WILLIAM LUCIAN 'GALLAS'.. |
Na Saleh Ally
KATIKA mechi ya Ligi Kuu
Bara iliyopigwa juzi Jumamosi jijini Dar es Salaam, ungeweza kuangalia mambo
mengi sana ambayo yanaweza kuwa burudani au mafunzo.
Kwanza kabisa ni idadi
kubwa ya mashabiki waliojitokeza na kuonyesha kuwa kweli klabu hizo mbili ni
kubwa, zimebeba furaha na majonzi ya watu na hakuna ubishi kuna kila sababu ya
kuhakikisha zinabadilika ili kuwaridhisha mashabiki na wanachama wao.
Wamejitokeza kwa wingi
sana, wameonyesha wanaziamini na kuzipenda, hilo ni deni kubwa na zinapaswa
kuwalipa kwa kuonyesha soka la uhakika na ushindi ili kuzifurahisha nyoyo zao.
Anayekupenda, mpende pia.
Lakini kuna somo
tunalolisubiri, maana kila mara kumekuwa na malalamiko ya uchakachuaji wa
mapato, hatujui ni klabu zenyewe, wadau wake au mashirikisho na vyama
vinavyosimamia, limekuwa ni jambo la siri.
Kwa kuwa juzi mashabiki
wamejitokeza kwa wingi sana huku tiketi za kielektroniki zikitumika na ndizo
zinazoaminika kwamba ni salama katika suala la mapato, sasa acha tusubiri.
Kweli mengi yalikuwa ya
kuangalia kama hayo ya mwanzo, lakini kubwa ni rekodi waliyoiweka Simba
kuwachezesha vijana saba katika mechi ngumu, wakitokea katika presha kubwa ya
sare tatu mfululizo, lakini wakathubutu kwa ajili pia ya soka ya Tanzania hapo
baadaye.
Simba ilianza mechi hiyo
ikiwa na wachezaji sita makinda, kati ya hao ni watano ambao wamelelewa katika
timu B hadi kufikia kiwango kizuri. Mchezaji wa sita, alikuwa ni kipa Peter
Manyika.
Waliokuwa Simba B na
walianza katika kikosi cha kwanza ni William Lucian ‘Gallas’, Hassan Isihaka,
Jonas Mkude, Haruna Chanongo na Saidi Ndemla.
Usisahau baadaye, Simba
ilimuingiza Ramadhani Singano ‘Messi’, hivyo kutimiza nafasi ya wachezaji
makinda saba katika dakika 90 dhidi ya Yanga ambayo haikuwa na mchezaji kinda
hata mmoja katika kikosi chake.
Listi ya Yanga iliyoanza
ilikuwa hivi; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’,
Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Geilson Santana ‘Jaja’,
Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho.
Wachezaji wote walioanza
katika kikosi cha Yanga ni wale waliojiunga na timu hiyo tayari wakiwa na
uzoefu wa ligi kubwa. Hakuna aliyekuzwa Yanga kisoka kama ambavyo ilikuwa kwa
Simba kwa makinda hao sita.
Lengo si kuonyesha Yanga
walikosea, lakini kuwafumbua macho hata wao kwamba falsafa ya kukuza vijana ina
faida yake. Hata kama si Simba iliyowaanzisha makuzi ya kisoka, lakini vijana
hao kuchipukia, wamepata nafasi wakiwa na Simba.
Kama Yanga itakuza vipaji,
Simba ikaendelea kufanya hivyo, kuna nafasi kubwa ya kutengeneza vijana wengi
waliokuzwa kiushindani, mwisho kutakuwa na wachezaji wengi wanaochuana
kusajiliwa na mwisho kuisaidia timu ya taifa kuwa na nafasi ya uchaguzi zaidi.
Tanzania haina wachezaji
wengi wanaocheza nje, hivyo timu ya taifa inategemea wengi wa nyumbani. Ili
ifanye vizuri pia inatakiwa kuwa na wachezaji bora wa hapa nyumbani na hakuna
ujanja, kuwakuza wachezaji sahihi ni lazima kujali vijana.
Mfano wa timu nyingi
zinazofanikiwa kupitia vijana upo, angalia Arsenal na Barcelona. Huenda Yanga
inakwenda kwa falsafa ya Chelsea ambayo kupitia makocha kama Jose Mourinho,
inataka watu wa ushindi na kuleta makombe.
Yote yanawezekana, lakini
bado kunatakiwa kubadilishwa kwa mfumo na wachezaji makinda wapewe nafasi kama
ilivyofanya Simba. Hakuna anayeweza kubisha kwamba walicheza vema na kuonyesha
uwezo wa juu.
Kutoa nafasi ni jambo zuri
kwa kuwa linatoa nafasi ya kugundua, kwamba waliopewa nafasi wanaweza kweli au
hawawezi kabisa ili utaratibu mwingine ufanyike. Wakiweza inakuwa faida na
makinda wa Simba wameonyesha.
Usisahau wakati Simba
inacheza, kwenye benchi kulikuwa na nyota wawili wa kimataifa. Amissi Tambwe na
Pierre Kwizera ambao sasa wanalazimika kupambana kupata namba.
Kama wameweza kucheza
vizuri kwenye mechi hiyo ya presha, maana yake wamekua kutokana na kujifunza
kitu na itawajenga kujiamini na kuweza kuwa huru kufanya mambo waliyonayo. Hiyo
ndiyo faida kwao, kwa klabu na taifa letu. Vijana wanaweza, wapeni nafasi.
Msisahau, bila ya nafasi, kipaji hakiwezi kuonekana.
So what!?
ReplyDelete