Kiungo mchezeshaji wa Yanga Myarwanda, Haruna Niyonzima, ameamua kuvunja ukimya na kusema anasumbuliwa au hajaukamata vizuri mfumo wa kocha mpya, Marcio Maximo.
Niyonzima alishindwa kuonyesha kiwango cha juu katika mechi iliyopita, Yanga ilipowavaa watani wake Simba.
Niyonzima raia wa Rwanda amesema kuwa mfumo wa uchezaji anaoutumia kocha wake ndiyo
umesababisha yeye acheze chini ya kiwango na siyo kitu kingine.
Niyonzima alisema, mfumo
anaoutumia kocha wake huyo wa kufanya mashambulizi ya kushtukiza ‘Counter
Attack’ yeye hauwezi tofauti na wachezaji wenzake.
Myarwanda huyo alisema,
yeye hawezi kucheza mfumo huo, mwenyewe amezoea soka la pasi, akiamini ndiyo
linalomfanya aonekane bora katika mechi zao za Ligi Kuu Bara na mashindano
mengine.
“Mashabiki ujue walikuwa
hawajanigundua, mimi kucheza chini ya kiwango siyo kwenye mechi dhidi ya Simba,
mechi nyingi nimekuwa sionekani kutokana na mfumo anaoutumia kocha wetu.
“Kocha anataka tucheze
mipira mirefu ya kushambulia kwa kushtukiza kwenye lango la timu pinzani, ambao
kwangu ni mgumu, kiukweli siuwezi kabisa, mimi ninataka tucheze mpira wa pasi
nyingi.
“Ninaamini tukiendelea
kuutumia mfumo huo, basi nitaonekana kiwango kushuka kadiri ya siku
zitakavyokwenda, ili nionekane bora tucheze soka la pasi lakini hivi
nitapotea,”alisema Niyonzima ambaye amekuwa akianza michezo yote ya Yanga msimu
huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment