DK NDUMBARO AKIWA MAKAO MAKUU YA FIFA. |
Siku moja baada ya Rais wa
TFF, Jamal Malinzi kusisitiza lazima klabu zikatwe asilimia 5 kwenye fedha zao
za udhamini wa Vodacom na Azam TV, zenyewe zimejibu mapigo.
Kupitia mwanasheria wao,
klabu 14 za Ligi Kuu Bara, zimesisitiza mambo haya ya msingi, kuwa hazitavaa
jezi zenye nembo ya wadhamini hao, kupinga kukatwa fedha zao.
Pili, zitaitisha mkutano wa
dharura wa kamati ya utendaji kupiga kura ya kutokuwa na imani na Malinzi
ambayo itamuondoa madarakani.
Mwanasheria maarufu nchini
Dk Damas Daniel Ndumbaro amesema kwa mujibu wa katiba ya TFF, klabu hizo 14
ambazo ni mwanachama zinaruhusiwa kufanya hivyo.
“Hilo linaruhusiwa kwa
mujibu wa ibara ya 25 (ibara ndogo ya TFF) kama wanachama tuitishe mkutano mkuu
maalum.
“Katika mkutano huo
tutapiga kura za kutokuwa na imani na Malinzi, kinachotakiwa ni kufikia
theluthi mbili tu, yaani kura mia moja,” alisema Ndumbaro.
TFF ina wanachama 150,
hivyo kama utaitishwa na kufikisha theluthi hizo mbili za kura ya kutokuwa na
imani, Malinzi atakuwa ameng’oka madarakani.
Uamuzi wa klabu hizo
kupinga umetokana na kwamba TFF kupitia sekretarieti yake iliyodai ni kwa
mujibu wa kamati ya utendaji, imepitisha uamuzi wa kutaka ipewe asilimia 5 ya
fedha za udhamini za klabu.
Jambo hilo halijafanyika
sehemu yoyote duniani, pia kumekuwa hakuna ufafanuzi mzuri wa kutosha zaidi ya
Malinzi kusisitiza kuwa ni lazima fedha hizo zikatwe.
Kiutaratibu inaonyesha
klabu ndiyo zinazotangaza wadhamini hao, ndiyo zenye haki ya fedha hizo.
Lakini katika mapato ya
milangoni, fedha zimekuwa zikikatwa fedha ambazo zinakwenda kwenye mfuko wa
maendeleo ya soka nchini ambao sasa TFF unataka ukate na fedha za wadhamini.
Mbeya City na Mtibwa Sugar,
zimetishia kuifikisha TFF mahakamani kama itaendelea kulazimisha uamuzi huo.
0 COMMENTS:
Post a Comment