Na Saleh Ally
BEKI Erasto Nyoni wa Azam FC alikumbwa na matatizo
makubwa sana, si vibaya kusema anapaswa kumshukuru Mungu na kusali zaidi kwa
kuwa amenusurika kifo.
Nyoni alipigwa kama mwizi, huenda kwa wale wanaochukulia
neno kupigwa kama ni jambo la kawaida, lakini Nyoni alishambuliwa na watu zaidi
ya 40 ambao walimkimbiza huku wakimpiga mfululizo.
Kumtetea ilikuwa haiwezekani, askari mmoja alijaribu,
akashindwa. Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto akiwa na mdau mwingine wa soka,
Mucky Zayumba pia waliingilia wakashindwa na wakatishiwa kupigwa, wakaacha.
GARI LA NYONI (KULIA), LIKIWA LIMEKWAMA BAADA YA KULIGONGA GARI LA GLOBAL PUBLISHERS INAYOMILIKI GAZETI BORA LA MICHEZO NCHINI LA CHAMPIONI. |
Madereva hao wa bodaboda waliokuwa wanampiga Nyoni kama
mwizi au jambazi anayetumia silaha, walikuwa wanafanya hivyo kwa kuwa tu
alimgonga mwenzao.
Nyoni alimgonga dereva bodaboda katika eneo la Tip Top,
Manzese jijini Dar es Salaam akiwa katika mizunguko yake ya kawaida jioni ya
Jumatatu iliyopita.
Inaelezwa awali alijaribu kusimama, lakini kundi la
madereva hao wa bodaboda waliofika pale walionekana hawana nia nzuri, walilenga
kumuumiza. Akachukua uamuzi wa kutimua mbio akipita sehemu mbalimbali ikiwemo Sinza
huku akiyagonga magari kadhaa.
Nyoni hakuwa kwenye akili yake vizuri, alichanganyikiwa,
alionekana alikuwa ni mwenye lengo la kuokoa maisha yake. Hivyo alikuwa tayari
kumgonga mtu yeyote, ili mradi ajiokoe.
Hata baada ya kumshika katika eneo la Kijitonyama baada
ya kuligonga gari la Global Publishers Limited, aliteremka haraka na kuanza
kuwaeleza kwamba hakimbii. Alitaka wazungumze ili aeleze ilivyokuwa hadi ajali
ikatokea na alitakiwa kufanya nini kama ni kulipa au kwenda polisi.
Haraka wakamvamia, wakaanza kumpiga, alianguka
alipoinuka tena alipigwa mfano wa kibaka ambaye amepatikana na kidhibiti.
Wakati wanampiga walisema ameua, lakini uchunguzi baadaye ukaonekana sivyo na
wale walisema vile ili kuonyesha wanachofanya ni sahihi.
NYONI (WA TATU KULIA) WALIOSIMAMA WAKIWA NA KIKOSI CHA AZAM FC. |
Hata baada ya Nyoni kukimbia, walirudi wakitaka kumpiga
abiria aliyekuwa kwenye gari lake. Jiulize yeye aliendesha, au apigwe kwa
sababu zipi? Wasamaria wema wakamuokoa kutoka kwa vijana wengi waliojijaza
jazba kwa makusudi na wengine wakiwa hawajui hata lililotokea, basi kwa kuwa ni
dereva bodaboda, anaona ni sahihi kumpiga kila dereva wa gari anapopata nafasi.
Hapa lengo si kumtetea Nyoni, lakini huenda umefikia
wakati Mwenyezi Mungu ametaka kuionyesha jamii ya Watanzania hatari inayokuja
mbele yetu kwa kuwa Nyoni ni mtu maarufu, amepigwa hivyo imekuwa ni rahisi
kujua kinachoendelea lakini watu wengi wamekuwa wakifanyiwa mambo hayo ya ajabu
na madereva bodaboda ambao sasa wamekuwa na nguvu kuliko serikali na wanachukua
hatua mkononi wanavyotaka wao.
Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na jeshi lake, lakini
Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga lazima ajue
kuna jambo la kufanya ili kuwahi kuepusha mauaji makubwa yanayoweza kutokea
siku zijazo.
Iwapo mtu amegonga, askari wa usalama barabarani wapo,
serikali inawalipa mishahara kutumia kodi ya wananchi na hiyo ndiyo kazi yao na
wao ndiyo wataalamu wanaoweza kung’amua, waachwe wafanye kazi yao. Sasa vipi
madereva bodaboda wawe ndiyo askari, mahakama na sheria?
Wanataka kumpiga kila aliyehusika na ajali ya mwenzao,
bila ya kujali kama mwenzao ana kosa au la. Hata kama aliyekosea ni dereva wa
gari, vipi wasisubiri askari wafike, au kweli alitaka kukimbia, wamzuie
akamatwe halafu aende kituoni, afunguliwe mashitaka na ikiwezekana mahakamani!
Madereva bodaboda wangapi wanafanya makosa makubwa
barabarani, mbona madereva wa magari hawaungani na kutaka kuwapiga? Jiulize
wapi kinakwenda kizazi cha bodaboda na mwisho wake ni upi!
Nimekuwa nawaza, kwamba kuna siku dereva mmoja wa gari
atakuwa amezingirwa anakaribia kuanza kupigwa na hana ujanja wa kujiokoa halafu
ana silaha anayoimiliki halali. Sijui atafanya nini?
Ajali zilikuwepo kabla ya kuwepo kwa rundo la bodaboda. Hakuwezi
kuwa na barabara kusiwe na ajali na hasa katika jiji kubwa kama la Dar. Kwa nini
wengine wawe na uwezo wa kuchukua sheria mkononi, nani aliye juu ya sheria kama
hata rais wa nchi hawezi kuwa hivyo.
Najua si madereva bodaboda wote wanafanya hivyo au
wanaingia kwenye mambo hayo ya kukurupuka, lakini wako wachache wanaharibu
taswira ya wengine ambao ni waelewa na hii ni kawaida katika jamii. Iko siku
wataingia kwenye matatizo makubwa, hawatasahau milele.
Kamanda Mpinga na timu yake hawapaswi kulipuuzia hili
jambo. Walifanyie kazi, ikiwezekana kutafuta fungu la kuanza kutoa mafunzo kwa
madereva bodaboda.
Ikiwezekana kuwaondolea kisaikolojia hisia kwamba wao
hawathaminiwi au wanadharauliwa, taswira ambayo naona kwa kiasi kikubwa imekuwa
ikijengwa kutoka mashariki kwenda magharibi bila ya utafiti wa kutosha.
Kamanda Mpinga, jambo hili si dogo, siku moja litaleta
maafa kwa kuwa kumbuka, hata madereva wa magari wana nguvu pia, siku watachoka
kuonewa, halafu itakuwa tatizo. Vizuri hili likafanyiwa kazi kwa njia nzuri ya
kufundishana, waandalieni kozi maalum, mkifundisha wachache, watafundisha
wenzao.
Lengo liwe ni kujenga Tanzania moja yenye amani, ubora
na watu wanaoheshimu kwa dhati sheria ikiwezekana, bila ya shuruti.
0 COMMENTS:
Post a Comment