ZAIDI ya miaka 13 au zaidi
iliyopita nilizungumza na mmoja wa makipa maarufu nchini, nikamuomba kwenda
nyumbani kwake kufanya mahojiano kwa kuwa kipindi hicho alikuwa anacheza soka la
kulipwa nchini Shelisheli.
Manyika Peter alikuwa
amerejea mapumzikoni nyumbani kabla ya kurejea tena Shelisheli kwa ajili ya
kucheza soka la kulipwa.
Nilifika kwake Ilala jijini
Dar es Salaam, kabla ya kuanza mahojiano, alimuita mtoto wake, sikumbuki kama
alikuwa mtoto ambaye aliniambia, halafu nikazungumza naye kuwa anaipenda timu
gani, akaniambia na wote tukacheka.
Baada ya kusalimiana na
Manyika, nilizungumza na mkewe na baada ya hapo, wao walitupisha nikaanza
kufanya naye mahojiano kuhusiana na soka la Shelisheli na maisha nje ya
Tanzania hasa kwa mwanasoka yanavyokuwa.
Huna haja ya kujua
alichonieleza Manyika au baba Peter kama nilivyosikia anaitwa siku hiyo na
mkewe.
Lakini nimelazimika
kukumbuka nyuma baada ya kumuona kwa mara ya kwanza mwanaye Peter Manyika
akidaka katika mechi kubwa ya Simba dhidi ya Yanga akiwa ndiyo ana umri wa
miaka 18.
Hiyo ni rekodi mpya kwa
kipa mwenye umri kama wake, hasa ukizingatia nafasi ya kipa mara nyingi inakuwa
inaaminika inahitaji wazoefu zaidi angalau kuanzia miaka 25 kwenda juu.
Kinda huyo alipata nafasi
baada ya makipa wote wawili kuwa majeruhi. Ivo Mapunda na Hussein Shariff ‘Casillas’
ambao waliumia kwa nyakati tofauti mjini Zanzibar na jijini Johannesburg,
Afrika Kusini, Simba ilipokuwa kambi.
Simba kumpa nafasi ndiyo
jambo muhimu zaidi, kwa kuwa kulikuwa na uwezekano wa Mapunda kucheza kwa kuwa
alikaa kwenye benchi.
Viongozi wa Simba, hasa
benchi la ufundi chini ya Patrick Phiri wanastahili pongezi na huenda kwa kiasi
fulani jambo hilo linaweza kuondoa imani Friends of Simba (Fos) wamekuwa
wakimuingilia kocha.
Kama ingekuwa hivyo huenda
kungekuwa na ugumu sana katika kukubali kumpa nafasi kinda huyo aitumikie Simba
katika mechi ngumu na muhimu ambayo Simba ilikuwa inataka ushindi wa kwanza
kwenye ligi lakini katika mechi yake ya kwanza ya msimu dhidi ya watani wao
Yanga waliokuwa wameshinda mfululizo.
Huenda watu wataanza kujifunza
kuwa kuna haja ya kuwaamini vijana lakini kuna kila sababu ya kuwekeza kwenye
soka la vijana kwa kuwa ndiyo watakuwa wakombozi wa soka yetu baadaye.
Angalia Manyika ambaye
amepewa nafasi na moja kwa moja hakuichezea, badala yake aliicheza vizuri na
kwa ufasaha mkubwa kama kipa wa siku nyingi kwa kuwa alijiamini vilivyo.
Manyika amecheza kwa
kujiamini, ameonyesha ni tegemeo Simba na timu yetu ya taifa hapo baadaye na
anapaswa kuendelea kupewa nafasi zaidi ya hiyo ili kukiinua kipaji kingine
msaada kwa taifa letu.
Usisahau licha ya kwamba
alikuwa akiichezea Simba kwa mara ya kwanza katika mechi kubwa dhidi ya timu
kubwa kama Yanga, lakini ndiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza ya ligi.
Hakuwahi kucheza Ligi Kuu
Bara, hiyo ndiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza, halafu ikawa mechi yake ya
kwanza dhidi ya Yanga. Haukuwa mzigo rahisi kwake, ndiyo maana baada ya mechi
alibaki chini akisali kwa dakika kadhaa.
Hongera Simba kwa kumpa
nafasi, hongera kwake yeye kwa kuonyesha vijana ni mhimili na njia, kikubwa
hapaswi kuvimba kichwa badala yake anatakiwa kujituma zaidi kuhakikisha anafika
mbali zaidi ya hapo.
Mara baada ya mechi, wakati
anahojiwa, Manyika alisema baba yake ndiye silaha yake. Neno kubwa na
inaonyesha kiasi gani anathamini mchango wake na hiyo ni dalili kuwa akiendelea
katika njia sahihi, ana kila sababu ya kufika mbali zaidi.
Umemsahau kipa wa Coastal Union aliyewanyima sare Simba msimu uliopita pale uwanja wa Taifa akiwa na umri wa miaka 16 tuu!
ReplyDelete