HAMU yangu kubwa ilikuwa ni kuona kama kweli
uwezo wa Amissi Tambwe kufunga mabao umekwisha kabisa.
Niliingia kwenye ubishi mkubwa na mmoja wa
viongozi wa Simba wakati tukijadili taarifa za kutaka kuachwa kwa Tambwe.
Alinipa sababu nyingi ambazo kwa asilimia 90
niliona hazina msingi msingi na hasa aliponiambia Tambwe hakuwahi kuwatoka hata
mabeki wawili.
Badala yake amekuwa akifunga mabao yake kwa
kuvizia tu, nilimtolea mfano wa Ruud van Nisterlooy alivyoisaidia Man United
kutwaa ubingwa akifunga mabao hayo ya ndani ya 18.
Lakini nilimkumbusha kwamba nina ushahidi wa
picha za Tambwe akikimbizana mabeki wawili akiwa nje ya 18 na si kweli kwamba
alikuwa hana uwezo wa kumtoka beki hata beki mmoja.
Wakati mwingine kunaweza kukawa na taarifa, mchezaji akazushiwa kitu na kila mmoja akakipokea na kuona ni kweli hata bila ya kujiuliza au kuchunguza naye akawa anasambaza, mfano hilo kwamba Tambwe anasubiri kufunga tu, yupi mwenye uhakika?
Yule kiongozi alipoona hoja zangu zina nguvu, akahamia na
kunieleza ni mfumo wa Kocha Patrick Phiri ndiyo uliomkataa Tambwe na anaonekana
ameshindwa kuendana nao.
Lakini nilipozungumza na Phiri, akaniambia
hakuwahi kuwa na mpango wa kumuacha Tambwe na si lahisi kuona kocha akitaka
kumuacha mfungaji bora wa msimu uliopita, hata angekuwa majeruhi, labda aambiwe
hawezi kucheza msimu mzima!
Ingawa sijui mpira, lakini nilikuwa nina
maswali mengi sana kama kweli Tambwe hawezi tena kufunga na hasa juzi
nikiishuhudia Simba ikicheza dakika 90 dhidi ya Kagera Sugar bila ya kufunga
hata bao moja.
Lakini jana kwa mara ya kwanza Tambwe
akiichezea Yanga katika mechi ya ligi, alifanikiwa kufunga bao lake la kwanza
na la pili msimu huu.
Tambwe raia wa Burundi ameifungia Yanga bao ndani
ya dakika 7 tu akiwa anaichezea. Siku moja nyuma kama nilivyoeleza, Simba
hawakuweza kufunga hata bao moja.
Lengo langu si kulinganisha, au kuonyesha
lazima
Tambwe atafunga mechi zote zijazo, lakini hii inaonyesha kuna baadhi ya
mambo huwa hayaendi kitaalamu.
Hasa mambo ya kuamini kuliko hali halisi.
Kusema Tambwe hawezi kufunga kisa anasubiri au kuvizia tu, si sahihi hata
kidogo. Na uwezo wa Tambwe kufunga, hauwezi ukamalizwa na mfumo.
Hata ukiliangalia bao la kichwa alilofunga
dhidi ya Azam si lahisi kusema ni mfumo au mafunzo mazuri ya Kocha Hans van der
Pluijm, badala yake ni uwezo binafsi.
Ulikuwa ni mpira wa krosi ulioingia ndani na
Tambwe alichofanya ni kumzidi kasi beki wa Azam, akawahi na kuupiga kichwa. Bao
lake ndiyo lilisaidia kuirudisha Yanga mchezoni baada ya kuwa imefungwa katika
dakika ya tano tu baada ya uzembe wa Mbuyu Twite.
Simba ina haki ya kumuacha Tambwe, lakini ilipaswa kueleza sababu nyingine za msingi, si zile ilizozitoa. Nidyo maana bado ninaamini na huu ndiyo ukweli kuwa
Simba ilikurupuka kumuacha Tambwe au hata lengo la kumuacha halikuwa madhubuti
kulingana na sababu zilizotolewa.
Huenda ni matakwa ya wachache wenye sauti ya
kusema ndani ya Simba au wanaoamini kweli amekuwa akivizia, hakuwahi kumpita
beki, amekwisha, mzee na vinginevyo.
Inawezekana kabisa hata wao walipitisha
uamuzi huo baada ya kuambiwa wakaamini. Hakuna aliyefanya tathmini. Hata
angekuwa anavizia, lakini kama anafunga, basi ni jambo zuri. Kama havizii,
anakimbia sana na mpira, halafu hafungi, faida yake ni nini?
Kwangu Tambwe amenipa somo, niliposikia
ataachwa kwa mara ya kwanza. Nilijiuliza maswali mengi na moyo wangu ukakataa
lakini nikataka kujiridhisha kwa kurudia kuangalia baadhi ya mechi zake za
nyuma, bado sikukubaliana na nilichokiona.
Lakini baada ya bao lake la jana dhidi ya
Azam FC, nimeamini kuna tatizo na nalichukua kama somo.
Yoyote atakayetaka
kuungana nami tujifunze awe huru, atakayeona kilichofanyika ni sahihi, pia
sawa, kila mtu aamini kivyake.
0 COMMENTS:
Post a Comment