October 25, 2014

WAZIRI NKAMIA AKIWA OFISINI KWAKE...

Na Saleh Ally
SERIKALI imeamua kuvunja ukimya kuhusiana na suala la kuwaandaa vijana ambao watakuwa nyota wa taifa hapo baadaye.

Naibu Waziri wa Habari, Vijana na Utamaduni, Juma Nkamia amesema litakuwa ni jambo la msingi kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litaangalia wakati huu kuwa mwafaka wa kuwapa nafasi vijana.
Nkamia amesema vijana wanapoandaliwa kwa muda wa kutosha ni vizuri kwenda mbali wakiwa imara kwa kuwa msingi wao ni bora.
AKIWA OFISINI KWAKE....

Vijana:
Katika mahojiano maalum na Championi Jumamosi, ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Nkamia amesema wakati wa michuano itakayofanyika Novemba nchini Ethiopia litakuwa ni jambo zuri kikosi kitakachoundwa kwa timu ya Tanzania Bara kutoa nafasi kwa vijana wengi.
“Vijana kawaida wanakuwa tegemeo la baadaye, lakini utaratibu ni lazima waandaliwe. Pamoja na mazoezi, vijana wanatakiwa kupewa kitu kigumu kwao. Michuano ya Chalenji itakuwa ni sehemu sahihi.
“TFF ikae na kuzungumza na mwalimu wa timu ya taifa, imueleze kwamba wanataka kuandaa vijana na wakongwe kama akina Kelvin Yondani, Amri Kiemba na wenzao wapunguzwe kidogo.
BAADA YA MAHOJIANO NA SALEH ALLY...

“Sisemi wote watoke, lakini nafasi ya vijana iwe kubwa kwa kuwa wachezaji hao ndiyo wanaondoka hivyo. Sasa ni vizuri kuwapa nafasi vijana ili kuwa na timu imara hapo baadaye,” anasema Nkamia na kusisitiza.
“Tunaweza kufurahia sasa kushinda mechi za kirafiki na kupata nafasi nzuri kwenye viwango vya Fifa, lakini haina faida kubwa kama vijana wakiandaliwa, Tanzania ikawa na timu bora na imara halafu ikaweza kufuzu kucheza Kombe la Mataifa hapo baadaye.”
DK NDUMBARO

Dk Ndumbaro:
Pamoja na hivyo, Nkamia ambaye kitaaluma ni mwandishi, amelizungumzia suala la kufungiwa kwa mwanasheria maarufu nchini Dk Damas Daniel Ndumbaro kama ni jambo linalishangaza na kusikitisha.
Nkamia ambaye ni Mbunge wa Kondoa Kusini anasema TFF imekurupuka na kutumia jazba katika suala hilo na ilifanya maamuzi baada ya serikali kuwa imeingilia na kuagiza TFF na klabu kukutana kupata mwafaka.
“Sijui hata nitumie neno gani ili nieleweke sahihi, nianze hivi; ninawaunga sana mkono TFF katika masuala ya maendeleo ya mchezo wa mpira hapa nyumbani.
“Lakini serikali haitawaunga mkono hata kidogo kwa kitendo kama hicho cha kumfungia Dk Ndumbaro. Kwanza wameonyesha walifanya mambo kwa jazba, walikirupuka na walitaka kutekeleza hilo.
“Wazungu wanasema a good listener is a good speaker (msikilizaji mzuri huwa msemaji mzuri). Hasira haziwezi kusaidia maendeleo ya mchezo wa soka nchini.
“Tayari sisi (serikali) tuliishangilia, tukawataka kukutana na baadaye kurejea kwetu. Kabla hata ya kukutana, wakafanya wanayojua, wakamfungia Dk Ndumbaro kwa miaka saba.
“Nilimsisitiza Malinzi kwamba wanapaswa kukaa na kulimaliza kwa mazungumzo, lakini ajabu haikuwa hivyo, sijui alinipuuza nilichozungumza naye, naona akaitisha kamati, mambo yakaenda haraka na Dk Ndumbaro akafungiwa.
“Miaka saba si kitu kidogo, adhabu hata ingekuwa kuna kosa kweli ni kubwa sana. Hawawezi TFF kufanikiwa kwa kuwa wanafungiana au kutisha watu hasa kwa wale wanaojaribu kurekebisha kunapokuwa kuna kosa.
“Nimesikia wanasema Dk Ndumbaro alimdhalilisha Rais wa TFF, wapi sasa! Kwani alikuwa anazungumza mwenyewe tu, alifanya hivyo kwa niaba ya klabu, hilo liko wazi kwa kuwa klabu zilionyesha kupinga hilo na utaratibu uliotumika. Maana yake wakati wanakaa, bado Dk Ndumbaro angekuwa upande wa klabu.
“Kumfungia kunaashiria nini, labda waliipuuza serikali! Kwanini wasingekaa na kumalizana, kuzungumza kunapokuwa na tofauti ndiyo jambo zuri, si kupeana adhabu kama hizo au kutishana. TFF hawajui tu, kufanya hivyo kunaweza kuwasababisha kukosa vitu vingine,” anasema Nkamia.

