Na Saleh Ally
UKIFIKA kwenye Mji wa Lubumbashi nchini DR
Congo, Mbwana Samatta au Samagoal, ni moja ya majina makubwa kabisa na unaweza
kuyalinganisha na wanasiasa au matajiri kadhaa.
Samatta anaonekana ni mtu wa watu, mashabiki wa
TP Mazembe hauwezi ukawaeleza lolote nje ya Samatta, wanaamini ndiye
mshambuliaji bora wa kizazi cha sasa.
Inapofikia TP Mazembe inacheza ligi ya DR
Congo, si kazi ngumu Samatta kufunga mabao matatu au manne au akawa chachu ya
ushindi ya kikosi chake hicho.
Lakini michuano ya kimataifa, Samatta tayari
ameonyesha kwa misimu mitatu sasa kuwa yeye ni msaada mkubwa kwa TP Mazembe kwa
kufanya vizuri.
Karibu kila timu kubwa unayoijua ya Afrika
iliyowahi kutua Lubumbashi, yeye alitikisa nyavu zao. Samatta amezifunga Al
Ahly, Zamalek, Berekum Chelsea, Power Dynamos na Al-Merrikh.
Kuzifunga timu hizo ni uthibitisho kuwa
Mtanzania huyo ni kati ya washambuliaji hatari zaidi wa Afrika kwa kipindi hiki
kwa kuwa amezifunga karibu difensi ngumu au bora za Bara la Afrika.
Samatta ndiye mwanasoka anayelipwa zaidi kuliko
mwingine yeyote nchini. TP Mazembe katika mkataba wa sasa imekubali kutoa dola
10,000 (Sh milioni 17) kwa mwezi ili kupata huduma ya Samatta.
Tayari Samatta amefikisha miaka 22 sasa, maana
yake ni wakati mwafaka kwake kwenda kucheza nje ya Afrika, ikiwezekana Ulaya au
kwingine ambako kutakuwa na maslahi zaidi.
Ndiyo, TP Mazembe haiwezi kuwa timu ya mwisho
kwa mafanikio ya Samatta wakati inawezekana kuna baadhi ya washambuliaji wanaocheza
Ufaransa, Italia na hata Hispania na England, hawana kiwango cha Samatta.
Miaka 22, ndiyo wakati sahihi wa kuondoka DR
Congo na kwenda Ulaya au kwingine kwenye maslahi zaidi ili autumie vizuri muda
wake wa kuwa mmoja wa nyota barani Afrika.
Kwa mtazamo wa haraka, mshahara anaolipwa
Samatta ni mkubwa sana kwa Mtanzania, lakini ukizungumzia katika soka kwa
kiwango chake alichonacho sasa, ni kidogo sana.
Mwanasoka anayelipwa zaidi Afrika au
anayeingiza fedha nyingi katika soka ni Samuel Eto’o wa Cameroon ambaye kwa
mwaka dola milioni 90 (Sh bilioni 144) licha ya kwamba yuko Everton.
Fedha za Eto’o zimetokana na sehemu alizopita,
Real Madrid, Barcelona, Anzhi, Chelsea. Jina ni kubwa na kweli alionyesha
uwezo. Namba mbili ni Didier Drogba aliyerejea Chelsea akiwa na dola milioni 70
(Sh bilioni 112).
Jiulize Samatta anaingiza kiasi gani kwa jumla,
kama itakuwa ni dola 120,000 (Sh milioni 193) ambao ni mshahara wa mwaka. Kama
kutakuwa na posho na matangazo kidogo pale Lubumbashi, basi haiwezi kuzidi dola
200,000, hii ni fedha anayopata kwa wiki tu Yaya Toure ambaye hawafikii Eto’o
na Drogba kwa malipo ya mwaka!
Kwa uwezo na kiwango alichofikia Samatta,
unafikiri anastahili? Jibu sahihi ni hapana na huu ndiyo wakati mzuri kwake
kuamini anaweza zaidi ya hapo, atafute sehemu nyingine.
Kuna taarifa kuwa, kuna baadhi ya timu za Ulaya
zimekuwa zikimtaka, lakini TP Mazembe wanaendelea kutaka kumzuia kupitia bosi
wake Moise Katumbi ambaye anaridhishwa na kazi ya mshambuliaji huyo.
Bado Samatta anaweza kubaki kama rafiki au
kijana wa Katumbi, lakini akapata nafasi ya kuendelea zaidi na maisha yake kwa
kuwa hajafikia mwisho wa kiwango chake na anaweza kwenda zaidi ya hapo.
Hata kama utachukua 50 bora ya wachezaji
wanaolipwa, Samatta hawezi kuingia. Lakini ukichukua 10 bora ya washambuliaji
wakali na wanaosumbua kipindi hiki, hauwezi ukamuacha, hiki ni kipimo kingine
kwamba Samatta sasa anastahili kuondoka TP Mazembe na kwenda zaidi ya hapo.
Samatta ni Mtanzania, anaweza kuwa kama Watanzania
wengi, kuhofia kujaribu au kuridhika. Hali halisi inaonyesha anapaswa kupiga
hatua na huu ndiyo wakati. Angalia 10 bora ya wanaoingiza mamilioni zaidi
Afrika kwa mwaka:
1. Samuel Eto’o (dola 90m)
Anaelekea mwisho wa maisha yake ya soka lakini
bado thamani yake ni kubwa uwanjani.
2. Didier Drogba (dola 70m)
Memba wa kikosi cha dhahabu cha Ivory Coast
ambaye naye anaelekea ukingoni mwa soka lake. Anaichezea Chelsea.
3. Yaya Touré (dola 65m)
Kiungo wa Manchester City ambaye amevuna fedha nyingi kote
alikopita ikiwemo Barcelona.
4.
Emmanuel Adebayor (Dola 27m)
Jina lake ni kubwa katika nchi yake ya Togo,
amepita klabu nyingi lakini sasa ametulia Tottenham Hotspur.
5. Michael Essien (dola 25m)
Kiungo wa Ghana ambaye alipata sifa nyingi
alipokuwa Chelsea, kwa sasa anaichezea AC Milan.
6. Kolo Touré (dola 18m)
Beki wa Liverpool ambaye naye anaonekana kuwa
ukingoni mwa soka lake, lakini bado anaingiza mkwanja mzuri.
7. John Obi Mikel (dola 15m)
Jina la Mnigeria huyu siyo kubwa sana lakini
umuhimu wake ni mkubwa Chelsea na ndiyo maana bado yupo klabuni hapo.
8. Frédéric Kanouté (dola 12m)
Mkongwe wa Mali ambaye sasa anaichezea Guoan ya
Ubelgiji.
9. Seydou Keita (dola 10m)
Kiungo wa Mali anayeichezea Roma ya Italia kwa
sasa.
10. Christopher Samba (dola 8m)
Beki wa Congo ambaye aliingiza fedha nchini
England na Urusi, kwa sasa yupo Dynamo Moscow.
0 COMMENTS:
Post a Comment