Na Saleh Ally
MECHI saba za mwanzo za
Ligi Kuu Bara kwa Simba zilikuwa na msukosuko mkubwa sana kutokana na mambo
kutokuwa mazuri.
Gumzo la kwanza zilikuwa ni
mechi sita za mwanzo ambazo timu hiyo ilitoka sare zote, likazuka suala la
Kundi la Ukawa ambalo zaidi lilitawaliwa na hisia za kishirikina.
Matokeo ya soka,
hayapatikani kwa kuamini ushirikina, badala yake maandalizi ya kutosha,
kumsikiliza mwalimu anayepaswa kuwa bora na ushirikiano wa kutosha uwanjani.
Baada ya mechi sita za sare
ambazo zilizua mengi kama uongozi wa Simba kufanya mazungumzo na Kim Poulsen
ikitaka kumleta kuchukua nafasi ya Patrick Phiri.
Usisahau, viungo watatu,
Shabani Kisiga, Haruna Chanongo na mkongwe mwingine Amri Kiemba walisimamishwa.
Mwisho waliondolewa, aliyebaki ni Kisiga ambaye ‘uhai’ wake Msimbazi unaonekana
ni wa mashaka hadi sasa.
Mechi moja kabla ya ligi
kusimama, Simba ilifanikiwa kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting na
kuamka morali huku Wanasimba wakiamini tabu imekwisha na maumivu sasa basi.
Kabla ya kurudi kwenye
ligi, Simba imecheza mechi tatu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, zote za
kirafiki.
Kwanza dhidi ya Express ya
Uganda, ikawa ni sare ya bila mabao. Halafu dhidi ya Yanga ambayo ilishinda kwa
mabao 2-0, furaha ikatawala na sasa ikaonekana Simba imeiva na sare sasa basi,
kosa la kwanza lakini pia wakaichapa Mwadui ya Jumhuri Kihwelo 3-1.
Simba imeweka rekodi mpya
ya kuwa timu ya kwanza nchini, kusajili wachezaji wake wageni wote kutoka
nchini moja. Wachezaji wake watano, wote ni raia wa Uganda.
Kuna mabeki, Joseph Owino,
Juuko Murishid, viungo washambuliaji, Danny Sserunkuma, Simon Sserunkuma na
Emmanuel Okwi.
Kwa wachambuzi wa mambo,
hofu ilitawala kuona Simba ikisajili Waganda wote, lakini uongozi ulisisitiza
ulichoangalia ni kiwango.
Inawezekana mengi
yakasemwa, lakini hili litakuwa ni kosa la pili la Simba kuwa na timu ndogo
ndani ya timu kubwa.
UGANDA:
Timu ndogo ya Waganda ambayo
kama itaamua kutengeneza kiota chake ndani ya kikosi hicho, lazima kitazua
mfarakano wa chinichini baina ya Waganda na Watanzania na kusababisha ‘matobo’
ya ndani.
Vigumu kwa sasa kukubali
kwamba kunaweza kuwa na tatizo, uongozi hauwezi kuliona hili kwa sababu hautaki
kuonekana umekosea. Lakini kiroho safi kabisa, hili litaisumbua Simba baadaye.
Litaisumbua kutokana na
tabia za Waganda na hii imekuwa ni kawaida. Utaona Okwi na Owino walivyochelewa
kurejea kambini mara ya kwanza.
Lakini utaona safari ya
pili namna Waganda hao walivyochelewa kwa mara nyingi na athari ipo hivi;
zamani alipochelewa Okwi na Owino, Warundi Amissi Tambwe na Pierre Kwizera
ambao walionyesha nidhamu ya juu, walikuwa wakiwahi sana.
Lakini sasa kama Waganda
wana tabia za kuambiana, basi wanapochelewa wote watano ni pengo kubwa kwa
makocha ambao wanataka kwenda na prpgramu zao.
MFUMO:
Mfumo wa klabu zetu si
mzuri, wachezaji wanaowaomba ruhusa viongozi badala ya makocha. Kocha hana la
kusema ingawa kiutendaji ndiye anakuwa muathirika namba moja.
Taarifa za kwamba al
manusura Simba ‘imwage’ Phiri mara tu baada ya kufungwa na Kagera zimezagaa.
Lakini bado utaona kuna makosa mengine hahusiki, nitafafanua.
Wakati Waganda wanapoingia
kambini wamechelewa, hakuna ubishi hawawezi kuwa fiti sahihi kama wale
walioanza mazoezi mapema kwa kufuata kilichotakiwa, mfano kufika kambini
mapema.
MORALI:
Kingine ni kuuwawa kwa
morali ya baadhi ya wachezaji. Kwamba wanapotakiwa kufika mazoezini, basi wale Wazalendo wanawahi kufika kama
ilivyotakiwa.
Halafu wageni ambao ni
Waganda wanafika wamechelewa huenda siku mbili kabla ya mechi. Halafu baada ya
hapo siku ya mechi, kama si wote basi angalau watatu wanaanza na wengine wako
benchi.
Wale baadhi Wazalendo,
wanalazimika kukaa jukwaani kabisa. Inawezekana ikawa ni ishu ya uwezo kweli,
lakini angalia kuhusiana na ukweli na suala la nidhamu.
Hii inajenga matabaka,
inasambaza chuki taratibu na mwisho ‘matobo’ ndani ya Simba na inaweza
kuwashangaza wengi kuona Simba inaanguka wakati ndiyo ina kikosi bora.
Angalia, Simba iliyoonekana
haina kikosi bora, ililaumiwa kwa sare mfululizo lakini haikuwahi kupoteza
mchezo.
Sasa ina kikosi bora chenye
wachezaji wa Uganda walio na uzoefu, imepoteza mchezo. Hapa kuna mengi ya
kujiuliza na uongozi wa Simba unapaswa kuyatilia maanani mambo ambayo
yanaonekana ni kama madogo lakini sivyo.
Inawezekana kabisa viongozi
wa Simba wakatumia nguvu nyingi kulazimisha ionekane si tatizo au haiwezi kuwa
tatizo.
Ushauri, walione hili ni
tatizo na kuanza kulishughulikia mapema kwa kuwa ligi ya sasa, si ya mwaka
jana, timu nyingi zimejiandaa, angalau zina Sh milioni 100 za Azam TV na
maandalizi yanaweza kuwa bora kuliko zamani.
Kingine, lazima uongozi wa Simba usisitize usawa kwa maana ya
nidhamu. Wale wachezaji Waganda wasitengenezewe daraja la juu utafikiri
hawaishi Afrika Mashariki.
Ubora wa watu watano katika
timu ya watu 28, hauwezi kukamilisha ubora wa kila kitu. Hivyo wanapaswa
kuamini wao ni sehemu ya timu na wanaunganishwa na ushirikiano wao na wenyeji.
Hakuna ubishi wala hadithi,
Waganda hao wanapaswa kuwaheshimu Watanzania, kuiheshimu Tanzania inayowapa maisha.
Hakuna kikosi au timu inayoweza kufanikiwa kama miongoni mwa wahusika, hakuna
heshima na upendo.
0 COMMENTS:
Post a Comment