kusamehe ingawa maumivu yaliumaliza moyo wangu.”
Ishu ya ‘logo’ nyekundu
“Ni kweli sisi baraza tulishinikiza kukataa
logo nyekundu (ya wadhamini wa Ligi Kuu Bara, Vodacom). Tangu zamani tangu
Yanga ianzishwe 1935, piga ua, rangi nyekundu haiwezi kukanyaga Yanga. Na Simba
hivyohivyo, piga ua haiwezi kuvaa rangi ya kijani au njano.
Maamuzi yoyote ya kamati ya utendaji lazima yapite
kwa wazee.
Anasema maamuzi yoyote yale ambayo kamati kuu
ya utendaji itafikia kabla ya kutekelezeka, ni lazima yapite kwa baraza la
wazee na kuomba ushauri. Kama baraza litaona jambo hilo ni baya, tunawashauri
na kutoa tathmini ya ubaya wa kitu hicho au kuketi chini na kamati kuu na
kufikia maridhiano pande zote.”
Akunwa na Manji, Katundu
Amefanya kazi na viongozi mbalimbali lakini
anasema uongozi wa Jabir Mohammed Katundu na uliopo madarakani kwa sasa chini
ya Yusuf Mehbub Manji hauna kifani.
“Siwezi kusahau kazi ya Katundu miaka ya 1970.
Uongozi ambao ulijenga jengo la makao makuu ya klabu (Mtaa wa Twiga na
Jangwani). Alikuwa jasiri na mpenda maendeleo ya Yanga, alijitosa mbele ya Rais
Karume na kumuomba fedha kisha akaijengea Yanga makazi ambayo mpaka sasa
wanatumia. Pili, ndiye aliyejenga Uwanja wa Kaunda, ambao mpaka sasa umeshindwa
kuendelezwa na viongozi wanaoingia madarakani.
“Manji kila mtu anaona juhudi zake na pengine
unaweza kuwa uongozi bora kuliko wote kutokana na juhudi zake ambazo amekuwa
akionyesha, akitaka timu iwe ngazi za kimataifa.”
Manji ampa jukumu jingine
Kutokana na harakati zake za kuiendeleza
Yanga, Abramovich anasema jukumu kuu ambalo amekabidhiwa rasmi ni kutoa hamasa
kwa wanachama kuelekea mchezo husika na kwa sasa kuna jukumu jingine amepatiwa
lakini ni mapema sana kulitaja.
Duh…! Wajukuu 32
Mzee Akilimali ni babu wa wajukuu 32 katika
watoto wake wanne aliobahatika kupata. Watatu wa kiume na mmoja wa kike aliowazaa
na wake zake watatu lakini kwa sasa ana wake wawili.









0 COMMENTS:
Post a Comment