Katika mikakati ya kuvaana na watani wao
Simba, Kocha Mkuu wa Yanga, Mbrazili, Marcio Maximo, amembadilishia namba
kiungo wake mshambuliaji Mrwanda, Haruna Niyonzima na Mbrazili, Andrey
Coutinho.
Hiyo yote ni kuhakikisha timu yake inapata
ushindi katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa leo Jumamosi kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Timu hizo zote mbili zitashuka uwanjani
kupambana huku kila moja ikiwa na kocha mpya. Yanga inanolewa na Mbrazili,
Maximo huku Simba ikiwa chini ya Mzambia, Patrick Phiri.
Kocha huyo, mara kwa mara amekuwa
akiwabadilisha namba wachezaji wake kutokana na aina ya timu atakayokutana nayo
katika mechi husika, hivi karibuni Maximo aliwahi kutamka kwamba hataki
mchezaji anayecheza nafasi moja ndani ya uwanja, hivyo anamuandaa kila mmoja
ili acheze nafasi nyingi uwanjani.
Awali, Niyonzima alikuwa akichezeshwa namba 11
kabla ya mazoezi ya wiki hii ya maandalizi ya mechi dhidi ya Simba kuhamishwa
na kuandaliwa kuchezeshwa 10 iliyokuwa inachezwa na Coutinho.
Coutinho yeye amehamishiwa kucheza namba 11
kwa ajili ya kupiga krosi safi zitakazomfikia mshambuliaji Mbrazili, Geilson
Santos Santana ‘Jaja’ mwenye uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya vichwa.
Katika mazoezi ya siku hizi tatu za kujiandaa
na pambano hilo, kocha huyo alionekana kuwachezesha viungo hao nafasi hizo,
tofauti na ilivyokuwa mechi zilizopita za ligi kuu.
Wakati mazoezi hayo yanaendelea kwenye Uwanja
wa Boko Veterani huko Ununio jijini Dar es Salaam, kocha huyo alionekana
akiwapa maelekezo viungo hao jinsi ya kulishambulia goli la wapinzani wao.
Kocha huyo, katika mazoezi yaliyofanyika
Alhamisi jioni, alionekana akiwapa maelekezo na mbinu mbalimbali Niyonzima,
Coutinho na Mrisho Ngassa jinsi ya kupiga krosi, kona na faulo safi
zitakazofika kwa Jaja mwenye umbile kubwa.
Wakiendelea na mazoezi hayo, Maximo alisikika
akiwataka wachezaji kupiga pasi za haraka huku wakicheza mipira mirefu kwa
kutumia mfumo wa kushambulia kwa kushtukiza ‘Counter Attack’ akiwatumia viungo,
Hassani Dilunga na Mbuyu Twite.
“Niyonzima, Coutinho chezeni pasi za harakaharaka
katika kushambulia na siyo kukaa na mpira muda mrefu ili msipoozeshe mpira, pia
nataka mcheze mipira mirefu mara baada ya kupigiana pasi,” alisikika Maximo kwa
sauti kubwa uwanjani hapo.
0 COMMENTS:
Post a Comment