Na Saleh Ally
NIANZE na kukumbusha baadhi ya mengi ambayo nimewahi kuzungumza,
kwamba soka yetu Tanzania imetawaliwa na mizengwe zaidi kuliko hali halisi.
Soka ni burudani, lakini soka ni biashara kubwa inayoweza
kulinganishwa na zile ghali kama za uuzaji mafuta au madini.
Hakuna anayeweza kukataa katika hilo, angalia katika mechi moja ya
soka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, zimewahi kuingia hadi Sh
milioni 700. Si mchezo, si kitu kidogo na si rahisi kutokea, biashara zenye
uwezo huo kwa muda mchache kama huo, ziko ngapi? Zitaje!
Nauchukulia mchezo wa soka kama ajira kubwa kabisa ambayo ingeweza
kuwakomboa Watanzania wengi na kuachana na kuamini kila mwenye maisha bora
lazima awe amekwenda shule na kupata digrii au ‘mastaz’.
Hata Ulaya haiko hivyo, wachezaji wanalipwa mamilioni ya fedha
kuliko hata maprofesa, huo ni mfumo mzuri wa mgawanyo wa ajira, waliosoma na
wasiosoma lakini wenye vipaji vyao, nao wanaweza kuishi maisha bora.
Viongozi wengi wa soka nchini kuanzia kwenye Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), klabu kubwa kama Yanga, Simba na nyinginezo si wale wanaotaka
maendeleo, wenye mawazo au mipango endelevu.
Viongozi hao ndiyo wamekuwa wakiua nguvu ya mchezo wa soka na kuugeuza
kutoka ule unaoweza kutengeneza mamilioni kwa ajili ya wahusika na maendeleo ya
taifa letu kwa jumla, hadi kuwa mchezo wa chuki, malumbano.
Lakini wachezaji nao, wanaamka, wanaliona hilo. Wanaweza kubadilika
na kuachana na kuamini ushirikina? Wanaweza kupunguza hadi kuondoa chuki ya wao
kwa wao?
Hebu angalia tukio hili lililotokea kule Ujerumani, mshambuliaji
Mario Gotze wa Bayern Munich amekitoa kiatu chake kimoja tu cha mguu wa
kushoto, kimeuzwa kwa euro milioni 2 (Sh bilioni 4.2).
Kiatu hicho aina ya Nike ndiyo kiliugusa mpira mara ya mwisho wakati
Gotze alipopiga shuti na mpira kujaa wavuni, likawa ndiyo bao pekee wakati
Ujerumani ilipoiangusha Argentina kwa bao 1-0 katika fainali ya Kombe la Dunia.
Gotze ambaye hakuwahi kukisafisha kiatu hicho tangu fainali,
alikubali fedha ziwasaidie watoto kupitia mradi wa 'A Heart for Children',
lakini hakuna aliyejua kitafikia bei hiyo.
Sasa kitasaidia watoto, hii ndiyo nguvu ya soka. Angalia, kiatu
kinauzwa kwa fedha zaidi ya gari la kifahari, zaidi ya jumba la kifahari, zaidi
ya thamani ya mishahara ya wachezaji wote wa Ligi Kuu Bara ikiwezekana kwa nusu
au msimu mzima!
Fedha hizo kama zingeletwa hapa nyumbani, Yanga na Simba wangeweza
kupata uwanja. TFF ingeweza kujenga uwanja mwingine na kupata fungu la kukuza
watoto wenye vipaji, si kama vile ilivyotaka kuchukua asilimia 5 za fedha za
wadhamini za klabu.
Mchezo wa soka uko hivi, unavyozidi kuuthamini na thamani yake
inapanda. Ujerumani wamejiandaa vema, wana programu nzuri ya vijana. Matunda
yao ilikuwa ni kuendelea kufikia kwenye Kombe la Dunia.
Gotze amefunga kwa kuwa wamefika Kombe la Dunia, kiatu chake
kimeuzwa bei kubwa kwa kuwa wako kwenye mashindano makubwa kama hayo. Jiulize
wamefikaje? Jiulize wangetanguliza majungu, ushirikina, ulafi wa fedha za
mashirikisho au klabu, wangefika hapo?









Watu wakitumiwa taaabu kwelikweli!
ReplyDelete🔥🔥
ReplyDelete