Na Saleh Ally
MIAKA kumi iliyopita, msanii aliyekuwa anatamba
sana, anayefanya shoo au kusafiri Marekani na barani Ulaya alikuwa ni Joseph
Mbilinyi, wakati huo akijulikana kama 2 Proud kabla ya kuamua kubadili jina na
kuwa Mr II.
Ukiachana na wale ‘watoto wa mama’ kutoka
maeneo ya ‘uzunguni’, Mr II alikuwa kati ya vijana wa kwetu uswahilini
waliokuwa wanavaa raba mtoni, cheni kali kama Public Enemy, miwani kama ya Jay
Z, pozi utadhani Notorious BIG, kitambaa kama kile cha 2 Pac Shakur, lazima
ungefurahi kukutana naye.
Hata iwe vipi, hakutakuwa na njia ya kukwepa
mchango mkubwa wa Mr II katika muziki wa kizazi kipya hasa kutokea kipindi
kigumu cha mapinduzi hadi ulipo sasa. Vipi alionekana hafai, kuna mambo mengi
sana pamoja na hali halisi.
Hakuna anayeweza kubisha kwamba wako
waliochukizwa na mafanikio ya Mr II ambaye sasa anajulikana kama Sugu. Pia
hakuna ubishi, kuna ‘wakubwa’ ambao hawakutaka aendelee kutamba kutokana na
kuwa na nguvu kubwa ambayo iliwasumbua na kusaidia kuwaamsha wengine.
Kwa jumla iko hivi, Sugu aliporomoka kutokana
na vitu vitatu vikuu. Kwanza muda wenyewe, wakati wa wengine kuchukua nafasi
uliwadia, pili; ‘wakubwa’ hawakutaka aendelee kutamba na kuwa na nguvu kubwa
iliyowasumbua, tatu; roho mbaya, maana wapo ambao hawamkupenda tu, ukiwauliza
kwa nini wanamchukua, jibu lao ni “basi tu!”
Msanii mwingine wa kizazi kipya ambaye ikifikia
siku ameshuka kisanii, basi tutasema alikuwa na mchango na hatuwezi kuukwepa ni
Nasib Abdul ‘Diamond’. Amefanya kazi nzuri, amepiga shoo nyingi Ulaya na
Marekani, amekuwa gumzo barani Afrika.
Ajabu wikiendi iliyopita kwenye tamasha la
Fiesta, alizomewa sana hadi kufikia kuahirisha shoo huku mwenyewe akilalama
kuwa kuna jambo au mpango wa kummaliza.
Siwezi kuchangia kwenye hilo kwa kuwa si rahisi
kung’amua, lakini haja ya yeye kujiuliza kwamba vipi watu wa Temeke, Ilala,
Kinondoni na mikoa jirani wamzomee kwa pamoja!
Kabla ya kuingia ndani kwenye kuchangia unaweza
kusema Diamond mchango wake hautakwisha pia kama ilivyo kwa Sugu kwa kuwa yako yale
makubwa ameyafanya.
Utaendelea kukumbukwa ingawa kwa sasa tunapaswa
kujiuliza, msanii huyo anaweza kukwepa sababu tatu zilizomporomosha Sugu
ukijumlisha moja ambayo Sugu hakuwa nayo, lakini Diamond inamsumbua?
Muda:
Hakuna ujanja, ukifikia wakati Diamond atashuka
tu kwa kuwa kwa tabia ya kila binadamu, hufikia wakati anahitaji kusikiliza
vitu vipya na si vile vya zamani ambavyo huonekana ni ‘vya kila siku’.
Wakubwa:
Hawa ni tatizo kwa kila msanii, walimshusha
Sugu kwa nguvu, wakampandisha Profesa Jay, naye wakamshusha na kumpandisha
mwingine wakitumia nguvu yao lakini lengo hasa linakuwa ni maslahi yao na si ya
sanaa au wasanii wenyewe.
Kitu kibaya wakati msanii mmoja anashushwa,
anayepandishwa huchekelea kwa kipindi hicho akiwa amesahau msemo wa ‘mwenzako
akinyolewa.’
Chuki:
Nani anakataa kuwa sisi binadamu tumeumbwa na
husda, hatupendani na wachache wanaobaki kuwa watu wazuri hujizuia na kupambana
na tabia hiyo. Wako wasiompenda Diamond kutokana na mafanikio yake, bila sababu
za msingi.
