Na Saleh Ally
HAKUNA mwenye uhakika kama
kweli Lionel Messi ndiyo anakwenda ukingoni au ni kipindi cha mpito na makali
yake yatarejea tena.
Pia hakuna mwenye uhakika,
Barcelona itaendelea kung’ara au taratibu inaendelea kutembea kwenye mteremko
wa “bye bye” ufalme.
Kikosi cha Barcelona
kimemtangaza Javier Mascherano kuwa mchezaji bora wa kikosi hicho kwa msimu
uliopita. Tuzo ambayo aliichukua Messi mfululizo miaka mitatu!
Wakati Messi anakosa tuzo
hiyo ya ndani ya Barcelona, kwenye Tuzo za La Liga, Barcelona na Messi wameonekana
kupwaya kupita misimu mingine yote kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano.
Real Madrid ndiyo
inaonekana kushika hatamu, inaonekana kuwa juu zaidi huku mpinzani mkubwa wa
Messi, Mreno Cristiano Ronaldo, akipiga ‘hat trick’ ya tuzo.
Ronaldo amekuwa Mchezaji
Bora, Mfungaji wa Bao Bora na Mshambuliaji Bora wa La Liga. Messi ameambulia
patupu pia.
Madrid imeendelea kutamba
kwa kutwaa zawadi nyingine tatu za Kiungo Bora (Luka Modric), Beki Bora (Sergio
Ramos) na Kipa Bora (Keylor Navas) ambaye ameshinda kutokana na kazi yake nzuri
msimu uliopita akiwa na Levante.
Barcelona ilichukua tuzo
tatu, Andrés Iniesta alitangazwa kuwa kiungo bora mshambuliaji, huku Ivan
Rakitic na Rafinha wakitwaa tuzo mbili za Fair Play na mchezaji aliyechipukia.
Utaona Barcelona imeondoka
kwenye zile tuzo tatu kubwa za La Liga, yaani mchezaji bora, kiungo bora, beki
bora au bao bora na imebaki kwenye Fair Play na mchezaji anayechipukia.
Barcelona ndiyo ilikuwa
ikitawala tuzo hizo kwa kiasi kikubwa. Lakini kadiri siku zinavyosonga, imeanza
kuonekana ya kawaida sana.
Si timu inayoogopeka tena
na kila kitu kinaonyesha mabadiliko ya makocha tokea Pep Guardiola, hadi
kufikia Luis Erinque, yanaweza kuwa chanzo na Barcelona inahitaji muda.
Kumalizika kwa kiwango cha
Xavi Hernandez ambaye sasa anaingia au hamalizi dakika 90, tayari kumetibua
ubora wa pembe tatu hatari zaidi duniani katika zote iliyokuwa ikiundwa na
Xavi, Iniesta na Messi.
Kazi kubwa kwa kocha
Enrique, lazima atengeneze kitu tofauti au kutengeneza pembe tatu nyingine
ambayo itamchukua muda.
Lazima mashabiki wa
Barcelona wakikubali kipindi hicho cha mpito. Wapo wanaoweza kuuliza kama
wamezama, ukweli kwa kipindi hiki unaweza kusema wanakaribia kuzama.
Lakini kwa kikosi
walichonacho, wakipata huo muda, wakaendelea taratibu na kuzoeana, wageni
wakazoea utamaduni wa uchezaji, basi Barcelona inaweza ikaibuka na kurudi
kwenye ubora uleule.
Angalia mechi ya El
Classico pale Bernabeu, Messi alikuwa haonekani, utafikiri alikuwa ‘likizo’.
Kuna jambo la kufanya kwake na kwa Enrique kwa kuwa Barcelona ya sasa, si ile
yenye makali na msisimko iliyokuwa tishio kwa kila mpinzani.
0 COMMENTS:
Post a Comment