Na Saleh Ally
PRESHA kubwa kwa klabu
kongwe nchini za Yanga na Simba katika kipindi hiki ni suala la ushindi na
uchezaji wao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kila upande unazungumzia
suala la ushindi na pia uchezaji wa vikosi vyao. Yanga na Simba ziko kwenye
presha kubwa ya kutaka kushinda mechi zinazofuata baada ya kuanza vibaya msimu
mpya wa 2014-15.
Simba ilianza kwa sare
katika mechi zake zote, haijapoteza hata mechi moja. Yanga ikaanza na kipigo
cha mabao 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar, ikicheza ugenini mjini Morogoro.
Matumaini makubwa ya
mashabiki yalihamia kwenye mechi zinazofuatia, Yanga dhidi ya Prisons ya Mbeya na
Simba wakipambana na Polisi Moro ambayo imerejea Ligi Kuu Bara.
Simba wakaambulia sare
nyingine ya bao 1-1 ambayo imewachukiza zaidi mashabiki wao huku Yanga
wakishinda lakini bado mashabiki wao hawakufurahia ushindi huo wa mabao 2-1,
kwa kuwa timu haikucheza vizuri.
Yanga haikucheza vizuri
katika kipindi cha pili na kuipa nafasi Prisons kutawala na kuwahenyesha
vilivyo. Hivyo bado imani ya mashabiki wa Yanga haijakamilika katika kikosi
chao.
Hata iwe vipi, hauwezi
kusema wachezaji wote wa Yanga au Simba wanacheza katika kiwango cha chini.
Mmoja wao ni Haruna Niyonzima, raia wa Rwanda.
Wakati Yanga ikiwa chini ya
Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji, ndiye alikuwa injini ya Yanga na alipata nafasi
kubwa ya kucheza timu na kuiwezesha kubeba ubingwa wa Kombe la Kagame.
Alipoondoka Mbelgiji huyo,
Ernie Brandts, kutoka Uholanzi akachukua gurudumu na kwake ilikuwa rahisi zaidi
kumpa nafasi Niyonzima kwa kuwa kabla alifanya naye kazi APR na wakafanikiwa.
Akampa nafasi, akaisaidia
Yanga kubeba ubingwa. Akaondoka na Mholanzi mwingine, Hans van der Pluijm,
akachukua nafasi ya kuinoa Yanga, mambo hayakuwa mazuri kwa Mnyarwanda huyo.
Akaanza kukalia benchi,
huku mashabiki wengi wa Yanga wakilalama kwamba uchezaji wake haukuwa mzuri na
anaremba sana! Uchezaji wake ni uleule siku zote.
Akiwa Yanga, kipindi kigumu
kwa Niyonzima kilikuwa ni kile timu ikiwa chini ya Pluijm. Sasa ameichukua
Mbrazil, Marcio Maximo, amempa nafasi na kubadili aina uchezaji, sasa anamtumia
kama free roll.
Mchezaji anayekuwa huru
kuzunguka uwanja mzima kama anavyofanya Jose Mourinho na Oscar au Barcelona na
Lionel Messi katika kipindi hiki, ndiyo maana utamuona anatoa pasi nyingi zaidi
za mabao kuliko kufunga.
Kama Yanga inafanya vibaya,
basi wana nafasi ya kujirekebisha. Lakini kama kuna mchezaji ameonekana
kutekeleza vilivyo majukumu yake kwa asilimia kubwa ni Niyonzima na amekuwa
akitoa pasi nyingi zaidi na kukaba sana.
Mabadiliko makubwa ni namna
alivyoingia ndani wa mfumo wa Maximo ambao hauna tofauti kubwa sana na ule wa
Saintfiet. Ndiye anayechukua mipira yote kuanzisha mashambulizi.
Ukiangalia katika uchezaji
wa Yanga chini ya Maximo, utaona Niyonzima ndiye anayekwenda nyuma kuchukua
mpira kwa mabeki wa kati Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ au Kelvin Yondani ‘Cotton’. Halafu anaupeleka sehemu moja
hadi nyingi naye akikimbia kuunga mkono.
Kwenye kundi la wachezaji
waliopiga pasi nyingi, hawezi kuwa nje ya tatu bora. Ukisema waliopiga krosi
nyingi, hautamkosa lakini hata utengenezaji wa nafasi, huenda anaongoza.
Maximo anamchukua kama ‘playmaker’,
yeye ndiye anaanzisha mfumo wa mashambulizi kwa kupema mipira mingi zaidi.
Lakini ndiye anatangulia mbele haraka kumalizia mashambulizi, ndiyo maana ana
pasi nyingi anaopiga langoni mwa timu pinzani kama alivyofanya kwenye mechi ya
Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC huku akimpoteza kabisa Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Kingine ambacho unaweza kugundua
kwa Myarwanda huyo, huenda kuwekwa benchi na Pluijm, kulifanya ajitazame upya.
Kweli ameongeza kasi, hakai na mpira muda mwingi kama ilivyokuwa mwanzo.
Mpira ni wa ajabu sana, si
rahisi kusikia mashabiki wa Yanga wakimzungumzia Niyonzima namna anavyojituma
na kutimiza majukumu yake kiufasaha kwa sasa au kuhamasisha wengine kufanya
vema zaidi.
Niyonzima sasa anacheza
katika kiwango kizuri na cha juu na kama akiendelea hivyo mfululizo, basi
atakuwa msaada mkubwa kwa Yanga na kumpunguzia majukumu mengi Maximo na hasa
kwenye suala la kurekebisha makosa.
Hawezi kucheza kwa kiwango
cha aina moja katika mechi zote za ligi, huenda kuna siku kitashuka au kupanda
zaidi. Ajabu hakuna anayemuona na wengi wanasubiri siku atakayokosea au ‘kuharibu’
ili waanze kulalama. Watu wa mpira bana!
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment