YANGA imepata ushindi wake
mnono wa kwanza katika Ligi Kuu Bara ikiwa chini ya Mbrazili, Marcio Maximo,
baada ya kuichapa Stand United kwa mabao 3-0.
Mechi hiyo iliyopigwa juzi,
Yanga imefanikiwa kuitwanga Stand kwa idadi hiyo ya mabao kwenye Uwanja wake wa
nyumbani wa Kambarage mjini Shinyanga.
Kabla ya kukutana na Stand
United, Yanga ilikuwa imecheza mechi nne, ikiwa imeshinda mbili, sare moja na
kupotea moja. Unaweza kusema ilikuwa imepitia matokeo yote matatu ya soka.
Hata hivyo, safu yake ya
ushambuliaji haikuwa imefanikiwa kufunga mabao manne katika mechi zake nne
zilizopita, hivyo kuifanya kuwa na mabao manne ya kufunga katika mechi nne.
Wastani wa mabao manne
katika mechi nne si sahihi kwa timu unayoweza kuipa kipimo cha fowadi kali na
bora inayoweza kuitwa ni hatari.
Inawezekana Maximo alikuwa
katika hatua za mwanzo kuanza kuiimarisha safu yake ambayo ni mpya kwake,
lakini kuna sehemu alikuwa anakosea na majibu ameanza kuyapata.
Ushindi huo mkubwa wa mabao
3-0 dhidi ya Stand United umekuwa wa kwanza, lakini idadi ya mabao imeongezwa
na mchezaji aliyekaa benchi mechi zote nne za mwanzo. Huyo ni Jerry Tegete.
Huwezi kumlaumu Maximo kwa
Tegete, kwa kuwa ndiye alikuwa wa kwanza kumuamini na kumtumia hadi kwenye
kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars wakati huo alipokuwa kocha kabla ya
kurejea kwao Brazil.
Lakini safari hii,
alionekana kutomuamini katika mechi zote nne za mwanzo hadi alipofanya hivyo
juzi na Tegete akamuonyesha mwalimu wake huyo kuwa alimsahau kwa kufunga mabao
mawili.
Huenda Maximo alikuwa na
hofu iwapo atamuweka Jaja nje anaweza kuonekana alileta mtu ambaye si sahihi au
aliona kumpa muda mwingi wa kucheza kunaweza kumsaidia kuizoea ligi ya Tanzania
Bara, yote hayo yanawezekana.
Lakini sasa tayari amepata
jibu kwamba Tegete na Hussein Javu, kwa mpira wa Kibongo, wanastahili nafasi ya
kucheza hata kama itakuwa hivyohivyo ya kugawana.
Tegete na Javu waliingia
kipindi cha pili wakati Yanga inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Mbrazil
Jaja. Javu akatoa pasi ya bao la pili kwa Tegete ambaye baadaye alifunga la
pili kwake na la tatu kwa Yanga.
Tegete aliingia dakika ya
70, dakika ya 77 akafunga bao akiwa amecheza dakika 7 tu. Hii inaonyesha mchezaji
huyo ana uwezo mkubwa wa kutupia mipira kwenye nyavu, vema akapewa nafasi.
Mimi siwezi kusema Jaja hafai
kwa kuwa anaonekana ana sifa zote za umaliziaji hata kama alikuwa anaandamwa na
ukame wa mabao. Lakini inawezekana pia Tegete akawa msaada kwa Jaja kama ataona
kuna mshindani anayeweza kuifanya vizuri kazi yake yeye akizubaa.
Hivyo Maximo anaweza
kumtumia Tegete kumsaidia Jaja kama sehemu ya changamoto, pia Tegete ni msaada
kwa kuwa ana uwezo wa kufunga mabao mawili katika nafasi nne au tano
anazozipata.
Soka ni mchezo ambao
unajumuisha makosa, maana yake kila mmoja anaweza kukosea lakini jaribio la
Maximo kwa Tegete limefanya kazi. Javu naye ameonyesha anaweza kutoa mchango.
Hivyo hakuna haja tena kwa
Maximo kuhofia au kutaka kurudi nyuma huenda kwa kuhofia lawama kwamba Jaja
hafai au vinginevyo, badala yake aangalie maslahi ya Yanga kwamba inastahili
ushindi.
Jaja atakayepewa changamoto
ya Tegete aliye katika kiwango, anaweza kuwa bora zaidi kuliko akiwa na uhakika
wa namba kwa asilimia mia, kila siku.
Kitu kizuri zaidi kwa
Tegete, kama Maximo atazitoa nafasi hizo kwake, ana kila sababu ya kuonyesha
kwamba kocha huyo alikuwa sahihi naye ajitume badala ya kujisahau kama atarejea
na kuanza kuonyesha cheche.
0 COMMENTS:
Post a Comment