SASA ni uhakika kwamba michuano ya Chalenji haitafanyika
mwaka huu baada ya waliokuwa waandaaji, Ethiopia, kuamua kujitoa kuandaa.
Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati
(Cecafa), limekuwa likihaha kupata mbadala baada ya uamuzi huo wa Ethiopia. Lakini
haikuwa rahisi, baraza hilo lilifanya juhudi ya kuwashawishi Sudan ambao
walikataa katakata kuandaa michuano hiyo.
Mashindano yalipangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu,
maana yake hakuna ujanja tena kwamba yanaweza kufanyika na taarifa zinaeleza
Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye amekuwa akihaha kuendelea kujaribu kuokoa
hiyo hali.
Wakati Musonye anahaha, nafikiri huu ndiyo wakati
mwafaka wa kuizungumzia Cecafa ambayo imekuwa ni kama genge la watu fulani kwa
kuwa inafanya mambo yake mengi kwa kubahatisha.
Cecafa naiita ni genge la watu kwa kuwa imekuwa
ikiongozwa na watu walewale wenye sura zilezile ambao hawana mawazo mapya,
wanataka kufanya vilevile na mwisho wao huwa ni kugawana tu fedha kwa faida ya
matumbo yao, kama ilivyo kwa viongozi wengi wa soka hapa nchini hasa kwenye
vyama na mashirikisho.
Cecafa inavyohaha kupata mbadala wa Ethiopia ambayo
imeamua kuachana na michuano hiyo ni dalili kuwa nchi au watu wameichoka
michuano hiyo. Utaona kimbilio la Cecafa kwa michuano yake ya klabu na timu za
taifa imekuwa ni Tanzania na Rwanda tu.
Kwingine wanaonekana kuchoshwa na michuano hiyo ambayo
unaweza kusema haina msaada wowote na soka la Afrika Mashariki na Kati, badala
yake ni sawa na mashindano ya urembo ambayo huandaliwa kwa kipindi fulani, watu
wakajipatia fedha za mlangoni na zile za wadhamini, halafu wakatokomea
kusikojulikana.
Jiulize katika fedha ambazo Cecafa wamekuwa wakiingiza
wao, kiasi gani kimekuwa kikitolewa kwa nchi husika kusaidia maendeleo ya soka
kwa kuwa baraza hilo ni la ukanda mzima?
Jiulize tena, lini Cecafa wamewahi kuweka mahesabu yao
hadharani kwamba wameingiza kiasi gani katika michuano fulani, hasa waweke wazi
mchanganuo kwamba fedha hizi zinatokea kwa wadhamini na hizi kwa viingilio vya
milangoni na shirikisho limepewa kiasi hiki au lilitumia kiasi hiki?
Bado unaweza kujiuliza, Musonye amekuwa katibu mkuu kwa
zaidi ya miaka kumi sasa. Yupo tu, mawazo ni yaleyale na nafasi yake inabaki
kuwa yake utafikiri mfalme kutoka katika nchi za Kiarabu!
Huwezi kumsikia akishiriki katika lolote kwenye
kuendeleza soka la nchi yoyote kwenye ukanda wetu. Mara zote anasubiri wakati
wa michuano hiyo kwa kuwa anajua ni sawa na mradi binafsi.
Kama ingekuwa michuano mikubwa na inayodhaminika kama
ile iliyo chini ya Baraza la Vyama vya Soka Ukanda wa Kusini mwa Afrika
(Cosafa), vipi haina wadhamini ambao wameingia mkataba angalau wa miaka mitatu
tu?
Kuna Rais Paul Kagame ambaye amejitolea kama kiongozi.
Lakini mashirika yanaonyesha hayana imani na Cecafa ambayo inaweza kubadili
rais pekee lakini viongozi wengine wakiwemo wa kamati ya utendaji wanaendelea
kubaki walewale tangu wakiitwa baba hadi sasa wameanza kuitwa kina babu.
Kama Cecafa ingekuwa na wadhamini wake ambao wana
mikataba minono kutokana na thamani na ubora wa mashindano, basi haingekuwa na
shida ya kuihamisha Ethiopia na kuipeleka kwingine. Wadhamini hawana imani nayo
na wengi wanaingia mkataba kwa mashindano ya msimu mmoja pekee.
Musonye asiendelee kujifanya kigogo, inabidi aanze
kukubali kuwa kuna tatizo ndani ya Cecafa, michuano isiyoisha mzozo kila msimu.
Halafu aanze kulifanyia kazi na kingine aangalie, kuendelea kung’ang’ania alipo
ni kuifanya Cecafa kuwa na mawazo ya kizamani katika dunia ya kisasa!
0 COMMENTS:
Post a Comment