“Tuliwaambia baada ya bunge ambalo linaanza Novemba 4, tutakutana. Sasa tusichekeshe watoto kwa kuonekana ni watu tunaolumbana tu. Na itakuwa vizuri kwa TFF kurudi na kuiangalia hiyo adhabu kwa kuwa haina faida kwenye soka hapa nyumbani.”
Kuhusianiana na serikali kama inaweza kuwa na bajeti kwa ajili ya kusaidia soka la watoto na vijana, Nkamia anasema bado hawana bajeti ya kutosha.
“Serikali ina mambo mengi sana, kuna wakati inahitaji kusaidiwa mambo fulani. Lakini tunaamini tunafikia huko katika siku za usoni, ni suala la kulifanyia kazi na tumekuwa tukilijadili kwa kuwa tunapenda kuona vijana wanaendelezwa na ndiyo nguzo ya maendeleo yas michezo nchini,” anasema Nkamia na kuongeza.
“Lakini tayari nimezungumza na BMT na kuwataka kuandaa plani, kwamba tunaweza kufanya vipi katika kusaidia michezo na hilo litasaidia katika siku za usoni.
“Pia unaweza kuandaliwa mfumo maalum ambao utakuwa unachangiwa kwa njia mbalimbali lakini kwa makubaliano, si kulazimisha watu. Mfano Kampuni ya Bia ya TBLna Bakheresa wanajitahidi kuchangia michezo, hivyo tunawapongeza na tunaomba wengine pia wajitokeze.”
Serikali iliamua kuingilia suala hilo baada ya klabu kupinga kukatwa asilimia 5 katika fedha zinazopata kutoka Vodacom na Azam TV kwa ajili ya udhamini wa Ligi Kuu Bara.
Dk Ndumbaro ambaye pia ni Mhadhiri wa Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam (UDSM) na kile cha Huria (Out), akazungumza kwa niaba ya klabu za ligi hiyo, zikipingwa kukatwa fedha hizo na mwisho kusababisha serikali kusikia kilio cha klabu na kuliingilia suala hilo.
Serikali kupitia Waziri Nkamia ilifanikiwa kuzima zoezi hilo kwa kuwa klabu tayari zimelipwa fedha zao za udhamini kupitia Bodi ya Ligi Tanzania (TPL). Lakini ikasisitiza klabu na TFF kukutana.
Suala hilo ndiyo lilionyesha kuwaudhi TFF, ambao walimfungulia mashitaka kwenye kamati ya nidhamu ambayo iko chini yake, nayo ikatoa adhabu Dk Ndumbaro akiwa nje ya nchi ambako amepata mwaliko wa moja ya vyuo vikuu vya nchini Marekani.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic