Katika hali isiyo ya kawaida, mashabiki wa
Yanga walivaana na kushambuliana wenyewe kwa wenyewe, kisa kikiwa ni kuwasema
vibaya wachezaji wawili wa timu hiyo, Mnyarwanda Haruna Niyonzima na Mbrazili
Andrey Coutinho.
Hiyo ilijiri juzi kwenye majukwaa ya Uwanja wa
Taifa jijini Dar, Yanga ilipokuwa inaumana na Simba na kutoka suluhu.
Sekeseke hilo lilianza
kuunguruma baada ya shabiki mmoja wa timu hiyo kutoa kauli kuwa Niyonzima na
Coutinho wanapenda mpira wa shoo na wanaigharimu timu, hivyo ni bora watolewe.
Kauli hiyo ilionekana kuwachefua mashabiki
wengine waliokuwepo jukwaani hapo ambapo ghafla walimvaa kwa kumtupia maneno
makali na kumtaka afute kauli yake hiyo mara moja la sivyo aondoke kwenye
jukwaa, kitu ambacho shabiki huyo alikipinga.
Kutokana na mgomo huo, jukwaani hapo paliibuka
mzozo mkubwa mpaka baadhi ya mashabiki wengine waliokuwa jirani na jukwaa hilo,
walipoingilia na kuwaweka sawa mashabiki hao wakiwasihi kuwa wote ni kitu
kimoja na haina haja ya kugombana.
Katika hatua nyingine, mashabiki wengine pia
walisikika wakitupiana matusi baada ya shabiki mmoja kuropoka kuwa Mrisho
Ngassa hakustahili kuanza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo siku hiyo bila
ya kutoa sababu maalum.
Zogo ambalo lilizimwa baada ya mmoja wa
mashabiki hao waliokuwa wakitukanana, kurudi chini na kuwa mpole.
0 COMMENTS:
Post a Comment