Wanaomchukia hawajui kwa sababu gani na
inawezekana katika wanaomchukia ni kwa kuwa msichana au mpenzi wake ameonyesha
kuvutiwa sana na msanii huyo. Basi bifu upepo, linaanzia hapo na linakuwa kubwa
utafikiri la watu waliowahi kupigana, kumbe hawajawahi kukutana hata siku moja.
Tandale:
Hii ndiyo hoja ya nne ambayo ninaamini
inachangia kwa kiasi kikubwa kumtafuna Diamond. Kumfananisha na Sugu, haina
maana wanafanana kwa kuwa hata muziki wanaopiga haulingani kwa asilimia mia.
Nimetengeneza mfano unaokumbusha zamani na
sasa, pia wale waliotamba hadi nje ya Tanzania na kufikia kujulikana Ulaya na
Marekani hata kama ni kwa Waafrika tu. Lakini utaona kwa Sugu, sikuzungumzia
suala la Tandale ambako alikulia Diamond.
Sugu alikuwa akirudi Mbeya, aliimba na kuusifia
mkoa huo, alionyesha mapenzi kwa watu wa eneo alilozaliwa na kukulia, aliisifia
Mtwara aliyosoma shule hata kama alifeli, leo ni Mbunge wa Mbeya, huu ni mfano,
aliwajali, nao wakamjali.
Tunajua ni mwenyeji wa Kigoma, lakini maisha
yake wakati akifanya biashara ya kuuza mitumba, ndiyo sehemu ambayo ina watu
wake, utaona hata alipoimba wimbo wa ‘Mbagala’, ilikuwa rahisi kwake kutoka na
kupata sapoti kubwa.
Mafanikio yake yamemfanya abadilike, aishi
Kimarekani, asahau watu wake hali inayojenga hisia za kudharau alikotoka au
kutowajali watu wake ambao walikua naye. Siku zote mbwembwe sana hujengwa na
msingi wa kiburi, kitu ambacho watu wengi hawapendi.
Kila mtu anapenda kuheshimiwa, kupendwa na
kupewa kipaumbele. Diamond amejisahau kwa watu wake na huu ndiyo wakati wa
kurudi Tandale na ikiwezekana Buzebazeba kule Kigoma na kuonyesha yeye kweli ni
mtu wa watu.
Bila mashabiki hakuna Diamond, kuna kila sababu
ya kuwaonyesha watu unawajali, unawathamini kwa kuwa ubora wa kazi zake
umesukumwa kwenye mafanikio na watu hao na kufanya hivyo ni kuonyesha
anawajali.
Huenda angeweza kutoa gari kwa Wema Sepetu au
yeye kuzawadiwa kwenye siku yake ya kuzaliwa, lakini hakuna ambaye
angeshangazwa au kutofurahia kama watu waliwahi kusikia alitoa gari la wagonjwa
au alichangia kwa kununua gari la wagonjwa katika Hospitali ya Tandale, eneo
moja la Mbagala, kokote jijini Dar es Salaam, kwao Kigoma au sehemu yoyote ile
ya Tanzania.
Jamii ndiyo inayofanya uingize au kutengeneza,
kuijali ni lazima na hili Diamond anaweza kujifunza kupitia gazeti hili la
Championi ambalo kila wiki linaendelea kutoa zawadi za jezi, mipira, runinga,
simu kwa wasomaji wake kuonyesha linawajali na kuthamini mchango wao, hakuna
gazeti jingine linafanya hivyo, labda lianze wiki ijayo.
Kuishi Kimarekani sana si jambo baya, lakini
kuishi Kitanzania ndiyo sahihi zaidi kwa kuwa hapa ni Tanzania. Inawezekana kwa
Diamond linaweza kuwa jambo gumu lakini jamii iliyompa umaarufu, fedha na
ukubwa alionao ni ya wa Tanzania, hivyo lazima awajali Watanzania na Tandale
ingeweza kuwa ya kwanza, kwingine kukafuatia.
Katika muda ambao Saleh umeutumia vizuri na mola wako atakulipa ni wakati wa kuandika waraka huu kwa Diamond na wasanii wengine kwa ujumla!
ReplyDelete